Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwili wa mwasisi Chadema kuzikwa kesho, Mnyika asema…

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa akisaini kitabu cha maombolezo ya msiba wa aliyekuwa mmoja wa waasisi wa chama na baadaye kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Bara (1998 - 2004), Dk Medard Mutungi aliyefariki jana Jumapili, Aprili 26, 2026 jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Maziko ya kiongozi huyo wa zamani wa chama hicho yanatarajiwa kufanyika kesho Jumanne, Aprili 28, 2026 katika Makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mwili wa miongoni mwa waasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Medard Mutungi, unatarajiwa kuzikwa kesho Jumanne, Aprili 28, 2026 katika Makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Dk Mutungi, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara kuanzia mwaka 1998 hadi 2004, alifariki dunia jana, Jumapili Aprili 26, 2026.

Kwa mujibu wa viongozi wa chama hicho, Dk Mutungi atakumbukwa kama miongoni mwa waasisi wa Chadema, aliyependa kuona vijana wanapewa uongozi wa chama na aliyejitolea fedha zake binafsi kukiendesha chama hicho.

Kifo cha mwasisi huyo kinatokea miezi mitatu tangu Chadema ilipompoteza mwasisi wake mwingine, Edwin Mtei, aliyefariki dunia Januari 20, mwaka huu. Mtei ndiye aliyekuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Historia ya chama hicho inamtaja Dk Mutungi kuwa miongoni mwa waasisi tisa wa Chadema, iliyoanzishwa Januari mwaka 1993.

Katika orodha ya waasisi tisa hao, yumo Edwin Mtei, Bob Makani, Brown Ngwilupipi, Edward Barongo, Mary Kabigi, Costa Shinganya, Evalist Maembe na Steven Wassira.

Katika orodha hiyo ya waasisi--- Wassira, Shinyanga na Maembe ndio wapo hai hadi sasa. Hata hivyo, Wassira si mwanachama tena wa chama hicho, alihamia Chama cha Mapinduzi (CCM) na sasa ni Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho tawala.


Mnyika amlilia

Akizungumzia msiba huo leo, Jumatatu Aprili 27, 2026, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, amesema Dk Mutungi atakumbukwa kama miongoni mwa wanasiasa wakweli, wapenda haki na waaminifu kuwahi kutokea nchini.

“Katika utumishi wake ndani ya chama, akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara mwaka 1998 hadi 2004, alikuwa mkweli na mtu wa haki, mwaminifu na alipenda vijana washike nafasi kwenye chama,” amesema.

Amemtaja kuwa mwanasiasa aliyejitolea kukiendesha chama hicho na wakati huo hakikuwa na fedha, hivyo alilazimika kutoa fedha zake binafsi kugharimia uendeshaji wa Chadema.

Katika misimamo ya kisera, amesema Dk Mutungi alikuwa muumini wa soko huria na alishinikiza kukoma kwa mfumo wa uchumi kumilikiwa na dola, badala yake alitaka sekta binafsi kuendesha uchumi.

“Mazishi yatafanyika kesho Jumanne Aprili 28, 2026 katika Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam. Misa itafanyika saa 7:00 mchana katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mwenge,” amesema.


Huyu ndiye Dk Mutungi

Katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa siasa za vyama vingi nchini mwaka 1995, Dk Mutungi aligombea ubunge wa Bukoba Vijijini kwa tiketi ya Chadema, akishindana na mgombea wa CCM, Sebastian Kinyondo.

Hata hivyo, Dk Mutungi hakushinda uchaguzi huo, lakini hakukubaliana na matokeo. Alifungua kesi Mahakama Kuu akitaka matokeo ya uchaguzi huo yafutwe kwa sababu za kutofuatwa sheria, rushwa na kudhalilishwa.

Jaji wa kesi ya awali alitupilia mbali madai ya kutokufuata sheria kwa sababu hayakuathiri matokeo ya uchaguzi. Hata hivyo, alikubaliana na madai mengine dhidi ya mlalamikiwa na alitangaza uchaguzi huo kuwa batili.

Aidha, kutokana na uamuzi wake kwamba mlalamikiwa alikuwa na hatia ya vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi, mahakama iliamuru kutolewa kwa cheti kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi kikithibitisha mlalamikiwa amepatikana na hatia ya kufanya vitendo vya rushwa.

Mbali na sababu hizo mbili zilizotajwa, mahakama ilibatilisha uchaguzi huo kwa sababu mlalamikiwa aliwavutia wapiga kura kwa kutumia hisia za kikabila katika kampeni zake.