Upinzani Kenya kutoa mwelekeo Septemba

Muktasari:
- Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, amewataka wafuasi wa muungano wa Azimio la Umoja Kenya, kutulia na subiri hadi mwisho wa mwezi huu wa Agosti, kabla ya kufahamishwa nini kinafuata baada Serikali kuonyesha nia ya kuwa na mazungumzo.
Kenya. Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, amewataka wafuasi wa muungano wa Azimio la Umoja Kenya, kutulia na subiri hadi mwisho wa mwezi huu wa Agosti, kabla ya kufahamishwa nini kinafuata baada Serikali kuonyesha nia ya kuwa na mazungumzo.
Raila ameyasema hayo leo wakati wa maziko ya David Omondi Ofwaya, yaliyofanyika katika Kaunti ya Siaya, na kwamba wametoa huo mwezi mmoja kwaajili ya mazungumzo ya maridhiano na upande Kenya Kwanza unaounda Serikali.
“Kenya Kwanza wana muda wa mwezi mmoja kuzungumza nasi. Ikiwa hatutakubaliana, tutawapa watu wetu mwelekeo mnamo Septemba 1, 2023,” amesema Raila.
Wakati kukiwa na maendeleo hayo chanya kuhusu maridhiano, dalili za vuta nikuvute zimeanza kujitokeza, na hasa baada ya Rais William Ruto, akiwa katika ziara yake Mlima Kenya siku ya Jumamosi, kusikika akisistiza kwamba atawawekea ngumu wapinzani.
Rais Ruto ambaye amewahutubia wakazi wa Githurai, Kaunti ya Kiambu, amesisitiza kuwa hakutakuwa na ‘handshake’.
“Wanapoteza muda kwa kuleta vitisho vya kutaka ‘handshake.’ Hao watu nitawakalia ngumu sana,” amesema Rais Ruto.
Pamoja na mambo mengine, Ruto amewaahidi wakazi hao kwamba masoko mengine 15 yatajengwa katika kaunti hiyo, huku akiahidi kwamba pesa zaidi zitaelekezwa katika sekta ya elimu.
Kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha, Rais Ruto amesema ilani ya Kenya Kwanza, imeweka wazi mikakati ya kurahisisha maisha ya Wakenya, Rais anatambua wamelemewa na mzigo mzito wa maisha.
Amechukua fursa hiyo kufafanua kwamba ujenzi wa nyumba za gharama nafuu utasaidia pakubwa kukabili tatizo la ukosefu wa ajira.
“Si tulisema Kazi Ni Kazi ama nyinyi ni wale wa kuchagua kazi?” ameauliza.
Rais vile vile amewahutubia wakazi wa Kenol (Murang’a) na Kagio (Kirinyaga).