Odinga atishia kurejesha maandamano, atoa siku 30

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga. Picha na The Times.
Muktasari:
- Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametishia kurejesha maandamano ya kuipinga serikali iwapo mazungumzo na Rais wa nchi hiyo William Ruto hayatafanikiwa
Nairobi. Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga ametishia kurejesha maandamano ya kuipinga Serikali iwapo mazungumzo na Rais wa nchi hiyo William Ruto hayatafanikiwa.
Odinga ambaye ni kiongozi wa Azimio la Umoja ametoa nafasi ya mazungumzo na Kenya Kwanza kwa mwezi mmoja ili kuweza kushughulikia masuala yanayowakumba Wakenya.
Kwa mujibu wa tovuti ya Tuko ya nchini humo Odinga yuko tayari kushirikisha upande wa Ruto na ametoa muda huo pia iwapo mazungumzo hayo hayatakuwa na suluhu, atatoa mwelekeo mwingine mpya kwa wafuasi wake.
"Nimesema kwamba kama Azimio la Umoja, tuko tayari kuzungumza na tutawapa watu hao siku thelathini majadiliano. Baada ya siku hizo kama watabaki kuwa ngumu basi nitatangaza hatua itakayofuata,” Odinga alisema alipokuwa kaunti ya Siaya.
Aliongeza kuwa wametoa fursa hiyo ambayo imeandaliwa pamoja na Kalonzo Musyoka ambaye pia ni mpinzani katika nchini hiyo. Odinga aliwaambia waombolezaji katika mazishi ya David Omondi, aliyepigwa risasi na kuuawa wakati wa maandamano ambayo kwa sasa yamesitishwa.