Prime
Siku 15 za moto ziara ya Wasira mikoa ya Ruvuma, Geita, Mwanza

Muktasari:
- Siku 15 za ziara yake, Wasira ameibua hoja mbalimbali ikiwemo kurusha vijembe kwa wapinzani, huku akikutana na changamoto kadhaa za wananchi katika baadhi ya maeneo aliyopita huko wilayani.
Mwanza. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira anaendelea na ziara yake ya kukagua uhai wa chama ambao amezungumza na viongozi na wanachama katika mikoa mitatu ya Ruvuma, Geita na Mwanza.
Wasira alianza ziara yake Juni 10, 2025 mkoani Ruvuma ambapo alitembelea wilaya zote za mkoa huo, kisha akaelekea Geita ambako nako alizungumza na viongozi na wanachama wa CCM, na sasa anaendelea na ziara hiyo mkoani Mwanza.
Siku 15 za ziara yake, Wasira ameibua hoja mbalimbali ikiwemo kurusha vijembe kwa wapinzani, huku akikutana na changamoto kadhaa za wananchi katika baadhi ya maeneo aliyopita huko wilayani.
Baadhi ya hoja alizokutana nazo kutoka kwa wananchi ni pamoja na kushushwa kwa bei ya gesi ya kupikia ili kuwapa unafuu wa kutumia nishati safi. Pia, hoja ya katika ziara hiyo, Wasira anawahamasisha wanachama kuchagua viongozi bora ambao wakienda kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, basi chama hicho kipate ushindi wa kishindo na kuendelea kutawala nchi hii.
Kilio gesi ya kupikia
Akiwa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, mkazi wa wilaya hiyo, Chimwaga Chimwaga alimweleza kuhusu gharama kubwa ya gesi ya kupikia, hivyo aliiomba Serikali kushushwa bei ya gesi ili wananchi wa kipato cha chini wanufaike na nishati hiyo badala yake wenye kipato pekee.
Hoja hiyo iliungwa mkono na mkazi mwingine wa Tunduru, Ally Jumbe ambaye ni mkulima, akisema pamoja na kero hiyo, changamoto nyingine wanayokumbana nayo ni kukosekana kwa skimu za umwagiliaji zenye ubora.
Hadija Kombo, mkazi wa Tunduru, naye hakubaki nyuma, alilalamikia suala la rushwa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru na wananchi kudharaulika wanapofuata huduma. Alikiomba chama kutoa maelekezo kwa viongozi wa Serikali ili tatizo hilo litatuliwe.
Alisema wanapokwenda hospitali kutafuta tiba, wanadaiwa fedha na hata wanapoandikiwa dawa huambiwa wakanunue nje huku wazee wenye vitambulisho vya matibabu bure wakitekelezwa wanapofika hospitali.
Akijibu kero ya huduma za afya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza Marando alikiri uwepo wa changamoto hizo, akisema watumishi wanaokula rushwa, tayari wamefukuzwa kazi na juhudi za kuboresha huduma kwenye hospitali hiyo zinaendelea.
Akiwa Mkoa wa Geita, mkoa wenye wachimbaji wengi wa madini, Wasira amewataka wananchi kuitumia ardhi yao yenye madini kujinufaisha, akiwashauri wasiiuze kwa wanaojiita wawekezaji bali waingie nao ubia.
“Tuna changamoto ndogondogo katika uchimbaji wa madini, kuna watu wenye ardhi yenye madini, sheria inasema ukitaka hilo eneo lazima mzungumze na mwenye ardhi na mkubaliane, kama mwenye ardhi hataki fidia au kutoka, basi wakubaliane,” alisema.
Kijembe kwa Chadema
Akiwa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Wasira alidai kwamba mgogoro uliopo ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanachama wake, ndiyo uliosababisha kupatikana kwa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Wasira alisema Chadema haipaswi kutafuta mchawi, bali yenyewe ndiyo mchawi kutokana na kunyima wanachama wake fursa ya kugombea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
Alisema Chadema imekuwa na kaulimbiu nyingi ikiwemo No reforms, No Election (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) na No hate, No fear (Hakuna chuki, hakuna hofu), lakini walipofanya uchaguzi ulionekana kujawa na chuki.
“Walipofanya mikutano yao ilijawa na chuki na walipomaliza, chama kikasambaratika, kila mtu akachukua virago vyake. Freeman Mbowe, mwenyekiti mstaafu, Tundu Lissu, mwenyekiti wa sasa, akachukua virago vyake, sasa hawapo pamoja na ndiyo wamesababisha kujulikana kwa chama kinachoitwa Chaumma,” aliongeza.
Wasira alisema Chaumma sasa kinaongozwa na waliokuwa wanachama wa Chadema na Mwenyekiti wa Chaumma Taifa, Hashim Rungwe, anafurahia hali ya chama hicho.
“Wanachama wao wanawaambia mturuhusu tukagombee ubunge, wao wanasema mna uchu wa madaraka na wanaosema mna uchu wa madaraka ni vijana wadogo wadogo, Tundu Lissu (Mwenyekiti wa Chadema) ameshakuwa mbunge miaka 10.
“Pia Godbless Lema, amekuwa mbunge miaka 10, wakati wao wanagombea hawakuwa na uchu wa madaraka, hawa watu ni wabinafsi na ndiyo wameifanya chama kimesambaratika, kwa hiyo watafute mganga wa kugangua chama chao,” alisema.
Sababu ya CCM kuaminika
Katika ziara yake wilaya za wilayani Songea, Madaba na Nyasa mkoani Ruvuma, Wasira alieleza sababu mbalimbali za chama hicho kuendelea kuaminika na kudumu madarakani, ikiwemo majukumu yake ya kuwatumikia Watanzania.
Miongoni mwa majukumu aliyoyataja Wasira ambayo alisema CCM inasimamia, ni kudumisha umoja miongoni mwa watu, kuleta maendeleo kwa wananchi, kusimamia amani ya Taifa pamoja na uhuru.
Miongoni mwa mambo ya maendeleo yaliyofanyika nchini aliyoyataja kiongozi huyo ni ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Daraja la JP Magufuli, ununuzi wa ndege mpya na ukamilishaji wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Julius Nyerere (JNHPP).
Mbali na miradi hiyo, alisema amani, usalama na mshikamano baina ya wananchi ni miongoni mwa mambo yaliyoiwezesha CCM kuaminika.
Wasira alisema kwa miaka minne ya Rais Samia, hali ya kisiasa na uhuru wa kutoa maoni umeimarishwa kupitia falsafa ya 4R (Maridhiano, Kujenga Upya, Ustahimilivu na Mabadiliko) chini ya Rais Samia.
Kupitia maridhiano hayo, Wasira amesema vyama vya upinzani vimepewa nafasi ya kufanya mikutano ya hadhara, kuandamana na kurejea nchini kwa viongozi waliokimbia, huku vyombo vya habari vikiwa huru.
Mbali na hayo, Wasira ameeleza ukomavu wa CCM kwenye siasa unaoifanya kutoyumba au kufa kama vyama vingine vya ukombozi Afrika Mashariki, akitolea mfano chama cha KANU cha Kenya.
Wamejipanga kwa uchaguzi
Akiwa Mbinga mkoani Ruvuma, Wasira alisema CCM imejipanga kwa uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu na tayari kimempitisha Rais Samia kuwa mgombea urais na Dk Emmanuel Nchimbi akiwa ni mgombea mwenza, wote wakitarajiwa kupeperusha bendera ya chama hicho.
CCM ni miongoni mwa vyama 18 vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu mwaka huu, Chadema ikiwa ni chama pekee nchini ambacho hakitashiriki uchaguzi huo kwa sababu kinasimamia ajenda yake ya kuzuia uchaguzi huo kupitia kaulimbiu yao ya “No reforms, no election”.
Chadema hakikusaini fomu ya maadili iliyotolewa na Msajili wa Baraza la Vyama vya Siasa, kitendo ambacho kinawaweka pembeni katika uchaguzi huo kama kanuni za maadili ya uchaguzi huo zinavyoelekeza.
Kuelekea uchaguzi huo, Wasira alisema hakuna kauli ya mifarakano itakayokubalika, akihimiza Watanzania kushiriki uchaguzi Oktoba mwaka huu kwani hakuna mtu anayeweza kuuzuia kwa kuwa unafanyika kwa mujibu wa Katiba.
Wasira alisema CCM iko tayari kukosolewa pale inapokiuka kanuni za utawala bora.
“Nawaambia chama chetu kinasimamia amani na kipo tayari kukosolewa ikiwa tunakiuka kanuni za utawala bora. Lakini wao wanaotukosoa tunawashauri wasitumie njia haramu kuvuruga amani na kuvunja haki za wengine,” alisema.
‘Chagueni wanaokubalika’
Ukiwa ni msisitizo wa kauli zake tangu alipoanza ziara yake, Wasira, akihutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Katoro mkoani Geita, alisema hatua ya kuongeza idadi ya wapiga kura za maoni ndani ya chama inalenga kupata wagombea wanaoendana na matarajio na mahitaji ya wananchi.
Alisema kuongezeka kwa idadi ya wapigakura ndani ya chama ni kuondoa uwezekano wa watu kupeana rushwa, akisisitiza mtu yeyote anayetaka kugombea kwa kutoa rushwa asigombee bali afanye uwekezaji kwenye kilimo.
“Tunataka wagombea wanaopendwa, wanaokubalika na ambao wananchi wenyewe wanawahusudu kwa utendaji wao. Ndiyo maana kura za maoni mwaka huu zitakuwa za kina na za wazi kwa wanachama wengi zaidi kushiriki ili kutoa maamuzi yao,” alisema Wasira.
Kauli kama hiyo pia ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu, ambapo katika hotuba yake aliwaasa wananchi kuchagua mgombea anayekubalika, mwenye uwezo wa kusaidia wananchi, na si kwa misingi ya makundi au rushwa.
Hoja hiyo ilihimizwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicolaus Kasendamila akisema tayari chama hicho mkoani hapo kimewaandaa wananchi kwa ajili ya uchaguzi mkuu na wapo tayari kupiga kura.
“Niliwaambia viongozi wajitahidi kuleta wagombea wazuri, tulianza mwaka jana na hakika walifanya hivyo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, tukashinda,” alisema.
Moses Ngonyani, mkazi wa Nyasa, alisema kauli ya makamu mwenyekiti huyo imetoa mwanga wa wananchi kumpata kiongozi atakayewatumikia na sio kutumikia matumbo yao.
“Kauli hii kwetu inatupa matumaini kwamba kiongozi tutakayempata awe diwani au mbunge ni yule tunayempenda na si aliyetoa fedha nyingi kwa wananchi kwa wajumbe,” alisema.
Balozi wa CCM, shina namba nane katika kata ya Masumuni, Wilaya ya Mbogwe, Rehema Kasudi alisema kazi yao ni kuhakikisha chama hicho kinawapata wagombea wanaokubalika na sio wenye fedha.
Alisema kama CCM itaendelea kuwajali kama ilivyowanunulia baiskeli mwaka huu, wataendeleza ushirikiano wao kuhakikisha wananchi wanapata viongozi bora.