Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Raila Odinga akutana na Ruto akisaka turufu mpya ya uongozi AU

Rais Yoweri Museven akiwa na wageni wake Rais wa Kenya, William Ruto (kushoto) na kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga (katikati) walipotembelea Uganda.

Wiki iliyopita, kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Kenya na kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga alitangaza rasmi nia yake ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU).

Waziri Mkuu huyo wa zamani, alizungumza na vyombo vya habari jijini Nairobi, Kenya akisema yuko tayari kuhudumu katika nafasi hiyo, baada ya kushika wadhifa wa Mwakilishi Mkuu wa AU kwenye Miundombinu.

Odinga, ambaye aliambatana na Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo wakati akitangaza nia yake, anasema wameshauriana sana kuhusu suala hilo.

“Kuhudumu kama Mwakilishi Mkuu wa AU kwenye Miundombinu kulinipa fursa ya kujifunza kuhusu kila nchi ya Afrika. Ninaamini kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kuikomboa Afrika,” Odinga anasema.

Tangazo lake la kugombea kazi liliidhinishwa papo hapo na Obasanjo, ambaye anasema ni wakati mwafaka kwa mtu kutoka Afrika Mashariki kuongoza Tume ya AU na anaamini Odinga atakuwa mgombea anayefaa.

“Tunahitaji mtu mwenye uzoefu, mtu anayeelewa hali tuliyonayo na mtu anayetoka katika historia ambayo inaweza kuleta mabadiliko,” Obasanjo anasema.

“Tunaamini watu ambao wameshikilia nyadhifa za wakuu wa serikali kama Waziri Mkuu au Rais watakuwa watu sahihi wakati huu mahususi kushikilia nafasi ya AUC (Tume ya Umoja wa Afrika),” anaongeza.

Odinga anafahamika kuegemea mitandao yake katika chombo hicho, baada ya kuhudumu kama Mwakilishi Mkuu wa AU kwa Maendeleo ya Miundombinu barani Afrika kati ya mwaka 2018 na Februari 2023, wakati muhula wake ulipomalizika kwa utata.
 

Wanasiasa Kenya wampigia debe

Viongozi wa kisiasa nchini Kenya wamemmwagia sifa Odinga, anayewania nafasi ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kuchukua nafasi ya Moussa Faki, anayemaliza muda wake mwaka huu.

Wakizungumza na kituo cha televisheni cha Citizen mapema wiki hii, Seneta Ledama Olekina, wabunge Beatrice Elachi (Dagoreti Kaskazini), Geoffrey Ruku (Mbeere Kaskazini) na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu Kenya (KNUT) Wilson Sossion, wanatoa maoni yao kwamba Odinga ndiye mtu bora zaidi kwa kazi hiyo.

Olekina anasema kuwa Odinga anajivunia utaalamu ulioboreshwa katika siasa za kijiografia za Afrika na ushindi wake utasaidia kuunganisha mataifa ya Afrika na kuruhusu kufikiwa kwa lengo la maendeleo la Afrika.

“Hakuna kiongozi mwenye tajiriba katika bara hili zaidi ya Raila Odinga. Tunataka kutoa wito kwa ndugu zetu wote wa Afrika kufikiria kutoa fursa kwa Raila kuweza kuhudumu kama mwenyekiti,” anasema.

“Yeye pia ni mtu mwenye ubinadamu, amefanya jukumu muhimu katika kuhakikisha kwamba wengine wanakuwa na mazingira mazuri.”

Mbunge Ruku anaongeza kuwa Odinga ana rekodi iliyothibitishwa katika uongozi wa Afrika kutokana na wadhifa wake kama mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika (AU) kwa maendeleo ya miundombinu barani Afrika.

Anabainisha kuwa uteuzi wake utachochea ukuaji wa uchumi na kukuza uhusiano thabiti kati ya uchumi wa Magharibi na Afrika.
“Raila ni mmoja wa wanamajumui wakubwa tulionao barani Afrika. Kuna watu wachache sana ambao wana hadhi ya Raila,” anasema.

“Ni sawa kwetu Kenya Kwanza kumuunga mkono. Tunamwomba Rais Ruto ampe Raila kura yake na kuhakikisha anawashawishi wakuu wengine wa nchi ili azma yake ipitie.”

Kwa upande wake, Elachi anasema uzoefu wa Odinga katika mawanda ya Afrika unampa nafasi ya kupata nafasi hiyo na utamruhusu kuanzisha mageuzi muhimu katika bara hilo.
“Ni yeye tu ndiye anayeelewa historia ya taifa lolote la Afrika. Mataifa ya Afrika yatafungua mipaka na miundo msingi,” anabainisha.

Kwa upande wake, Sossion anarejea hisia za watatu hao akibainisha kuwa ujasiri wa Odinga utaipa Afrika hadhi ya mshindani wa kimataifa.

“Raila ndiye bora zaidi kwa Tume ya AU ikizingatiwa kuwa Kenya ni demokrasia yenye nguvu ya vyama vingi na kwa hivyo tunahitaji thamani kubwa ya kisiasa.”

Wakati akitangaza azma yake ya kuwania nafasi hiyo katika Tume ya AU, Odinga alithibitisha kwamba atadhamiria kubadilisha sura ya Afrika na kulifanya kuwa bara lenye nguvu kiuchumi.

“Kama Pan-Africanist ninaamini sana kuwa Afrika inacheza ligi ambayo haifai kucheza. Kwamba Afrika inastahili bora zaidi,” anabainisha.

“Hili ni jambo tunalohitaji kulibadilisha na linaweza kubadilishwa ikiwa tu kama bara tutasimamia rasilimali zetu zote kwa ukuaji wa haraka wa kijamii na kiuchumi wa bara letu.”

Uungwaji mkono kutoka kwa wakuu wa nchi za Kiafrika utakuwa muhimu katika kumpa Odinga nafasi hiyo.

Kiti hicho kinatarajiwa kuwa wazi mwaka ujao, huku mwenyekiti wa sasa, Moussa Faki wa Chad, akitarajiwa kumaliza muhula wake wa pili. Faki aliteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na alishinda muhula wa pili mwaka 2021.
 

Ruto, Odinga, Museveni

Katika hatua nyingine, Rais wa Kenya, William Ruto amemtembelea Rais wa Uganda, Yoweri Museveni akiwa na Odinga, huku lengo la ziara ya wawili hao likiwa ni kutafuta kuungwa mkono kwa Odinga kwenye nafasi hiyo anayoitazamia.

Viongozi hao watatu wamechapisha picha wakiwa pamoja katika mtandao wa X (zamani Twitter), jambo ambalo limepokelewa vizuri na watu mbalimbali, hasa ikizingatiwa Ruto na Odinga walikuwa mahasimu kutokana na uchaguzi uliopita.

Watatu hao walikutana nchini Uganda Jumatatu iliyopita katika shamba la Rais Museveni lililoko huko Kisozi, ambapo mbali na kujadili diplomasia wamezungumzia uamuzi wa Odinga kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

“Nimefurahi kukutana na Rais Ruto na Odinga mchana huu katika shamba langu la Kisozi. Tulijadili masuala yenye maslahi kati ya nchi zetu mbili na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ninawakaribisha,” ameandika Museveni kwenye ukurasa wake wa X.

Naye, Rais Ruto ameandika kwamba ana furaha kukutana na Rais Museveni nyumbani kwake. Wamejadili masuala muhimu yanayozihusu nchi zao hizo kama vile masuala ya nishati na petroli.

“Katika mkutano wangu na Rais Museveni leo, pia tulijadili haja ya nchi hizi mbili kufuatilia kwa haraka usanifu na ujenzi wa bomba la bidhaa iliyosafishwa ya mafuta ya petroli Eldoret-Kampala-Kigali,” ameandika.

Anaongeza kuwa Kenya na Uganda zimejitolea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia na kiuchumi. Uhusiano huo ni pamoja na kuleta mataifa yote saba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki karibu katika lengo lao kuu la kuunda Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.

Ruto anaongeza kwamba: “Pia, kilichojadiliwa ni kutangazwa kugombea kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga katika nafasi ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.”

Vilevile, kiongozi huyo wa upinzani na Waziri Mkuu wa zamani ambaye mara kadhaa amekuwa akiitia kashkash Serikali ya Kenya, ameandika:

“Siku kadhaa zilizopita, nilikubali mwaliko kutoka kwa Rais Museveni kwa ajili ya mkutano wa pamoja na Rais Ruto leo kujadili kuimarika kwa utangamano wa kikanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki”.

Pia, anasema walijadili kuhusu kugombea kwake uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika siku zijazo.
“Ninamshukuru sana Rais Museveni kwa kuidhinisha kwa dhati kuteuliwa kwangu na kwa Rais Ruto kwa kuunga mkono kikamilifu.”
 

Odinga Namibia

Katika hatua nyingine, Odinga alihudhuria ibada ya kitaifa ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Namibia, Hage Geingob ambaye alifariki Februari 4, 2024 na hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa mataifa 24 duniani ilifanyika Februari 24, 2024.

Katika matukio tofauti akiwa huko, Odinga alionekana akizungumza na viongozi tofauti wa Afrika, ikitajwa kwamba huenda ni njia mojawapo ya kiongozi huyo kutumia fursa hiyo kutafuta uungwaji mkono kwa viongozi hao.

Odinga aliambata na Rais Ruto kwenye hafla hiyo iliyowakutanisha pamoja viongozi mbalimbali wa sasa na wastaafu katika kusherehekea maisha ya Geingob. Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla hiyo.