Samia ataka Bahi, Manyoni wajiandae kutumia fursa za SGR
Muktasari:
- Ujenzi wa SGR awamu ya tatu unaendelea ukihusisha kipande cha kutoka Makutopora, Dodoma hadi Tabora, chenye urefu wa kilomita 294.
Manyoni. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Bahi mkoani Dodoma na Manyoni mkoani Singida kujiandaa kunufaika na fursa zitakazoletwa na mradi wa reli ya kisasa (SGR) itakayopita katika maeneo yao.
Samia ametoa wito huo kwa nyakati tofauti alipotembelea majimbo ya Bahi na Manyoni, ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake ya kampeni za kuomba kura kwa wananchi, ili aendelee kuiongoza Serikali.
Ujenzi wa SGR awamu ya tatu unaendelea ukihusisha kipande cha kutoka Makutopora, Dodoma hadi Tabora, chenye urefu wa kilomita 294.
Akiwa Bahi, Samia amesema kutakuwa na kituo cha treni hiyo ya kisasa na pia itajengwa bandari kavu, hivyo mji huo utakuwa kutokana na fursa nyingi zitakazoletwa na reli hiyo.
"Hayo yote yatakwenda kuvutia uwekezaji hapa Bahi, biashara zitakua, vitaanzishwa viwanda, hivyo ajira nyingi zitazalishwa. Niwaombe mjiandae kunufaika na fursa hizi na sisi tutaendelea kuwatengenezea mazingira wezeshi ili muweze kufanya shughuli zenu," amesema Samia.
Mgombea huyo ameongeza kwamba anatambua baadhi ya wananchi waliopisha mradi wa SGR hawajalipwa fidia zao, amewahakikishia kwamba uhakiki unafanyika na utakapokamilika, watalipwa stahiki zao.
Akiwa Manyoni, Samia amesema mradi wa SGR utapita Singida, hivyo kutakuwa na fursa nyingi za ajira na uwekezaji, amewataka wananchi kuchangamkia fursa hizo ili kujiletea maendeleo.
"Reli ya SGR itapita hapa hapa Singida, hivyo itatengeneza fursa za ajira na uwekezaji utafunguka. Jiandaeni kuzitumia fursa hizo ambazo zinaletwa na Serikali yenu," amesema mgombea huyo.
Mbali na hilo, Samia ameahidi kuboresha usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia mradi wa kuimarisha mawasiliano unaotekelezwa na Ucsaf, ili kuwapa wananchi usikivu mzuri wa vyombo vya TBC.
"Tutajenga kituo cha kurushia matangazo ya TBC katika mji wa Itigi ili kuwapa usikivu mzuri wananchi wa Singida," amesema Samia huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wake wa kampeni kumsikiliza.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, mgombea ubunge Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo ameomba kutekelezwa kwa miradi ya maji ili kuwasaidia wananchi wake ambao wanatumia maji ya chumvi.
"Nimesomasoma ilani ya uchaguzi, kuna mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria, mradi huo utapita hapa. Tunaamini kwamba na sisi hapa tutanufaika," amesema Nollo huku akishangiliwa na wananchi.
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Manyoni, Dk Pius Chaya ameishukuru Serikali kwa kutoa Sh800 milioni kwa ajili ya fidia kwa wananchi, shughuli ambayo tayari imefanyika.
"Katika mradi wa maji katika miji 28, Manyoni ni moja ya maeneo yaliyo katika mradi, tunaamini kwamba ukikamilika wananchi wetu watapata maji ya uhakika," amesema Samia.