Mwita: Nimeondolewa ukatibu sekretarieti sababu ya chuki dhidi ya Mbowe

Muktasari:
- Siku moja baada ya aliyekuwa Katibu wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chadema, Julius Mwita kutenguliwa wadhifa huo, amefunguka kilichotokea akilitaja kundi la WhatsAAp.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chadema, Julius Mwita amesema pamoja na mambo mengine uamuzi wa kutenguliwa kwenye wadhifa huo, umechochewa na chuki na visasi alivyodai bado vipo ndani chama hicho, tangu kumalizika kwa uchaguzi Januari 21,2025.
Mwita ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Mafunzo, Tathimini na Ufuatiliaji amekwenda mbali zaidi hasira na uhasama hizo ndizo zilisababisha kusambaa kwa jumbe walizokuwa wakijadiliana kuhusu hatima ya watia nia katika kundi la WhatssApp lililopewa jina la G-55.
Jumbe hizo zilisambazwa na mmoja ya mtia nia (jina tumelifadhi kwa sasa), ambaye alijumuishwa kwenye kundi, lakini muda mchache akaondolewa ndipo alipoamua 'kuscreen shot' jumbe zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuwafikia viongozi wakuu wa Chadema.
Ujumbe uliosambaza ulionekana kama unapingana na uamuzi wa chama hicho kuhusu ‘No Reforms No Election’ hatua iliyonekana kama usaliti hasa kwa Mwita ambaye ni msaidizi wa Mnyika
Uteuzi wa Mwita ulitenguliwa jana Jumatano Aprili 2, 2025 na Katibu Mkuu wa Chadema (John Mnyika), ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuteau na kutengua cheo hicho.
Hata hivyo, mapema leo Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia ameithibitishia Mwananchi kutenguliwa kwa Mwita, pasipo kutoa sababu zaidi ya kueleza kuwa hata wakati anateuliwa haikutangazwa popote.
Mbali na hilo, Rupia amesema hakuna chuki, visasi wala uhasama baina ya timu Mbowe na Lissu na kwamba mambo yanakwenda vizuri.

" Kilichopo baadhi ya wanamuunga mkono Mbowe bado wana maumivu ya uchaguzi ndio maana wanapinga na hawakubaliani na kila ajenda zinazoletwa na uongozi wa sasa," amesema Rupia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 3, 2025 Mwita ambaye amehudumu nafasi hiyo kwa tangu miaka 2017 amekiri kutenguliwa akisema hana kinyongo na Mnyika kuhusu uamuzi aliouchukua.
Mwita ameweka wazi hapingani na No Reforms bali hakubalina na ‘No Elections’ akisema ni jambo lisilowezekana Chadema kuzuia uchaguzi katika mazingira ya sasa.
Amesema hicho, ndicho walichokuwa wanajadili katika kundi sogezi akiwa na wanachama wenzake (watiania) 54 ambao ambao miongoni mwa mwambo waliokuwa wakijiuliza ni namna gani Chadema itaweza kuzuia uchaguzi wakati vyama vingine vimeshaanza maandalizi.
"No Reforms sawa, lakini ukianiambia No Election...kwa wale mliobahitika kuona 'screen shot' maswali yangu yalikuwa ni haya tutazuiaje uchaguzi? Kama mtu anaweza kunijibu sawa.CCM imeshaanza maandalizi imeteua mgombea urais na mgombea mwenza na inaendelea kuwaanda wagombe ubunge na udiwani.
" Kama kuzuia tungeanza kuzuia uandikishaji kwanza, sasa unashindwa kuzuia halafu unasema No Election how? (vipi) hakuna anayesema tunazuiaje uchaguzi tunaambiwa tu No Reforms No Election," amesema Mwita.
Mwita amesema katika kundi la G- 55 watia nia wanakubaliana na No Reforms, lakini No Election wanapata kigugumizi kuielewa.Amehoji kwamba unaposema No Election maana yake unazuia uchaguzi, ambao huwezi kushiriki uchaguzi, hutopata ruzuku wala wabunge na madiwani.
"Kwenye lile kundi tulikuwa tunauliza maswali tu kama ukishindwa kuzuia uchaguzi CCM ikiendelea, tishio la Chadema itakuwa nini kwa miaka mitano ijayo? Chadema itakuwa wapi miaka mitano ijayo? amehoji Mwita.
Mwezi uliopita Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Amos Makalla amesema chama hicho, hakitakibembeleza Chadema kishiriki uchaguzi, huku kikitoa wito kwa watia nia wao kujiunga na vyama vingine kikiwemo CCM ili kutimiza ndoto zao.
Kwa mujibu wa Mwita, hakuna taifa lolote ambalo chama kimoja kimewahi kuzuia uchaguzi bali watu wanaingia katika uchaguzi na kukabiliana na wanaohusika na mchakato huo.
"Mwaka 2010 Chadema ilishindwa majimbo 24 na wabunge wa viti maalumu 25 kulikuwa na tume gani huru? Mbona tulishinda maeneo mengi Musoma Mjini na Ukerewe. Kura ziliibiwa, lakini tulishinda uchaguzi,"
"Huwezi kuzuia uchaguzi bora hiyo nguvu uitumie kushinda uchaguzi, kwenye lile kundi tulijadili kutafuta Reforms kwa njia mbalimbali kwenye jamii, lakini hii No Election haijakaa sawasawa.
"Tulipanga leo kwenye kikao cha watia nia kwa umoja wetu G55 tuhoji haya mambo ndani ya hicho kikao, tujibiwe na tuwaambie fikra zetu kwamba No Election haiwezekani.Lakini mtu mmoja aliyetaka kuonekana mwema ' aliscreenshot' na kuzipeleka kwa viongozi kwamba tumepinga msimamo wa chama hadharani," amesema Mwita.
Mwita amesema uwepo wa kundi la G55 sio kosa kwa kuwa walipanga mkakati wa kuwasilisha hoja zao katika kikao cha watia nia wa ubunge wote kilichongozwa na mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Hata hivyo, Mwita amesema G55 imeandaa hoja sita kuhusu msimamo wa No Reforms No Election zilizowasilishwa kwa Mnyika wakitarajia zitasomwa mbele ya kikao cha watia nia kinachoendelea makao makuu ya chama hicho, Mikocheni.
"Tumeandika petition yetu yenye kurasa tano na tumeiwasilisha kwa Mnyika kwamba mawazo yetu sisi watia nia 55 ni haya.Tumeomba ufafanuzi tunakwenda kama chama cha siasa kinachokengeuka chenyewe," amesema.
Visasi na chuki
Katika mazungumzo yake, Mwita yote yaliyofanyika dhidi yake na wengi ni visasa visivyoisha tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho uliogawa pande mbili za wanaomuunga mkono Lissu na Freeman Mbowe.
"Sijaondolewa kwa sababu ya hizo jumbe bali chuki, ubinafsi, hasira, uchungu na vinyongo.Ndani ya miezi miwili wakati nafanya kazi, nilikuwa kama yatima.Nimeondolewa kwa sababu mimi mbaya amesema Mwita.
Mwita ambaye yeye ni kwanza kutenguliwa lakini kuna kigogo mwingine (jina tumelifadhi) anafuata kutokana msimamo wake.
"Kwa taarifa yenu yupo mwingine atafukuzwa hivi karibuni, sidhani kama hii wiki itaisha, labda wabadilishe uamuzi baada ya mimi kuzungumza hadharani ila yupo. Pia wapo wajumbe wa kamati kuu waliokuwa wanamuunga mkono Mbowe wanashughulikiwa kwelikweli," amesema Mwita.