Ni zamu ya Tabora mjini opresheni C4C ya Chaumma

Muktasari:
- Operesheni hiyo ambayo siku ya uzinduzi haikupata msisimuko uliotarajiwa lakini baada ya kuanza kutumia usafiri wa Chopa umekuwa mchawi na kivutia tosha cha kujaza wananchi kwenye mikutano yake na kusikiliza ujumbe na hoja za Chaumma.
Tabora. Kwa mara ya kwanza tangu kuzinduliwa kwa operesheni ya C4C ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) Juni 3 Juni 2025 katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, leo ni zamu ya wananchi wa Tabora Mjini.
Operesheni hiyo ambayo inazidi kushika kasi kadiri inavyohubiriwa na viongozi wake kwa wananchi, inaendelea kuwavuta wananchi kwenda viwanjani kusikiliza kinachohutubiwa.
Inaelezwa kingine kinachowavuta wananchi kwenye viwanja wanavyotumia Chaumma kunadi kampeni yao hiyo ya C4C, ni usafiri wa chopa unaotumiwa na baadhi ya viongozi wake akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe.
Kampeni hiyo ilipozinduliwa kwa mara ya kwanza jijini Mwanza, baadhi ya wadau walionesha wasiwasi kama itafanikiwa kutoka na kuhudhuriwa na watu wachache, hata hivyo, kadiri siku zinavyokwenda, wananchi wameendelea kumimika kuwasikiliza viongozi wanaoinadi C4C.
Chaumma kilianza kukusanya watu kwenye mkutano waliofanya Musoma Mjini mkoani Mara na sasa ni mwendo wa ‘nyomi’ ya watu.
Mbali na kuonekana chopa kama mchawi na kichocheo cha kujaza watu, lakini Mwenyekiti wa Chaumma, Rungwe naye amegeuka kivutio kikubwa kwa wananchi kutokana na sera yake ya ubwabwa hasa anavyoifafanua kwa kina kwamba inamaanisha nini.

James Shegeni akizungumza na Mwananchi leo, amesema awali alikuwa hatilii maanani kile kilichokuwa kikihubiriwa na Rungwe kuhusu Ubwabwa, lakini kadiri siku zinavyoenda, anamuelewa.
“Tunaona kama masihara, lakini sera ya ubwabwa imebeba ujumbe mzito, kama mtu atatafakari ni wazi ataona chama hiki kinamaanisha nini, huwezi kuwa na taifa ambalo watu wake ni dhoofu ukatarajia watakuletea matokeo chanya kwenye maendeleo,” amesema Shegeni.
Hivyo, baada ya Kigoma jana, Chaumma leo wako Tabora mjini ambako viongozi wake waandamizi wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Rungwe na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chaumma Bara, Devotha Minja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu wathutubia mkutano wa hadhara.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia alasiri sambamba na mambo mengine, chama hicho kitatambulisha safu yake ya uongozi.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, Mwalimu, mkutano huo utafanyika katika uwanja wa shule ya Msingi Uyui iliyopo mjini Tabora.
Jana jioni katika uwanja huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilihitimisha mkutano wake wa hadhara wa kampeni ya No reform No Election.
Nacho Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Makamu mwenyekiti wake, Stephen Wassira ambaye yuko mkoani Ruvuma, jana alihutubia pia wananchi wa Wilaya ya Tunduru na leo, yuko wilayani Nyasa.
Hata hivyo, wakati mikutano hiyo ya vyama ya hadhara ikiendelea nchini, jana Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ilitoa onyo kwamba vinapaswa kuheshimu sheria ya vyama vya siasa. Na wale watakao kiuka watachukuliwa hatua za kisheria.
Opresheni ya C4C inatarajiwa kufika mikoa yote Tanzania. katika awamu ya kwanza ya ziara hiyo inayolenga kukiandaa ili kushiriki Uchaguzi Mkuu, kupokea wanachama wapya na kuziba ombwe la viongozi kwa maeneo ambayo hayana viongozi, chama hicho kimesema kitazunguka mikoa yote ya Kanda nne, Kaskazini, Victoria, Serengeti na Magharibi.
Baada operesheni hiyo itageukia Kanda ya Nyasa, Kusini, Kati, Pwani kabla ya kuhitimisha Zanzibar.