CCM: Hatutakata majina Uchaguzi Mkuu Oktoba

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM Wilayani Sengerema mkoani Mwanza leo Juni 24.2025.
Muktasari:
- Kwa wale ambao hawatateuliwa kugombea nafasi ya ubunge na udiwani, watasubiri awamu nyingine.
Sengerema. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, hakuna mgombea atakayekatwa jina lake bali watateuliwa wale wanaokubalika na wananchi pekee.
Chama hicho kimewasisitiza wajumbe wake kusikiliza sauti ya wananchi na kutowapitisha watu ambao hawakubaliki na wananchi, hususan wale wanaotumia fedha kupata madaraka.
Kauli hiyo ilitolewa jana jioni Juni 24, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira, wilayani Sengerema mkoani Mwanza katika mkutano wa hadhara wenye lengo la kukiimarisha chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
“Kazi iliyobaki kwa CCM baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuvunja Bunge Juni 27, 2025 ni kuendesha utaratibu wa kupata wagombea wa nafasi za ubunge.
Wanachama wetu wanaotaka ubunge ni wengi, lakini tunahitaji mgombea mmoja kwa kila jimbo, hivyo tutawachuja, hatutawakata, tutawateua, tofauti kati ya kukata na kuteua ni kwamba ukikata unakata kwa hasira, lakini ukiteua unaangalia uwezo wa mtu kwa wakati,” amesema Wasira.
Wasira amesema kwa kuwa wagombea ni wengi, wale ambao hawatateuliwa na chama hicho watasubiri awamu nyingine, kwani wengi wao ni vijana.

Kuhusu nafasi ya urais, Wasira amesema anaamini Rais Samia atachaguliwa tena kuongoza kwa miaka mingine mitano si kwa sababu ya zawadi, bali kutokana na uwezo wake aliouonyesha.
“Sio kwamba amesimamia ujenzi wa madaraja na miradi mikubwa tu kwa Wilaya ya Sengerema pekee, amejenga shule mpya tano za msingi na madarasa 236, Sekondari 17 mpya zimejengwa pamoja na madarasa 124.
"Pia, Hospitali mpya moja, vituo vya afya vitano na zahanati 12 zimejengwa, hatua ambayo imesogeza huduma karibu na wananchi,” amesema Wasira.
Awali, akimkaribisha Makamu Mwenyekiti huyo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Nganga amesema kutokana na miradi iliyotekelezwa wilayani humo, Rais Samia atapata ushindi wa kishindo.
Ameongeza upo mradi wa maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni tano ambao utaondoa kero ya maji, huku changamoto ya umeme kukatika katika ikiwa mbioni kumalizwa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Mark Makoye amesema wilaya hiyo ina majimbo mawili ya uchaguzi Buchosa na Sengerema.
Alibainisha kuwa Jimbo la Sengerema lina kata 26 na Buchosa lina kata 21, na zote zimefikiwa na shughuli za maendeleo, huku asilimia 100 ya miradi ikiwa imetekelezwa.
“Kuna miradi ambayo ilikuwa imesimama, sasa imekamilishwa, ikiwemo mradi wa maji wa Shilingi bilioni 13 uliopo Kagunga, ambao kwa sasa unatekelezwa,” amesema Makoye.
Ziara ya Wasira wilayani Sengerema inahitimisha mfululizo wa mikutano ya ndani na baadhi ya mikutano ya hadhara aliyoifanya kiongozi huyo katika mikoa mitatu tangu Juni 10, 2025.
Makamu huyo alianza ziara mkoani Ruvuma kwa siku nne, kisha akaelekea mkoani Geita na kuhitimisha ziara yake mkoani Mwanza, ambako alishiriki hafla ya uzinduzi wa Daraja la JP Magufuli lililozinduliwa Juni 19, 2025, na Rais Samia.