Mbeto asisitiza Tanzania kuendelea kuheshimu taasisi za kiraia, dini

Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis.
Muktasari:
- Mbeto ameyataka makundi ya kisiasa, kidini na kijamii kutambua Serikali ya Tanzania tangu iundwe, haina dini na katika nyakati zote iliweka bayana msimamo wake kitaifa na kimataifa, haitajiegemeza katika dini
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeyaahidi makundi huru ya kijamii na madhehebu ya dini, kupokea ushauri na maoni huku ikiyataka kutambua Serikali ya Tanzania haina dini.
Pia, CCM imeyaasa makundi hayo ikitaka yajue mantiki ya utawala wa sheria ni utamaduni wa kutatua hoja za kisheria; kwa mujibu wa sheria mahakamani si kuicharaza bakora hoja au kuipiga rungu.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, alipozungumza na waandishi wa habari wakati akituma salaam za Pasaka kwa Wakristo wote duniani kisiwani Unguja.
Mbeto amesema makundi hayo , yasilishinikize Jeshi la Polisi kibabe na vitisho badala yake, watumie busara ya kutii sheria bila shuruti wala chagizo .
Amesema ikiwa makundi hayo yataamua kila moja liseme kivyake au kuandamana bila kibali cha polisi, huku baadhi yao wakivua nguo na kutembea utupu, huko pia ni kwenda kinyume na sheria za nchi hivyo watakamatwa.
"Kwa muda mrefu makundi hayo yamekuwa kimya hata pale baadhi ya wanasiasa wa upinzani walipotoa matamshi ya kuogopwa.
“Ni matamshi mfululizo yalioambatana na vitisho kinyume na sheria. Jumuiya hizo zingetosha kuwaonya viongozi hao kwa kuwaelimisha, hivyo wafanyavyo sivyo, "amesema Mbeto.
Katibu huyo mwenezi huyo, amesema kumeanza kusikika sauti za makundi hayo yakitaka pPolisi kumwachia huru Mwenyekiti wa Chadema , Tundu Lussu kutokana na kesi inayomkabili mahakamani.
Mbeto ameyataka makundi hayo ya kisiasa, kidini na kijamii kutambua Serikali ya Tanzania tangu iundwe, haina dini na katika nyakati zote iliweka bayana msimamo wake kitaifa na kimataifa, haitajiegemeza katika dini.
“Nchi yetu inafuata utawala wa sheria. Endapo kila mwanasiasa atakapokiuka sheria yatoke mashinikizo kwa dhehebu lake haitaleta maana. Waumini wa dini moja wafuasi wake walikaa zaidi ya miaka kumi mahabusu hayakutokea madhehebu yao kushinikiza, "amesema Mbeto.
Aidha Mbeto, amesema ikiwa kiongozi wa kisiasa atakuwa wa Dhehebu la Wasabato, Waanglikana, Ethnaasheeria , Suni, Ismailia au Mkatoliki anayekabiliwa na kesi mahakamani , viongozi wa madhehebu hayo wakishinikiza aachiwe mara moja kutazuka utata na tafran isiokuwepo.
"Joseph Kasela Bantu, Christopher Kassanga Tumbo,Modestus Choga na James Mapalala walikaa vizuizini katika Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere . Viongozi wa dhehebu la kikatoliki waliheshimu uamuzi wa Serikali . Utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete , masheikh wa Kiislamu walitupwa jela lakini madhehebu yao zilitii sheria,”amesema.
Pia, Mbeto ametoa mfano mwingine, akimtaja Mchungaji Christopher Mtikila ambaye alikuwa kiongozi wa chama cha DP, amekamatwa mara nyingi na hadi akafungwa jela, viongozi wa dhehebu lake hawakuzua mijadala yenye jazba .
"Tumemuona mwenyekiti mstaafu wa Chadema Freeman Mbowe ni Mlutheri. Ameshitakiwa kwa tuhuma ya kesi ya ugaidi katika utawala wa marehemu Rais Dk John Magufuli. Amekaa mahabusu akatolewa na Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan bila shinikizo lolote,”amesema Mbeto.
Katibu huyo mwenezi, pia ametoa mfano wa kesi ya uhaini ya wanasiasa 18 wa Chama cha CUF katika utawala wa Rais mstaafu Dk Salmim Amour , watuhumiwa wote wakiwa waislamu, waliiachiwa huru katika utawala wa Rais mstaafu Dk Amani Abeid Karume.
"Katika kesi ya uhaini ambayo kiongozi wake, Pius Lugangira na wenzake, walifungwa jela maisha katika utawala wa mwalimu Nyerere. Wakaachiwa huru Awamu ya Pili ya Rais marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi bila hekaheka zozote, " amefafanua Mbeto.
Hata hivyo, mwalimu Nyerere aliwahi kukataa ombi la Kiongozi wa dhehebu la Orthodox wa Cyprus, Askofu Makarios la kutaka amwachie huru mfanyabishara mmoja aliyeleta kiburi na jeuri hadi pale Nyerere alipojiridhisha.