Prime
Rungwe atoa kauli muasisi wa Chaumma kujiengua

Muktasari:
- Jina la Kabendera ni kati ya manane ya waanzilishi wa chama hicho kilichosajiliwa Juni 2012 na kupata usajili wake wa kudumu mwaka 2013
Dar es Salaam. Wakati aliyekuwa mmoja wa waasisi wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Eugene Kabendera akitangaza kukihama bila kutaja jukwaa analokwenda, mwenyekiti wa chama hicho, Hashimu Rungwe amesema kila jambo na wakati wake.
Jina la Kabendera ni kati ya manane ya waanzilishi wa chama hicho kilichosajiliwa Juni 2012 na kupata usajili wake wa kudumu mwaka 2013.
Leo, Jumanne Mei 27, 2025, ametangaza kuondoka kwenye chama hicho kwa kile alichodai kimepoteza misingi ya uanzishwaji wake baada ya kuwapokea baadhi ya wanachama kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ingawa wanachama hao wapya wanatajwa kukiingiza chama hicho kwenye neema ya fedha, lakini Kabendera amesema kulingana na falsafa zao, watakuwa wapinzani na watarudisha nyuma sera yao ya kupigania mabadiliko ya Watanzania.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo, Rungwe amesema kabla ya uamuzi wa kuwapokea mamia ya makada kutoka Chadema, aliwashirikisha viongozi wenzake wote wa chama hicho, lakini Kabendera hakujulishwa.
“Niliwashirikisha viongozi wenzangu nilipopata taarifa ya awali juu ya ujio wao, kwa kuwa walikuja na mapendekezo ya kuhitaji baadhi ya nafasi za juu ndani ya chama niliwaeleza na wakakubali kuachia nafasi zilizokuwa zinahitajika.
“Kabendera kama muasisi sikumjulisha kwa sababu hakuwa mwanachama hai tangu Septemba 2024 aliposusa baada ya kuteuliwa kuwa msemaji wa chama, toka hapo alikaa kimya alikuwa hajishughulishi na chama kila jambo na wakati wake aende tu,” amesema Rungwe.
Kulingana na Rungwe, pamoja na kuwa muasisi, lakini hakuona haja ya kumshirikisha wakati wanachama wapya wanahamia kwao kwa sababu hakuwa hai na mchango wake ulikuwa hauonekani.
Akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam, leo, Kabendera amesema kukengeuka misingi waliyokuwa wanaisimamia tangu kuanzishwa kwake miaka 13 iliyopita ni sababu iliyomsukuma kukihama.
“Kumekuwa na tofauti kubwa ya kimtazamo kuhusu uelekeo wa sasa wa chama na siasa za nchi yetu, ambao kwa maoni yangu hauendani tena na misingi na maono yaliyotufanya tuiasisi Chaumma.
“Nimefikia uamuzi wa kujiondoa ni uamuzi wa kimaadili unaotokana na kutimiza uadilifu wangu wa kisiasa na kuwa na utumishi wa kweli kwa umma wa Watanzania na dunia nzima,”amesema.
Amesema hata kundi lililohamia ameona litakuwa kikwazo na kushindwa kutekeleza ajenda zao, hivyo ameona bora kujiweka pembeni kuliko kuendelea kubaki na kuwa mpinzani ndani ya chama.
“Msimamo wangu umekuwa huo, kama watu wanakuja kukinzana na ajenda iliyopo, shari ya nini? Nimejiondoa umma utasema na nitaangalia jukwaa lingine,” amesema.
Kabendera amesema ingawa kwa sasa hatangazi kujiunga na chama kingine chochote, anajipa muda wa kuangalia jukwaa lingine litakalokuwa linaenda sambamba na maono yake kwa Taifa la Tanzania.
“Nitaendelea kushiriki maisha ya kisiasa Tanzania kwa uadilifu mkubwa kwa kuzingatia dhamira ileile iliyokuwa inaniongoza, naondoka Chaumma nikiwa na moyo wa shukrani kwa wote tuliopambana kwa miaka 13,” amesema.
Kabendera aliyewahi kushika wadhifa wa msemaji wa kwanza wa chama hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Tanzania Bara amesema historia yake anajua haiwezi kufutika kulingana na kazi alizozifanya lakini ni wakati wa kuandika sura mpya kwa misingi ileile ya haki, utu na uadilifu.
“Huu ni ujumbe na taarifa yangu niliyofikiria kwa kina nikiongozwa na misingi ile ile wakati tunaanzisha Chaumma ya kutaka kwenda kutatua matatizo ya Watanzania,” amesema.
Kabendera amesema kwa muda mrefu walikuwa wanapigania kuona demokrasia ikitendeka na si kutamkwa mdomoni pekee katika kuhakikisha Watanzania wanajua haki zao kwa kushiriki chaguzi za huru na haki.
Wakati akieleza hayo, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano, Uenezi na Taarifa kwa Umma, Ipyana Njiku amekiri kada huyo alikuwa miongoni mwa waasisi wa chama hicho.
“Ni kweli kuwa Kabendera ni miongoni mwa waasisi wa chama chetu, na ni kweli aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara mpaka Septemba 29,2024 yalipofanyika mabadiliko ya kiutendaji tangu hapo alikuwa kimya,” amesema.
Amesema sababu ya kuwa kimya na kushindwa kujihusisha na shughuli za kichama ni baada ya kuteuliwa kuwa mkuu wa idara ya habari na taarifa kwa umma uteuzi ambao hakuridhika nao.
“Baada ya ziara ya kichama mkoani Mbeya, kamati kuu ilikaa Mjini Mbeya na kuziba nafasi hiyo ili shughuli za chama ziendelee kwa kumteua Ipyana Njiku na kuthibitishwa katika nafasi hiyo tangu Februari 25,2025,” amesema Njiku.
Njiku amesema wameona barua yake hiyo ambayo imesambazwa mtandaoni, lakini kwa sasa chama hicho kinamtakia kila jema huko aendako.
“Chaumma kwa sasa kimewekeza nguvu zake zote kwenye tukio kubwa la uzinduzi wa Operesheni Chaumma 4 Change (C4C) itakayofanyika Mwanza Juni mosi, 2025,” amesema