Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia aagiza majengo ya CCM yatumike kusikiliza kero za wananchi

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa CCM mara baada ya kuweka jiwe la msingi, kuashiria kuzindua rasmi ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya CCM, katika hafla iliyofanyika eneo la Tambuka reli, jijini Dodoma, litakapojengwa jengo hilo.

Muktasari:

  • Chama cha CCM wameanza mchakato wa ujenzi wa jengo la makao makuu wa CCM, jijini Dodoma huku Rais Samia Suluhu Hassan akitoa maagizo.

Dodoma. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi katika uzinduzi wa jengo la makao makuu ya CCM, huku akiagiza ofisi za chama kutumika kusikiliza kero za wananchi na kuzifikisha Serikalini zipatiwe ufumbuzi.

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatano, Mei 28, 2025 katika eneo la Tambukareli jijini Dodoma.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Samia amesema baada ya kukamilika kwa jengo hilo, siyo litatumika kwa kazi za utawala pekee, bali ni alama nyingine isiyofutika ya uimara, umoja na utambulisho wa chama hicho ndani na nje ya nchi.

Amesema kuwa litakuwa jengo la kisasa litakalobeba taswira si tu ya ukubwa wa chama, bali pia nafasi yake ya kuongoza taifa la Tanzania, pamoja na kuwa miongoni mwa vyama vikubwa barani Afrika, hususan katika eneo la Kusini mwa Afrika.

Aidha, Rais Samia amewakumbusha viongozi wenzake, hususan vijana wa CCM, kwamba mafanikio ya chama hayategemei tu kuwa na jengo la kifahari lenye mapambo mazuri ya dari na sakafu, bali yanatokana na utendaji bora wa chama wenyewe.

Amesema jengo hilo linalojengwa, pamoja na majengo ya mikoa na wilaya, ni sehemu muhimu ambayo wanachama, hasa vijana, wataitumia kwa ajili ya kujifunza, kujijenga katika uongozi na maadili.

Pia, amesisitiza kwamba majengo hayo yatatumika kama vituo vya mikutano, mijadala, tafiti, mafunzo na uamuzi wa kisera ili kuhakikisha CCM inaendelea kusimama imara, kuonekana, kusikika na kuheshimiwa.

Aidha, amewataka viongozi na wanachama wote wa CCM waendelee kujitolea na kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wabunifu ili kuimarisha chama.

Ameeleza umuhimu wa viongozi kuwa karibu na wanyenyekevu mbele ya wananchi, kwa sababu wananchi ndio wamiliki halisi wa chama.

Rais Samia amekumbusha kwamba Ilani ya Uchaguzi inaweka wazi wajibu wa viongozi kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi.

Hivyo, amehimiza viongozi kutumia ofisi za chama pia kuwasikiliza wananchi na kufikisha kero zao serikalini ili ziweze kutatuliwa.

“Ndugu viongozi na wanachama wenzangu wa CCM, kupitia mradi huu chama chetu kinafungua sura mpya ya makao makuu, nasi sote ni sehemu ya mafanikio haya,” amesema. Amewataka pi wanachama na wapenzi wa CCM kuchangia kwa hiyari gharama za ujenzi wa ofisi hizo.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema uamuzi wa kujenga jengo hilo la ghorofa tano umetokana na ndoto ya waasisi wa chama mwaka 1977, baada ya kuundwa kwake. Alifafanua kuwa mazungumzo ya awali juu ya ujenzi wa makao makuu yalianza mwaka 1983, na eneo lililochaguliwa lilikuwa Chimwaga, Dodoma.

“Mchakato huo ulichukua muda mrefu, lakini hatimaye mwaka 1992 makao makuu ya chama yalijengwa Chimwaga. Baada ya tafakari ya kina, wazee wa chama waliona elimu ni jambo la msingi, wakaamua sehemu ya makao makuu ibadilishwe kuwa sehemu ya miundombinu ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),” amesema.

Dk Nchimbi amesema ilichukua muda mrefu kufikia uamuzi mpya, lakini Juni 26, 2024, Kamati Kuu ya CCM iliwasilisha mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa juu ya umuhimu wa kujenga jengo hilo jipya.

Kikao cha Juni 30, 2024, cha NEC kilikubali hoja hiyo na ramani iliyopendekezwa.

Dk Nchimbi amesema Rais na Mwenyekiti wa CCM, alielekeza jengo lijengwe kwa kasi ili likamilike kabla ya jubilei ya miaka 50 ya CCM mwaka 2027.

Amesema ujenzi huo unakadiriwa kugharimu Sh34.13 bilioni na tayari Sh8 bilioni zipo mkononi, fedha ambazo zimetokana na mapato ya kampuni za chama hicho kwa asilimia 100.

“Kwa miaka miwili, makampuni haya yamelipa mrabaha wa Sh37 bilioni na kwa jumla katika miaka hiyo miwili, tumetoa Sh42 bilioni,” amesema katibu mkuu huyo.

Kampuni hizo zimeajiri watu 100 ambao wanapata kipato kupitia ajira hizo.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema Rais anaweka historia kwa kukidumisha chama na kuweka anwani ya kudumu.

Ametoa wito kwa wanachama kushirikiana kumpongeza kwa kazi hiyo itakayochochea maendeleo ya kudumu.

Uwekaji wa jiwe la msingi ni sehemu ya shughuli zizazoendelea kufanywa na CCM kuelekea  Mkutano Mkuu wake utaoanza kufanyika kesho Alhamisi na kuhitimishwa Ijumaa Mei 30, 2025, katika Ukumbi wa JK Convention Center, jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla mkutano huo maalumu utakuwa na agenda tatu kuu.

Amezitaja kuwa ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya 2020–2025 kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), pamoja na mabadiliko madogo ya Katiba ya Chama.

Mkutano huo umetanguliwa na kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu Chamwino jana, kikiongozwa na Rais Samia.

Leo Jumatano, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM watakutana katika Ukumbi wa NEC, White House, Dodoma chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Rais Samia.


Hali ilivyo mtaani:

Barabara nyingi za jiji la Dodoma zimepambwa kwa mabango yanayowakaribisha wajumbe wa mkutano mkuu, yakionyesha picha za wagombea urais wa CCM, Rais Samia na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi zikiwa na kaulimbiu ya chama: kazi na utu.

Pia picha za mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi, zimewekwa katika mabango mbalimbali jijini humo.

Wagombea hawa ambao watapeperusha bendera ya chama katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, walipitishwa na Mkutano Mkuu uliofanyika jijini Dodoma, Januari 18–19, 2025. Katika makao makuu ya chama, mabasi ya CCM yaliyowabeba wajumbe wa mkutano huo mkuu maalumu yameanza kuwasili.

Kwa upande wa malazi, wapangaji wa nyumba katikati ya jiji wameombwa kuziachia kuanzia leo ili kupisha wajumbe wanaoanza kuwasili.

“Mimi nimekuja tangu juzi; wahudumu wamenieleza kwamba kesho (Mei 29, 2024) nitafute mahali pengine kwa sababu vyumba hivi vimeshachukuliwa na CCM, watakaa hadi Mei 31, 2025,” amesema mgeni mmoja mjini hapo.

Mkutano huo unatarajia kushirikisha watu 2,700, wakiwamo wajumbe 2,000 na wageni waalikwa 700.