TLP wamchagua Rwamugira kugombea urais 2025

Muktasari:
- Rwamugira amechaguliwa kwa kupigiwa kura 51 na kuwashinda washindani wake Wilson Elias aliyepata 47 na Neema Nyerere aliyepata kura sita kati ya kura 103 zilizopigwa na wajumbe
Dar es Salaam. Mkutano Mkuu wa TLP umemchagua Katibu Mkuu wake, Yustas Rwamugira kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Rwamugira amechaguliwa kwa kupigiwa kura 51 na kuwashinda washindani wake Wilson Elias aliyepata 47 na Neema Nyerere aliyepata kura sita kati ya kura 103 zilizopigwa na wajumbe.
Mwanamke huyo anatarajiwa kupeperusha bendera ya chama hicho huku mgombea mwenza wake akiwa ni Aman Seleman Mzee.
TLP inaungana na vyama vingine 10 vilivyoteua wagombea wao wa urais mapema na kusubiria wagombea hao kusubiri uteuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Katibu Mkuu wa TLP, Yustas Rwamugira (kushoto) ambaye amechaguliwa kuwa mpeperusha bendera wa chama hicho kwa nafasi ya urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu 2025.
Vyama vingine vilivyopata wagombea urais ni CCM, SAU, AAFP, Ada-Tadea, NLD, CCK, NCCR Mageuzi, UPDP, NRA, Demokrasia Makini na ADC.
Vyama ambavyo havijapata wagombea ni CUF, UDP, ACT Wazalendo, Chaumma, UMD na DP.
Licha ya TLP kumpata mgombea katika uchaguzi huo uliokuwa chini uangalizi wa watendaji kutoa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, washindani wawili waliojitosa kwenye kinyang'anyiro hicho wanadai uchaguzi huo haukuwa huru na haki.
Malalamiko ya Elias na Neema, wote wakiwa ni wafanyabishara nje ya nchi, wanadai utaratibu uliotumika haukuwa huru na haki kwani kulikuwa na wajumbe mamluki walioingizwa kwa ajili ya kupiga kura.
Akizungumza leo Jumatatu Mei 26, 2025 baada ya ushindi huo, Rwamugira amesema amewaahidi wajumbe hatowaangusha kikubwa wamuombee kwa kuwa, dhamira ni kuleta mabadiliko ya maisha kwa Watanzania.
“Nawashukuru wajumbe kwa kunipa imani kubwa kwa kunipigia kura katika uchaguzi huu uliokuwa huru na haki, mmefanya uamuzi sahihi kwa mustakabali wa uhai wa chama chetu hasa katika hatua iliyo mbele yetu,” amesema.
Rwamugira ameongeza kwamba pamoja na kuvuka hatua hiyo, bado wanalo jukumu kama chama kujipanga kwa kuandaa sera shindani ili kukabiliana na wagombea wa vyama vingine.
“Tukibweteka tutakuwa tumejimaliza, tunataka kwenda kushindana na si kushiriki ili tukawakomboe Watanzania wanaopitia magumu kutokana na sera zisizotabirika,” amesema mgombea huyo.

Wakati akieleza hayo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, aliyeongoza jopo la watendaji kutoka Ofisi ya Msajili, amesema mchakato wa uchaguzi huo ulikuwa huru na haki ingawa katika kinyang'anyiro chochote hayakosekani malalamiko.
“Asiyekubali kushindwa si mshindani. Nawapongeza walioshinda, kikubwa unganeni na kuwa pamoja na walioshindwa kukijenga chama chenu na kufuata taratibu za nchi yetu,” amesema Nyahoza.
Nyahoza amewataka walioshindwa kuacha kulalamika, bali wanapaswa kutumia fursa ya kukosa kwao kujipanga upya wakati ujao.
Amesema hata malalamiko yanatolewa na wadaiwa hayana mashiko kwakile wagombea hao muda mwingi wanaishi nje ya nchi ilikuwa ngumu kwao kuleta ushindani dhidi ya katibu mkuu hushinda na wajumbe wake.
Malalamiko ya walioshindwa
Akizungumzia mchakato wa kumpata mgombea, Elias amesema haukuwa huru na haki huku akiituhumu ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kusababisha hali hiyo kwa kile alichodai iliingiza wajumbe mamluki katika uchaguzi huo.

“Ofisi ya msajili ilituma watu kuwa waangalizi lakini katika hali ya kawaida wapigakura walikuwa wajumbe 103, katika hao nimepata kura 46, Neema kura sita, na Yustas kapata kura 52,” amesema.
Amesema awali, walipewa taarifa kwamba kulikuwa na wajumbe mamluki waliokuwa wameingizwa na ndiyo walienda kumpigia kura Katibu Mkuu.
“Mzee alitakiwa kupata kura 39, lakini chakushanga, Ofisi ya Msajili imebariki kwa kumaanisha matokeo ya uchaguzi huu kura zilikuwa za mfukoni,” amesema Elias.
Amesema baada ya matokeo hayo, amebaini kwamba vyama vya upinzani ni vyama vya mfukoni na ili uweze kupata haki labda uanzishe chama chako.
“Najuta, nimetumia hela zangu nyingi, kwanza kulipia pango la ofisi na kusaidia uendeshaji wa uchaguzi huu. Nimegundua leo kwamba hivi vyama ni vya mfukoni, naenda kutafakari kujua uamuzi wa kuchukua,” amesema.
Kwa upande wake, Neema amesema anaona kama mchakato haukuwa sawa ingawa alikuwa anaamini wangeruhusu mabadiliko kwani shabaha yao ilikuwa nzuri, kuboresha maisha ya Watanzania.
“Tulikuwa na dira ya kukijenga chama ili kiweze kushiriki ipasavyo siasa, nasikitika sana nilikuwa na imani kupitia jukwaa hili, tungeweza kuwaletea Watanzania mabadiliko makubwa lakini wajumbe wameamua kurudi kulekule,” amesema.
Neema amesema ameishi nchi za watu, ameshuhudia walivyopiga hatua licha ya kuwa na uchache wa rasilimali na wanafanya makubwa.
Hata hivyo, mwenyekiti wa chama hicho, Richard Lyimo amesema amefarijika kuona uhuru umetamalaki kwenye mchakato kwa wajumbe wote waliojitokeza.
“Ingawa kulikuwa na sintofahamu kwa mwenzetu kuonekana hawakubaliani na matokeo, lakini ndiyo hivyo, wajumbe wameamua, ni muhimu kama chama tudumishe umoja wetu kuelekea uchaguzi mkuu,” amesema.
Lyimo amesema anajua utendaji kazi wa Yustas, aliyechaguliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika mbio za urais, na ni matumaini yake ataonyesha ushindani unaotakiwa.
“Yustas ni kijana niliyempika mwenyewe na amepikika, bado tunaenda kumuongezea madini ili muda ukifika, akizungumza na kumwaga sera, basi wananchi wamchague,” amesema Lyimo.