Mbowe: Acheni kulalamika, chukua hatua kuiondoa CCM

Mwanza. Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amewataka Watanzania kuacha kulalamika ugumu wa maisha na badala yake wachukue hatua kwa kuiondoa CCM madarakani.

Mbowe alitoa kauli hiyo jana, alipohutubia wananchi wa jimbo la Buyungu katika Kijiji cha Gwarama wilayani Kakonko Mkoa wa Kigoma, katika 'Operesheni +255 Katiba Mpya' na kwamba lengo hilo litafikiwa kwa nchi kuwa na Katiba mpya, Tume Huru ya Uchaguzi na sheria mpya za uchaguzi.

Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini alisema changamoto zinazoikumba nchi, ikiwemo ubadhirifu wa fedha ya umma kama ilivyoonekana kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni matokeo ya utendaji mbovu wa CCM.

"Nawaomba wananchi msiishie kulalamika tu, bali tushirikiane kwa umoja wetu kuiondoa CCM madarakani. Na lengo hili tutalifikia endapo tutakwenda kwenye uchaguzi tukiwa na Katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na sheria mpya za uchaguzi.

"Tutakuwa tunafanya makosa makubwa kama tutarudi kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa sheria hizi hizi, kwa tume hii hii ya uchaguzi na Katiba hii. Ndiyo sababu ajenda yetu kubwa sasa ni kuipata Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi," alisema.

Katika hatua nyingine, Mbowe alieleza machungu waliyopitia upinzani katika kipindi cha miaka saba iliyopita kuwa ni baadhi ya viongozi wa chama hicho kununuliwa, kukosa uhuru wa kujieleza na kuikosoa Serikali, huku akisema uhuru wa mikutano ya hadhara ni matokeo ya mateso waliyopitia viongozi wa chama hicho.

"Tuliteswa, ila tumeendelea kuilinda imani yetu kwa watu wote bila ubaguzi. Tuna kila sababu ya kupongezana kwa haki ya kujieleza kurejea, hatimaye leo tunaikosoa Serikali huku Polisi wakitulinda wakati walikuwa wanatupiga mabomu," alisema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu aliwataka wakazi wa jimbo la Buyungu kuacha kuwa ndumilakuwili, badala yake walinde imani yao kwa chama hicho kwa kujisajili kidijitali, ili kurahisisha utambuzi kuwa ni wanachama wa chama hicho.

"Endeleeni kulinda imani yenu kwa Chadema kwa sababu ni chama kitakachoendelea kubeba matumaini ya Watanzania na kuwasemea na kuwa chachu ya maendeleo katika jamii," alisema Mwalimu.

Pia aliwataka wananchi kutokata tamaa kutokana na matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwaka 2020, badala yake wajipange kwa ajili ya kurejesha viongozi wao madarakani katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani na katika Uchaguzi Mkuu 2025.

"Hatuko kwenye maridhiano na Chama cha Mapinduzi na Serikali yao kwa sababu ya fedha, bali kwa sababu tunahitaji kurejesha haki ya Watanzania ambayo ilikuwa imepokwa kwa miaka saba. Misukosuko tuliyopitia ni mikubwa, lakini tunamshukuru Mungu tumepita na tunaendelea kusonga mbele," alisema.

Aliyekuwa mgombea ubunge wa Buyungu katika Uchaguzi Mkuu 2020, Ashura Masoud akihutubia wakazi wa Kijiji cha Kakonko mkoani humo alitishia kuitisha maandamano kushinikiza mkuu wa wilaya hiyo kuingilia mgogoro wa wananchi zaidi ya 100 wanaodaiwa kuporwa zaidi ya ekari 450 za mashamba.

Ashura alitaja vijiji vilivyoathirika na uporaji wa mashamba hayo kuwa ni Bukililo, Gwanumpu, Kasuga, Kewe, Nkuba, Nyamtukuza na Lumashi vilivyoko katika Halmashauri ya Kakonko mkoani Kigoma.

"Ekari 450 zimeporwa, kuna mashamba ya wananchi yakiwa na mazao bila kushirikishwa na hakuna fidia. Ekari 50 zilikuwa mashamba yenye mazao mbalimbali, ikiwemo miti ya mbao, ekari 15 mali ya Abel. Tunaitaka Serikali kuingilia kati suala hili kabla sijaitisha maandamano," alisema Ashura na kuongeza:

"Ardhi ambayo si mashamba yao ni eneo la kijiji ambalo halipaswi kuuzwa bila ridhaa ya wanakijiji, walighushi muhtasari wa mkutano kwamba wananchi walishiriki katika kuuza ardhi ya kijiji. Tunaelekea wapi kama ardhi inachukuliwa na watawala wamekaa kimya," alihoji Ashura.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, Gaston Garubindi alisema migogoro ya ardhi nchini itatatuliwa kwa kupata Katiba mpya, kwani Katiba inayopendekezwa na chama hicho itabainisha taratibu za mtu kujimilikisha ardhi.

"Tunahitaji Katiba mpya itakayoweka mipaka ya viongozi wasiwe sehemu ya matatizo yetu. Mnalalamika kuporwa ardhi na mtu anayejiita mwekezaji, lakini viongozi wamekaa kimya. Chadema haitafumbia macho uhalifu wa aina hii," alisema Garubindi.

Mkazi wa Gwarama, Abel Mapembe alikiomba chama hicho kuendelea kupaza sauti kuhusu changamoto zilizopo katika kijiji hicho, huku akizitaja kuwa ni pamoja na ukosefu wa elimu ya uzazi wa mpango, afya duni na ukosefu wa miundombinu, ikiwemo barabara.

Jana, Mbowe akiwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu walifanya mikutano ya hadhara katika kata ya Nyabibuye, Gwarama, Ganumpu na Kakonko Mjini, zilizopo jimbo la Buyungu wilayani Kakonko Mkoa wa Kigoma.