Prime
CCM, Chadema, Chaumma ni mwendo wa kufuta nyayo

Muktasari:
- Vyama vya Chaumma, Chadema na CCM, vinaendelea za ziara zao zenye malengo tofauti kwa kukutana na wananchi, kuzungumza nao na kueleza ajenda zao wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025
Dar es Salaam. Vyama vitatu vya siasa vimeendelea kuchanja mbuga katika mikoa mbalimbali nchini huku vikipishana kwenye maeneo wanayopita wenzao ili kufuta nyayo walizoziacha waliowatangulia kwenye maeneo hayo.
Vyama hivyo vya Chaumma, Chadema na CCM, vinaendelea za ziara zao zenye malengo tofauti kwa kukutana na wananchi, kuzungumza nao na kueleza ajenda zao wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Vigogo wa CCM akiwamo Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Stephen Wasira anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Ruvuma.

Leo alikuwa Songea wakati Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla akiendelea na ziara yake Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wa Chadema, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche anaendelea na ziara mkoani Singida, leo alikuwa Itigi baada ya kumaliza ziara yake mkoani Dodoma akigawana maeneo na Kaimu katibu mkuu wake, John Mnyika.
Kwa upande wa Chaumma, viongozi wa chama hicho wakiongozwa na mwenyekiti, Hashim Rungwe wanaendelea na ziara mkoani Kigoma wanakoutambulisha uongozi mpya baada ya kundi la waliokuwa makada wa Chadema kuhamia kwenye chama hicho.
Makalla amefanya ziara katika mikoa ya kaskazini ikiwa ni wiki moja baada ya Heche na viongozi wengine wa Chadema kupeleka ajenda yao ya No reforms, no election (bila mabadiliko hakuna uchaguzi) katika eneo hilo.
Kadhalika, Heche amefanya ziara mkoani Dodoma zikiwa zimepita wiki chache tangu Wasira alipofanya ziara mkoani humo kwa kuzunguka wilaya moja hadi nyingine.
Huo ni mwendelezo wa viongozi wa vyama hivyo kuviziana kwa kupita walipotoka wenzao.

Wasira ameanza ziara yake mkoani Ruvuma ukiwa umepita mwezi mmoja na nusu tangu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alipofanya ziara yake mkoani humo kabla ya kukamatwa Aprili 9, 2025 akiwa Wilaya ya Mbinga.
Baada ya kumaliza ziara yake Ruvuma, Wassira ataendelea na ziara yake mikoa Mwanza na Geita kuanzia Juni 15 – 18, 2025, mkoa ambao Chaumma walizindulia ziara zao za kukijenga chama huku wakizunguka kuzungumza na wananchi.
Wakati Chadema wakiifafanua ajenda yao ya No reforms, no election kwa wananchi, CCM nayo imekuwa ikieleza kazi zinazofanywa na Serikali pamoja na umuhimu wa kushiriki uchaguzi mkuu.
Chaumma nao wamekuwa wakihamasisha wananchi kushiriki uchaguzi mkuu ujao ili waweze kupigania mabadiliko wanayoyataka.
Ziara za CCM mikoani
Akiwa Wilaya ya Rombo, Makalla amesema Tanzania na Kenya zimekuwa na uhusiano mzuri wa kihistoria na kindugu, hivyo amewataka wananchi waliopo mpakani mwa nchi hizo (Tarakea) kutumia fursa za kiuchumi zilizopo.

Aidha, amewataka wananchi hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri katika mpaka huo kwa kuendelea kudumisha amani iliyopo ili watumie fursa mbalimbali za kujiinua kiuchumi.
Makalla amesema kuwa, eneo la Tarakea limeendelea kukua lakini ukuaji wake unachagizwa na mwingiliano wa kibiashara baina ya Tanzania na Kenya.
"Kwa historia, uhusiano kati ya Tanzania na Kenya umekuwa wa kihistoria, ni wa kindugu, ni uhusiano mzuri, watu wetu wanafanya biashara kati ya Tanzania na Kenya. Tuwapongeze marais wetu,Samia Suluhu Hassan na William Ruto kwa kuendeleza uhusiano huu mzuri,” amesema.
Akizungumzia kampeni inayoendelea mtandaoni ya No reforms No election, amesema mpango mzima wa Watanzania ni ‘Oktoba Tunatiki’ na hakuna wa kuzuia uchaguzi huo kwa kuwa, unafanyika kwa mujibu wa Katiba.
“Hebu wenye yale mabango wayanyanyue juu, No reforms no election haina nafasi, Oktoba tunatiki, huo ndiyo mpango mzima wa Watanzania na wao walisema wana nguvu ya umma. CCM ndiyo yenye nguvu ya umma Tanzania, chama chetu ndiyo chama namba moja Tanzania.
“Uchaguzi unaoweza kuzuiwa ni uchaguzi wa kwenye ukoo…tu, uchaguzi mkuu hauwezi kuzuiwa maana uko kwa mujibu wa Katiba na Watanzania wanaojitambua watakwenda kupiga kura,” amesema Makalla.
Kwa upande wake, Wasira, akiwa Songea, amesema wanaotaka uchaguzi mkuu Oktoba 2025 uahirishwe, waahirishe mambo yao wenyewe.
Wasira amesema tayari CCM imeshajipanga kwa uchaguzi mkuu kwa kuwateua wawakilishi wa nafasi ya urais na makamu wa Rais ambao ni Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Emmanuel Nchimbi.

“Wapo rafiki zangu wa 'Tone Tone' wanapita wanawaambia wananchi tusifanye uchaguzi, mimi nawauliza tusipofanya wananchi waongozwe na nani,” amehoji Wasira.
“Wanasema tuahirishe uchaguzi, hatuahirishi ng’o, aahirisha mambo yako mwenyewe sisi tayari tumeshaweka wagombea,” amesema.
Heche atikisa Itigi
Akiwa, Itigi mkoani Singida, Heche amesema umaskini wa Watanzania si wa bahati mbaya bali umetengenezwa kwa makusudi kutokana na uongozi mbovu wa Serikali kwa kipindi cha zaidi ya miaka 63 tangu kupata uhuru.
Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwamo madini, mbuga za wanyama, mito, maziwa, milima, ardhi na gesi, lakini wananchi wake bado wanaishi katika hali ya umaskini mkubwa.
“Mtu hawezi kuelewa ni kwa nini nchi yenye utajiri mkubwa kama huu inaendelea kuwa maskini. Jibu ni rahisi ni kutokana na uongozi mbovu na matumizi mabaya ya fedha za umma,” amesema Heche.
Akitoa mfano, Heche amedai kuwa mwaka wa fedha uliopita, Serikali ilitumia Sh571 bilioni kwenye maeneo ambayo hayakuleta tija ya moja kwa moja kwa wananchi, akisema kiasi hicho kingeweza kubadili maisha ya wakulima endapo kingeelekezwa kwenye sekta ya kilimo.
“Angalau, kama hizo hela zingetumika kununua matrekta na kuwapa wakulima, tungeona maana yake. Lakini sasa ni matumizi ya kufurahisha viongozi tu na si maendeleo ya watu,” amesema.
Chaumma yaunguruma Kigoma
Viongozi wa Chaumma wametua Mkoa wa Kigoma kuendelea na mikutano yao ya Operesheni C4C iliyoanzia jijini Mwanza Juni, 3, 2025 ambako walipita kukiandaa chama hicho tayari kwa uchaguzi mkuu.
Viongozi hao wanafanya mikutano hiyo wakitokea Mkoa wa Geita walikofanya mikutano mitatu ya hadhara katika maeneo ya Masumbwe, Katoro na Geita mjini.

Akizungumza wilayani Kibondo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chaumma – Bara, Devotha Minja amewaahidi wananchi wakichukua dola baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025, chama hicho kitakuja na mkakati wa kufuta mikopo ya kausha damu inayowatesa kina mama.
Amesema baada ya kufuta mikopo, watatumia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na kila halmashauri kulikopesha kundi hilo, kuliwezesha kufanya shughuli zake kwa uhuru tofauti na ilivyo sasa, fursa hiyo wananufaika wake ni wachache na wahitaji wengi hawafikiwi.
Minja amesema kama kiongozi mwanamke, anaumizwa anaposhuhudia kila uchwao madhila wanayopitia kuhangaika kufanya marejesho ya mikopo ya kausha damu.
“Kila mahali ukipita, wanawake hawana furaha, walio wengi wanaumizwa na vikoba, kausha damu, ndugu zangu, unakopa Sh50,000 baada ya wiki moja unaenda kulipa Sh100,000.
“Chaumma tunasema tukishika dola, asilimia 10 zinazotolewa na halmashauri zitaenda kutibu jambo hili, sasa hivi fedha hizo zipo lakini wengi hawapati, ni shida, na wanaosimamia ni madiwani kutoka chama fulani, wanawaangalia wao tu,” amesema Minja.
Imeandikwa na Janeth Mushin a Janeth Joseph (Kilimanjaro), Baraka Loshilaa (Ruvuma), Tuzo Mapunda (Kigoma) na Mintanga Hunda (Dar es Salaam).