Mbowe awataka CCM kutubu dhambi, kujiunga Chadema

Muktasari:

  • Mbowe amesema Chadema imejengwa katika msingi wa Demokrasia na ushindani hivyo anawakaribisha wanachama na viongozi wa vyama vingine ikiwemo Chama tawala (CCM) kujiunga Chadema ili kukijenga chama kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (2024) na Uchaguzi Mkuu (2025).

Kigoma. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe amewakaribisha wanachama na viongozi wa vyama vingine vya upinzani na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiunga na Chadema ili kukiondoa chama tawala madarakani.

 Mbowe ametoa ukaribisho huo leo alipokuwa akihutubia wananchi wa Kata ya Kakonko mjini mkoani Kigoma, ikiwa ni mwendelezo wa Operesheni +255 Katiba Mpya iliyozinduliwa Mei 17, 2023 Kitaifa mkoani humo.

"Kama kuna masalia ya vyama vingine vidogo vidogo ambavyo vimeshakosa mwelekeo karibuni kwenye jeshi la ukombozi, Jeshi la Chadema; tuunganishe nguvu hata wale wa Chama Cha Mapunduzi wanaopenda haki na wanaoamini kwamba haki hunyanyua Taifa karibuni Chadema tubuni dhambi zenu tusonge mbele kukomboa taifa letu," amesema.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mmoja wa waasisi wa chama hicho cha upinzania, amewataka wana Chadema ambao ni waathiriwa wa vitendo vya uminyaji wa Demokrasia nchini, kusahau maumivu waliyopitia na kuanza safari ya mapambano upya ili kuikomboa nchi kutoka kwenye mikono ya CCM.

"Tuliteswa, tulipigika, tulitukanwa sana, wengine walipigwa risasi, wengine wakauwawa na wengine walipotezwa lakini hatukupiga magoti kuungana na CCM. Ni bora kufa umesimama kuliko kuishi umepiga magoti," amesema Mbowe.

Katika hatua nyingine, Mbowe amelitaka Jeshi la Polisi kutotumika kuingilia shughuli za uchaguzi badala yake amelitaka kusimamia haki, ulinzi na usalama wa raia bila kujali itikadi za vyama vyao.

"Ninyi Polisi niwaombe mtuachie siasa tupambane na hawa CCM, wameshatepeta hawa uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu kabla ya misa ya asubuhi wagombea wa CCM wote watakuwa wamelala chali," amebainisha Mwenyekiti huyo.

Chadema inaendelea na ziara yake ya kufanya mikutano ya hadhara kila kata nchi nzima ambapo kwa kuanza imeanzia katika kata na majimbo ya mkoa wa Kigoma.