Prime
Mpina aingia anga za Gwajima

Mwanza. Hatima ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kisiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), iko njiapanda sawa na ilivyo kwa Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima.
Hii ni baada ya ukosoaji wa mbunge huyo kwa Serikali, kukosolewa hadharani na Rais Samia Suluhu Hassan akiwataka pia wananchi wamuache.
Rais Samia ameenda mbali akiueleza umma kuwa Mpina amekuwa kama mbunge wa Taifa, hivyo wananchi “wamuachie yeye amwangalie kwenye nafasi zake kumi za uteuzi.”
Huyu ni mbunge wa pili kukumbana na rungu la Rais Samia, baada hali hiyo kumkuta Askofu Josephat Gwajima katika Mkutano Mkuu wa CCM mwishoni mwa Mei, alipowataka wajumbe wa vikao vya chama kufanya uchujaji wa haki na uadilifu lakini wale “magwajima” waachwe nje.
Akisisitiza hilo, bila kufafanua alisema: “Tukitoa mwanya ndugu zangu, tukipitisha wale wanaotaka ‘na mie niwemo’, ndiyo tunapata wale wanaokwenda huko, chama kinakuwa Gwajimanized. Kwa vyovyote vile, tusigwajimanize chama chetu, magwajima tuyaache nje, hamna kuoneana aibu wala haya."
Mwenyekiti huyo wa CCM alieleza hayo, kipindi ambacho mbunge huyo wa Kawe alikuwa anatoa matamshi ya kuikosoa Serikali kwa masuala mbalimbali, akiitaka Serikali kushughulikia matukio ya utekaji na watu kupotea.
Siku mbili baadaye hata Kanisa na Ufufuo na Uzima analoliongoza lilifutwa na Serikali na askari polisi wakatanda na kuwatimua waumini hadi sasa.
Kuwa njiapanda kwa wabunge hao wawili kunapata uzito, hasa kwa kuwa anayekosoa kauli zao, ndiye mwenyekiti wa CCM, chama kinachoamua hatima waombaji wa ubunge, akiwa ndiye kiongozi wa vikao vya uteuzi vinavyotarajiwa kuketi mwezi ujao, kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hatima ya Mpina
Rais Samia ametoa kauli kuhusu Mpina wakati akieleza kutoridhishwa na mtindo wa mbunge huyo jimboni kwake, ikiwemo kuwasilisha maombi ya miradi mbalimbali katika ziara ya mkuu huyo wa nchi mkoani Simiyu, badala ya bungeni.
Yote hayo, yalitokana na salamu za Mpina katika mkutano wa hadhara wa Rais Samia ziarani Meatu, leo Jumanne, Juni 17, 2025 alizozigawa katika makundi matatu – maombi, changamoto na pongezi.
Katika maombi, pamoja na mengine, Mpina amemwomba mkuu huyo wa nchi afanikishe ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami jimboni humo akiongeza kuwa, katika eneo hilo bado wanamdai Rais Samia.
“Sisi kule Kisesa tunakudai, maeneo mengine kote wanaosema hawakudai, zile fedha zote zihamishe zilete Kisesa kwa sababu bado tuna mipango mingi ya maendeleo katika maeneo yetu,” amesema Mpina, aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi katika awamu ya tano.
Maombi mengine ametaka wafugaji walioshinda kesi mahakamani warudishiwe mifugo yao, kadhalika utaratibu wa ununuzi wa pamba usihusishe mnunuzi mmoja.
Kwa upande wa changamoto, ametaja uvamizi wa tembo na katika pongezi amempongeza Rais Samia kwa utekelezaji wa miradi ya Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, kuanzisha Tume ya marekebisho ya masuala ya kodi na ujenzi wa miundombinu ya barabara na afya.
Salamu hizo za Mpina, zilipata majibu ya moja kwa moja kutoka kwa Rais Samia, aliyesema kitendo chake cha kutoa maombi hayo kwenye mkutano ni kama anajitafutia umaarufu, kwani yote alipaswa kuyaomba bungeni.
Amesema hata pongezi zilizotolewa na mbunge huyo zimehusisha miradi iliyopo nje ya jimbo lake, jambo linaloashiria anatekeleza majukumu ya kitaifa badala ya jimboni, kwamba ni kama mbunge wa Taifa.
“Lakini ndugu zangu maombi kama haya Leah huyu (Leah Komanya, mbumge wa viti maalum) aliyawasilisha bungeni na mawaziri wakatekeleza maombi yake, sasa maombi kama haya kuyaleta kwenye mkutano kwa wananchi kwa Rais, ni kujitafutia umaarufu na kuthibitisha kwamba mbunge hakulifanyia haki jimbo lake,” amesema Rais Samia
Amesema mbunge huyo angewasilisha hoja hizo bungeni zingefanyiwa kazi.
“Huyu si mbunge wa jimbo bali ni mbunge wa taifa, kwa hiyo nadhani tunapokwenda huko muache nimchukue kwenye nafasi zangu 10,” amesema Rais Samia.
Sambamba na hilo, ameeleza kukerwa na hatua ya Mpina kufananisha barabara zinazojengwa jimboni humo na mwanamke aliyesuka nywele za twende kilioni.
“Ndugu zangu (wananchi) nadhani mngekuwa serious (makini) kutuletea wabunge wa kukutoleeni huduma kwenye majimbo yenu, nadhani huyu ni mbunge wa taifa siyo wa jimbo, kwa sababu hakuongea chochote cha jimbo lake, badala ya barabara za kusuka nywele ndicho alichoongea,” amesema.
Mpina, mara kadhaa amesikika akikosoa au kupingana na baadhi ya misimamo ya Serikali na amewahi kuhojiwa na kuonywa.
Katika mkutano wake na wananchi hivi karibuni, Mpina aliwaambia wananchi kuwa, yale yote ambayo hayakutekelezwa vema, atayakatia rufaa kwa Rais Samia.
Alichokisema Bashe
Awali, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe naye alimjibu Mpina kuhusu utaratibu wa kuwa na mnunuzi mmoja wa pamba, akisema bei ya zao hilo inapangwa na Serikali na si mtu mwingine yeyote.
“Wanasiasa wa Mkoa wa Simiyu wameitumia pamba kama siasa na si zao la kiuchumi la kuwatoa watu kwenye umasikini. Kwanza hakuna mtu yeyote anayeweza kutathmini bei ya pamba isipokuwa Serikali, hata wakiwa wanunuzi 500 kwenye kijiji,” amesema.
Amesema tayari alishakubaliana na Mpina kuwa, kila atakaposema hoja zake atazijibu hadharani kwa kuwa hakuna ambalo Serikali inaficha.
“Mpina huyu aliua kitalu cha mbegu katika kitalu cha Mwabisalu kwa siasa hizihizi za kuwadanganya wananchi, Serikali ikajiondoa. Tuliweka kitalu wananchi wale walikuwa wanapata zaidi ya Sh250 milioni hadi Sh320 milioni, fedha za ziada ukiacha bei, akaenda kuwahamasisha wapande mahindi katika hivyo vitalu.
“Mwaka 2019/20 alikuwemo kwenye Serikali, ni mmoja kati ya watu waliompotosha Rais Magufuli (Hayati John), kumwambia kuwa bei ya pamba duniani ni juu Rais atangaze bei, matokeo yake pamba ikafa, hawa wananchi pamba zikanunuliwa Sh500 ikawa matatizo matupu,” amesema.
Amesema hatamruhusu mtu yeyote aharibu mfumo ulioanza kujengwa, kwani mwaka huu pamba katika Wilaya ya Meatu imefikia tani 30,000.
Amesema kwa sasa wanatarajia kuvuna tani 60,000 na kwamba wakulima wote waendelee kukusanya zao hilo kwani anayeamua bei ni Serikali.
“Tulianza na Sh1, 150, tukamaliza na Sh1,700, Serikali itakuwa inatoa bei kutokana na mwenendo wa soko la dunia, mfumo wa kilimo cha mkataba ndiyo mfumo sahihi wa kuondoa tatizo la pamba,” amesema.
Baada ya kuilichotokea mkutanoni hapo, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Benson Ontario amesema isingehitaji kumsikia akiongea bali macho na uso wa Mpina viliashiria kustushwa.
“Hali ya Mpina ilikuwa dhahiri kwamba ameguswa na maneno ya Rais. Alionekana hana amani kabisa na hii si kwa bahati mbaya. Kauli ya Rais ilikuwa ya moja kwa moja, ikihusiana na misimamo ambayo Mpina amekuwa nayo,” amesema.
Mbali na tukio hilo, akiwa ziarani mkoani Simiyu Rais Samia amefungua kiwanda cha kuchakata pamba cha Biosustain, Hospitali ya Itilima na amefanya mikutano miwili ya hadhara kati ya Meatu na Itilima.
Rais Samia amesema kinachochakata Pamba mbali na kutengeneza ajira kitapanua soko la wazalishaji pamba katika wilaya ya Meatu na kuwa na uhakika wa soko kwa wakulima, jambo ambalo ni malengo ya Serikali kupeleka viwanda katika maeneo mbalimbali nchini.
“Muhimu zaidi wawekezaji wa kiwanda hiki wanakusudia kupanua uwekezaji wao kwa kuongeza kiwanda kingine chenye thamani ya Sh12 bilioni kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta ya mbegu za pamba na alizeti, haya ni maendeleo makubwa sana nami nawahamasisha wawekeze zaidi,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda cha Biosustain Tanzania Limited, Dk Riyaz Haider amesema wanatumia mfumo wa kilimo cha mkataba kwa kuwekeza moja kwa moja kwa wakulima kupitia mabwana shamba, ambao wanawapa pikipiki, mafuta na elimu pamoja na vitendea kazi vingine ikiwemo pembejeo.
Amesema uwekezaji huo ni kuwa karibu na wakulima na kuipata pamba kwa urahisi ambapo wataichakata na kuipeleka sokoni, lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji kufikia tani 1,000,000, huku wakulima wakiongeza uzalishaji kutoka kilo 350 hadi tani 2.5.
“Lengo letu ni kuhakikisha kweli hii pamba tunayoinunua hapa kwa wakulima, soko liko karibu tunafikiria mkulima kumpa bei nzuri zaidi, huko ndiyo tunakoelekea. Huu mfumo wa BBT ambao tumekuja nao unafaa uendelee tuwekeze zaidi ili tufikie uzalishaji wa tani 1,000,000 na kuendelea,” amesema Dk Haider