Chadema yatoa salamu kwa waliohama
Mwenyekiti wa Chama cha Dermokrasia na maendeleo Kanda maalum ya Serengeti Lucas Ngoto akizungumza katika hafla ya kufungua rasmi shughuli za kichama baada ya zuio, iliyofanyika katika ofisi ya kanda maalum iliyopo Manispaa ya Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.
Muktasari:
- Kiongozi wa kanda ya Serengeti amesema chama kimeendelea kuwa imara zaidi kuliko awali na kuwasihi waliobaki kudumisha mshikamano na uadilifu.
Shinyanga. Katika hafla ya kuzindua upya shughuli za kichama baada ya kusitishwa kwa takribani miezi kumi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Serengeti kimetoa salamu kwa waliokuwa wanachama wake ambao, kwa sababu mbalimbali, waliamua kujiondoa na kujiunga na vyama vingine.
Akizungumza leo Jumapili, Aprili 26, 2026, katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za kanda zilizopo Manispaa ya Shinyanga, Mwenyekiti wa Chadema Kanda Maalumu ya Serengeti, Lucas Ngoto, amewahimiza wanachama waliobaki kuendelea kuwa thabiti na kutoathiriwa na ushawishi wa watu wengine.
“Leo tuko imara zaidi kuliko tulivyokuwa jana. Baadhi yetu walijiondoa njiani, lakini sisi tuliendelea na safari. Walioondoka tuwahurumie, kwani kuondoka kwao hakukutuzuia kusonga mbele na sasa tumerejea na nguvu mpya,” amesema Ngoto.
Aidha, Ngoto amewahimiza wanawake wa chama hicho kujishughulisha kiuchumi badala ya kubaki nyumbani bila shughuli zinazoweza kuwaingizia kipato.
“Sitaki kusikia wanawake wa Chadema wakijitambulisha kama ‘mama wa nyumbani’ bila kufanya shughuli za kiuchumi. Anzeni na mtaji mdogo, hata Sh10,000, muuze bidhaa kama nyanya na mjitafutie kipato,” ameongeza.
Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Kanda Maalumu ya Serengeti, Jackson Mnyawami, amesema kipindi cha zuio, kimewapa fursa ya kujipanga upya na kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi, ikiwemo kuboresha ofisi za kanda ili ziwe za kisasa.
Amesema lengo ni kuimarisha mazingira ya utoaji huduma kwa kujenga ukumbi mkubwa wa kisasa utakaoweza kuchukua zaidi ya watu 200, pamoja na ukumbi mdogo wa watu 50. Ameongeza kuwa makadirio ya awali ya gharama za mradi huo ni Sh112 milioni, huku tathmini ikiendelea.
Mwenyekiti wa Chama cha Dermokrasia na Maendeleo Kanda maalum ya Serengeti, Lucas Ngoto akipandisha Bendera ya Chadema, kuashiria kufungua rasmi shughuli za kichama kanda maalum ya Serengeti baada ya zuio kuisha. Picha na Hellen Mdinda
Mnyawami pia amebainisha kuwa hadi kufikia hatua ya sasa, asilimia 99 ya fedha za uboreshaji wa jengo zimetolewa na wanachama wenyewe, na tayari Sh5 milioni zimetumika kujenga uzio.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Mkoa wa Mara, Alfonce Machira, amesema ziara rasmi katika mkoa huo zitaanza Mei mosi, 2026, sambamba na usajili wa wanachama wapya na ujenzi wa ofisi za chama katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kwa upande mwingine, Katibu wa Chadema Mkoa wa Simiyu, Johnstone Musibukya, amesema changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa mkoa huo ni uvamizi wa fisi wanaoshambulia mifugo na watu.
Hivyo, ameahidi kuendeleza juhudi za kukabiliana na tatizo hilo. “Fisi wanashambulia mifugo na hata watu, usiku na mchana. Tumejipanga upya kuendeleza mapambano, si tu kisiasa bali pia katika kudhibiti wanyama hawa ambao wamekuwa tishio kubwa kwa wakazi wa Simiyu,” amesema Musibukya.