‘No Reforms, No Election’ yamwondoa Mwita sekretarieti ya Chadema

Aliyekuwa Katibu wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Julius Mwita
Muktasari:
- Inadaiwa kuwa Mwita hakubaliani na msimamo wa Chadema na amekuwa akihamasisha wengine kupinga ajenda ya “No reforms, no election” ambayo ina lenga kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi ili kuwapo na usawa na haki.
Dar es Salaam. Katibu wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Julius Mwita ameondolewa katika wadhifa huo kwa madai kwamba amekwenda kinyume na msimamo wa chama hicho kuhusu ajenda ya “No Reforms, No Election”.
Inadaiwa Mwita hakubaliani na msimamo huo na amekuwa akihamasisha wengine kupinga ajenda hiyo ambayo inalenga kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi ili kuleta usawa na haki.
Sekretarieti ya kamati kuu inaundwa na Katibu Mkuu, pamoja naibu makatibu wakuu na miongoni mwa majukumu ya sekretarieti ni kuandaa ajenda za kamati kuu.
Uteuzi wa Mwita umetenguliwa jana Jumatano Aprili 2, 2025 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia amelithibitishia Mwananchi leo Alhamisi Aprili 3, 2025.
“Ni kweli ametenguliwa nafasi hiyo na uteuzi wa Mwita haukuwahi kutangazwa kwa sababu ni kazi ya KM (Katibu Mkuu), ndio maana hatujalitolea ufafanuzi,” amesema Brenda bila kueleza sababu za kutenguliwa kwa Mwita.
Mwananchi limezungumza na Mwita ambaye amewahi kuwa Katibu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) ambapo amekiri kuondolewa katika nafasi hiyo.
“Ni kweli nimeondolewa, lakini nitazungumza leo baadaye nitaweka wazi kila kitu, vumilia tu,” amesema Mwita ambaye amehudumu kama Katibu wa Bavicha kwa miaka zaidi ya mitano.
Hata alipoulizwa sababu za kutenguliwa, Mwita amesema: “Mbona una haraka sana, unataka niweke wazi kila kitu, baadaye nitazungumza nini?” amehoji Mwita.
Endelea kufuatilia Mwananchi na mitandao yake ya kijamii kwa taarifa zaidi.