Prime
Vikao CCM kuibuka na mrithi Dk Nchimbi?

Muktasari:
- Macho na masikio yako Dodoma vinakofanyika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM vinavyotajwa kuamua mrithi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi aliyeteuliwa mgombea mwenza wa uraia.
Dar es Salaam. Swali kuu miongoni mwa wadau wa siasa, makada na wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ni nani atakayeteuliwa kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, inayoshikiliwa kwa sasa na Dk Emmanuel Nchimbi?
Swali linaibuka kutokana na uwezekano wa Dk Nchimbi kuachia wadhifa huo ili kupata fursa ya kujiandaa kikamilifu na majukumu ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kufuatia uteuzi wake kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa mitazamo ya wachambuzi wa siasa, huenda isiwe rahisi kwa CCM kuendelea kumwacha Dk Nchimbi katika nafasi hiyo nyeti, hasa ikizingatiwa atakuwa na majukumu makubwa ya kampeni, hivyo chama kitahitaji kumpata mrithi atakayesimamia utendaji wa chama.
Hali hiyo inajitokeza wakati chama hicho kikuu nchini kimeitisha vikao vyake vya juu – Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vitakavyofanyika kuanzia kesho, Jumatatu Mei 26 hadi Mei 28, 2025, ambavyo ndivyo pekee vyenye mamlaka ya kupendekeza, kupokea na kuidhinisha jina la katibu mkuu wa CCM. Vikao hivyo, vitafuatiwa na Mkutano Mkuu wa CCM Mei 29 na 30.
Hata hivyo, Mwananchi lilipomuuliza Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla iwapo vikao hivyo vitahusisha uteuzi wa katibu mkuu mpya, amesema hiyo si miongoni mwa ajenda za vikao.
"Hilo la Dk Nchimbi si miongoni mwa ajenda za vikao," amesema Makalla.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia anaweza kushtukiza kama alivyofanya huko nyuma kwenye nafasi mbalimbali za watendaji wa chama.
Kiongozi mwandamizi wa CCM aliyeomba jina lake lisitajwe ameliambia Mwananchi kuwa: “Kwa hatua ya sasa na miezi iliyobaki, lolote linaweza kutokea, mwenyekiti anaweza kumleta katibu mkuu mpya au Emmanuel akaendelea.”
“Lakini hofu yetu, ikiwa ataendelea Emmanuel, ukifika wakati wa michakato ya uchaguzi kuna kaugumu fulani, anakuwa mgombea mwenza huku katibu mkuu, kwa hatua ya sasa kuna hitajika katibu mkuu mpya ili aanze kazi mapema,” amesema.
Hata hivyo, Januari 19, 2025, Rais Samia alisema pamoja na Dk Nchimbi kuteuliwa mgombea mwenza, bado angeendelea kutumikia nafasi yake ya katibu mkuu, ingawa hakueleza hadi lini.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Msigani, Dar es Salaam, Reihad Chikando amesema ni vigumu kutabiri yajayo kwa chama hicho kwa kuwa kina taratibu zake za ufanyaji kazi na kuamua mambo yake, tofauti na vyama vingine.
Amesema chama hicho kinaweza kuteua mrithi wa Dk Nchimbi au kikaliacha hilo kwa ajili ya baadaye.
"CCM bwana haitabiriki, inaweza kukuletea jambo nyakati usizotarajia. Kwa hiyo ni mawili ama imteue mrithi au isimteue," amesema.
Hata hivyo, amesema kama uteuzi utafanyika anatarajiwa kupatikana mwanasiasa mwenye uwezo wa kustahimili mikikimikiki ya siasa ngumu kwa kuwa hiki ni kipindi cha kampeni.
Amesisitiza anahitajika kiongozi mwenye uwezo wa kuzungumza na kuongoza katika nyakati muhimu na asiwe na malengo binafsi kisiasa zaidi ya kuhakikisha ushindi wa CCM.
Kauli ya Chikando haiku mbali na ya mwanazuoni wa sayansi ya siasa, Dk Revocatus Kabobe aliyesema kwa nyakati zilizopo CCM inahitaji mtendaji mkuu atakayefanana na Dk Nchimbi si sura, umri wala kimo, bali kwa kaliba, haiba, tabia, misimamo na utu wake anapokuwa majukwaani na hata pembeni.
Sambamba na sifa hizo, Dk Kabobe amesema mrithi huyo anapaswa na historia ya kushiriki katika shughuli za chama kwa muda mrefu na kuwahi kushika nafasi za juu ndani ya CCM au Serikali, akionyesha uwezo wa kusimamia na kutekeleza ilani ya uchaguzi.
Amesema mrithi huyo anapaswa kuwa na uwezo wa kuongoza taasisi kubwa, kupanga mikakati ya kisiasa na kuhakikisha utekelezaji wake kwa ufanisi.
"Awe na uwezo wa kujenga mshikamano ndani ya chama na kuratibu shughuli katika ngazi zote na awe mtu mwadilifu, anayeaminika na anayejali misingi ya chama, asiwe na historia ya kashfa au utovu wa maadili unaoweza kudhoofisha taswira ya chama," ameeleza.
Atakayerithi nafasi hiyo, amesema anatakiwa kuwa na ufanisi katika kujenga hoja, kueleza sera za chama na kuvutia wapiga kura.
Amesema anapaswa kuwa na uelewa wa teknolojia na namna ya kuitumia kuendesha siasa za kisasa na utayari kwa mabadiliko na kuleta uhai mpya ndani ya chama.
"Awe na maono na mkakati thabiti wa kusimamia ushindi wa chama katika uchaguzi mkuu na awe na uwezo wa kusimamia kampeni zenye ujumbe unaovutia wananchi na kushughulikia changamoto za kisiasa kwa wakati," amesema.
Wanaotajwa
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ndani ya CCM, majina yanayotajwa kurithi nafasi hiyo, ni John Mongella, Martine Shigela, Anthony Mtaka, Issa Haji Gavu na William Lukuvi, kuwa ndio wanaoweza kuhimili ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi.
John Mongella
Mongella kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu CCM bara, akiwa na historia ya kuwahi kushika nafasi ya mkuu wa mikoa ya Mwanza na Arusha na mkuu wa wilaya kadhaa kwa nyakati tofauti.
Historia yake ndani ya chama inaanzia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), akihudumu katika nafasi mbalimbali.
Martine Shigela
Shigela naye ana historia inayofanana na Mongella, wote wakizianza siasa zao Chipukizi, baadaye UVCCM na wamekuwa ndani ya chama hicho.
Kwa sasa mwanasiasa huyo ni Mkuu wa Mkoa wa Geita na amewahi kuhudumu kwa nafasi hiyo katika mikoa mbalimbali ikiwemo Tanga na Morogoro.
Anthony Mtaka
Mtaka naye historia yake kisiasa inaanzia UVCCM na baadaye CCM. Kama ilivyo kwa wenzake, amewahi kuwa mkuu wa wilaya mbalimbali kabla hakupandishwa na kuwa mkuu wa mikoa, Simiyu, Dodoma na sasa Njombe.
Mtaka amewahi kutajwa mara kadhaa kama miongoni mwa wanasiasa walio karibu na teuzi nyingi za ndani ya CCM.
William Lukuvi
Huyu ni mwanasiasa mkongwe zaidi ya wote wanaotajwa, akizianza siasa zake tangu vijana, ni mbunge, mkuu wa mikoa kadhaa na waziri muda mrefu.
Lukuvi amekuwa waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu muda mrefu na Wizata ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Issa Gavu
Kwa sasa ni Katibu wa NEC ya CCM Oganaizesheni na amewahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa miaka kadhaa. Anatajwa kama turufu kwenye nafasi hiyo endapo CCM itakuwa inahitaji katibu mkuu wa kwanza atakayetokea Zanzibar.
Gavu naye historia ya siasa zake inaanzia UVCCM akiwa mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji na Kiongozi katika idara ya uchumi ya jumuiya hiyo.
Amewahi kuwa, Naibu Waziri, Waziri na Mwenezi wa CCM upande wa Zanzibar.