Mfanyabiashara ajitosa kuwania urais kupitia TLP

Muktasari:
- Kada huyo wa TLP anakuwa wa kwanza kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho baada ya pazia la watia nia wa chama hicho kufunguliwa rasmi tangu Aprili 25, 2025 na linatarajiwa kufungwa Mei 29, 2025.
Dar es Salaam. Kada wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Wilson Elias amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Elias ambaye ni mzaliwa wa Tanga, anakuwa kada wa kwanza kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho baada ya pazia la watia nia wa kufunguliwa rasmi tangu Aprili 25, 2025 na linatarajiwa kufungwa Mei 29, 2025.
TLP, wako kwenye mchakato wa kutafuta mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho, wakiungana na vyama vingine vya ACT Wazalendo, CUF, ADC na Chaumma vilivyo katika mchakato huo.
Vyama ambavyo vimekamilisha mchakato huo na kuwapata wagombea wake ni pamoja na CCM, AAFP, NLD, UDPD na SAU.
Elias ambaye ni mfanyabiashara nje ya nchi, amejitokeza kuchukua fomu hiyo makao makuu ya chama hicho, Magomeni na kukabidhiwa na Katibu Mkuu wa TLP, Yustas Rwamugira, hafla iliyohudhuriwa pia na makada wa chama hicho.

Akizungumza Dar es Salaam leo Mei 8, 2025 baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, Elias amesema lengo la kuwania nafasi hiyo ni kuwatumikia Watanzania.
“Kipaumbele changu ni kuinua uchumi wa kila Mtanzania kwa sababu nimebobea eneo hilo, nimezunguka mataifa mbalimbali na nimejionea wenzetu wamepigaje hatua kwa kugusa nyanja zote hadi mwananchi wa chini kabisa, nahitaji kuondoa umaskini,” amesema.
Amesema umaskini kwa Watanzania bado ni janga linalohitaji jitihada za ziada licha ya Serikali iliyopo madarakani kufanya kazi kiasi, lakini inahitaji mawazo mapya katika usimamizi wa rasilimali zilizopo.
“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na raslimali nyingi kama madini na sasa mkoani Mbeya yamegundulika madini ya helium ambayo ni muhimu, yanatakiwa kusimamiwa ili yamnufaishe kila Mtanzania,” amesema.
Katika hotuba yake, pia, amezungumzia mpango wake wa kuja na mkakati sahihi na thabiti wa teknolojia ya kumaliza tatizo la maji linalolalamikiwa na Watanzania hususan kwenye jiji la Dar es Salaam.
“Nimezunguka mataifa kama Misri na mengine yaliyopitiwa na bahari na zile Falme za Kiarabu, kuna kitu ‘Disalination Plant’ ni teknolojia inayovuna maji ya bahari kwa ajili ya matumizi ya kawaida majumbani ni jambo ambalo hata hapa Dar es Salaam tunaweza kulifanya,” amesema.
Amesema kufanya hivyo na kuweka teknolojia hiyo mikoa mingine iliyopitiwa na habari utakuwa suluhu ya kuondokana na changamoto ya uhaba wa maji ya kutegemea mito, ambayo maji yake si ya uhakika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Rwamugira amesema dirisha la kuchukua fomu bado liko wazi na makada wao waendelee kuchukua fomu ambapo mkutano mkuu utakaojumuisha wajumbe 190 kutoka nchi nzima utakapofanyika watawachuja.
“Mkutano tunategemea utafanyika baada ya kuvunjwa Bunge la Tanzania, leo amekuja kada huyu kuchukua fomu lakini bado wengine wanne wameonyesha nia ya kuitaka nafasi ya urais kupitia chama chetu,” amesema Rwamugira.
Rwamugira amesema kuanzia Jumatatu ofisi yake itakuwa bize kutoa fomu hizo huku akieleza katika uchaguzi wa safari hii wanaenda kushindana na si kushiriki.
“Tumechoka kuwa oyaoya, katika mchujo tunataka kupata mtu mwenye sifa na uwezo na anayejibeba kwanza mwenyewe kabla ya chama kutia nguvu zake,” amesema Rwamugira.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho, Richard Lyimo amesema hataki kugombea nafasi ya urais isipokuwa nguvu zake amewekeza kwenye ubunge katika jimbo la Vunjo.
“Nahitaji kurudi bungeni, nimeona walioko wanatupeleka siko, wananchi wa Vunjo wamenifuata kama kiongozi na mkombozi wao nami sina hiana, safari hii naingia mazima Vunjo, ni nyumbani nilikozaliwa, siwezi kuwaangusha,” amesema Lyimo.