Shonza aeleza sababu wananchi Songwe kumchagua Rais Samia mwaka 2025

Muktasari:
Mbunge wa Viti Maalumu, Juliana Shonza amesema kitu pekee ambacho wananchi wa Mkoa wa Songwe watakifanya kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo katika mkoa huo ni kumpa kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Amesema Rais Samia amefanya miradi mingi iliyoufungua Mkoa wa Songwe na wananchi wanapaswa kutofanya makosa kwa kuwa Rais Samia ameonesha kuwa anatosha katika nafasi hiyo kupitia kazi zake anazozifanya katika kila sekta.
Ameeleza hayo katika mkutano wa hadhara kueleza utekelezaji wa Ilani ya CCM uliofanyika katika mji mdogo wa Mlowo na kuhudhuriwa na mbunge wa Mbozi, George Mwanisongole.
Mbunge huyo ametaja baadhi ya miradi ambayo itaifungua Songwe kuwa ni ujenzi wa barabara ya Mlowo-Kamsamba yenye urefu wa kilometa 50 kwa kiwango cha lami.
“Wote mtakubaliana nami kuwa wananchi wanapata shida sana barabara yetu ya Mlowo-Kamsamba magari ni mabovu ukitoka Kamsamba inabidi ubebe nguo za kubadilisha ukifika Mlowo. Tumepiga sana kelele kuhusu barabara hii lakini tunasema mama (Rais Samia) yupo kazini, barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami,” amesema mbunge huyo.
Amesema kuwa barabara hiyo ikikamilika itakuwa mkombozi kwa wananchi kiuchumi kwani pamoja na wananchi kusafiri kwa urahisi, lakini watasafirisha vitu vyao ikiwemo mazao kwa urahisi.