Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wataka haki itendeke ili kulinda amani

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa wito wa kulinda amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, wadau kutoka makundi mbalimbali wametilia mkazo umuhimu wa haki na usawa katika jamii ili kuimarisha utulivu wa nchi.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, wadau hao wameeleza kuwa amani ya kweli inaweza kudumu endapo dosari zilizojitokeza katika chaguzi zilizopita za mwaka 2019, 2020 na 2024 zitafanyiwa kazi, kwani mifumo ya uchaguzi isiyotoa haki kwa wananchi inaweza kuwa chanzo cha machafuko.

Jana, Rais Samia akiwa mgeni rasmi katika Baraza la Idd lililofanyika jijini Dar es Salaam, alisema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayetumia dini kuchochea chuki na uhasama nchini na kuhatarisha amani.

Kiongozi huyo alisisitiza kwamba amewiwa kulitupa jukumu la ulinzi wa amani na utulivu nchini mikononi mwa viongozi wa dini na kuwa Serikali kwa upande wake, italinda na kusimamia misingi ya Katiba ya kuheshimu uhuru wa raia wa kuabudu na kuhubiri dini.


CCM yampongeza Samia

Kufuatia kauli hiyo, Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis amempongeza Rais Samia kwa kuliona hilo kwa sababu amani ni tunu ya taifa na si jambo la kufanyika wakati wa uchaguzi pekee, bali wakati wote.

Amesema pamoja na uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, uhuru huo usisababishe uvunjifu wa amani, hivyo amemshukuru Rais Samia kwa kuonya juu ya mtu yeyote atakayechezea amani kwani vyombo vya dola vitamshughulikia.

“Nampongeza Rais Samia kwa kulitamka hili katika Baraza la Idd na ni vizuri tukarudi kwenye mstari, wale viongozi wa dini tukahimiza watu wetu katika kumtii Mungu na kuhimiza utulivu na umoja,” amesema Mbeto.


Amani itategemea haki

Hata hivyo, wakizungumza na Mwananchi leo Aprili mosi 2025, wadau hao wa dini na siasa wamesisitiza kwamba haki ndiyo msingi wa amani, kama haitatendeka katika jamii, basi hata suala ya amani ya kudumu itakuwa ni changamoto.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Padri Charles Kitima amesema amani itakuwepo kama watu watatendewa haki, watapewa haki zao na haki zao zitalindwa wakati wote na waliopewa dhamana.

“Kama mtu anapiga kura yake halafu inavurugwa, usitegemee amani. Kwa hiyo, Serikali ionyeshe kwa vitendo kusahihisha makosa ya watu kukoseshwa haki zao za kisiasa kwenye uchaguzi uliofanyika mwaka 2019, 2020 na 2024.

“Kama hayo hayataachwa, hao wanaofanya hayo, chama kinachofanya hayo, wasimamizi wanaoyaruhusu hayo, ndiyo chanzo cha kuvuruga amani,” amesema Padri Kitima wakati akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mabalozi wastaafu nchini, Dk James Nsekela amesema suala la kudumisha amani linaanza na mwananchi mmoja mmoja kwa kuwa sehemu ya kuleta amani na siyo kuwa chanzo cha vurugu.

“Kila mtu anafahamu ili awe na amani anahitaji kuwa na utulivu kiasi gani na yeye asiwe chanzo cha vurugu yoyote, isipokuwa chanzo cha amani,” amesema Dk Nsekela.


Amani tunda la haki

Maoni ya viongozi hao hayako mbali na ya Dorothy Semu, kiongozi wa ACT Wazalendo, ambaye amesema ni muhimu kufahamu kwamba amani ni tunda la haki na chama chake kimekuwa kikikumbusha haki ya Watanzania kuchagua viongozi na kuchaguliwa, ambayo imepokwa kwenye chaguzi wa mwaka 2019, 2020 na 2024.

“Tumeshuhudia namna uchaguzi wa serikali za mitaa ulivyopokwa kutoka kwa wananchi kinyume na matarajio, makubaliano na rai ya Serikali pamoja na Rais Samia mwenyewe,” amesema Dorothy.

Amesema Rais Samia aliwaahidi Watanzania kwamba watapata chaguzi huru na haki na za kuaminika na kuwa aliwataka waache yaliyopita, badala yake wagange yajayo ili walijenge taifa lao.

Dorothy amesisitiza kwamba wameona yote yaliyofanyika miaka mitatu iliyopita yalikuwa ni hadaa, hata hivyo hawatachoka kusukuma mabadiliko ili yatokee kwa wananchi na zisiwe ni hadithi za hadhaa.

“Kudumisha amani, kusimamia haki kunahitaji utashi wa kisiasa ambao ukiwekwa kazini, wananchi na watu wote watafurahia matunda yake. Hatuoni umuhimu wa kuja na kauli za kulinda amani wakati wao CCM ndiyo wanaosimamia michakato ya kunyima haki za wananchi,” amesema.


Wito wa wafanyabiashara

Kwa mtazamo huohuo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamis Livembe naye amesema ili kudumisha amani katika msimu huu wa uchaguzi wangependa kuona kunakuwa na uchaguzi huru na haki ili amani iendelee kudumu.

Amesema wafanyabiashara wamekuwa ni waathirika wakubwa zinapotokea vurugu au maandamano, jambo linalosababisha biashara zao kufungwa au kukabiliwa na uporaji au uharibifu wa mali zao.

“Zinapotokea vurugu, wafanyabiashara tunaathirika, tuliona kilichotokea wakati wa vurugu za Kidongo Chekundu wakati ule wa maandamano ya CUF, kuna mfanyabiashara alifariki nyumbani kwake kabisa.

“Kunapokuwa na maandamano au ghasia, magari yanavunjwa vioo, yanachomwa moto na magari mengine barabarani ya biashara kama mabasi au daladala. Kwa hiyo, sisi kama wafanyabiashara tunaogopa hizo kadhia kwa sababu biashara na uwekezaji vinaathirika,” amesema.

Ameongeza kuwa katika kipindi ambacho biashara zao zinaharibiwa kwa kukosekana kwa amani, wafanyabiashara hushindwa kulipa kodi.

Ametolea mfano hali inayoendelea Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako biashara haziwezi kufanyika.


Zanzibar yamulikwa

Kilio cha haki pia kimetolewa na Mwenyekiti mstaafu wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji akisisitiza huwezi kupata amani kama hakuna haki, huku akitolea mfano vitabu vya dini, kuwa vinahimiza watu kutenda haki.

Hata hivyo, amedai Wazanzibari kwa muda mrefu wamekuwa wakinyimwa haki zao.

Amesema ni haki ya kila mtu kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, lakini wapinzani zaidi ya 70,000 hasa Pemba, hawapewi vitambulisho hivyo sababu ikitajwa ni kutofanya kazi kwa mashine wakati Unguja zinafanya kazi.

“Wamebadilisha sheria uchaguzi ufanyike siku mbili, hakuna haja kwa uchaguzi wa Zanzibar kufanyika siku mbili, Zanzibar ina watu milioni 1.7 au milioni 2. Mbona Bara kuna wapigakura zaidi ya milioni 30 lakini wanapiga kura siku moja?” amehoji.

Babu Duni amesisitiza kwamba ni muhimu mambo ya haki yakafanyika ili kuleta amani inayotarajiwa, hasa kwa Zanzibar ambayo imekuwa ikitumbukia kwenye ghasia za baada ya uchaguzi.


Timiza wajibu

Ili kuondoa sintofahamu hiyo, Wakili Dk Onesmo Kyauke amesisitiza kwamba ni muhimu kila mtu kutimiza wajibu wake katika kufuata sheria na kwamba uchaguzi hauna maana ya kuvunja sheria, bali kuhubiri amani, umoja na mtengamano wa kitaifa.

“Amani inaweza kupotezwa kwa mambo mengi, hasa wanasiasa wanaweza kuchochea kwa kutaka kuchaguliwa kwa kutumia dini, ukabila au ukanda au ujinsia. Kwa hiyo, ni kila mwanasiasa kujizatiti kutimiza wajibu wake,” amesema.

Ameongeza kuwa ni muhimu kila mmoja kufuata maadili na kuhakikisha amani inakuwa ni kipaumbele badala ya kuhubiri chuki majukwaani.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema amani inatunzwa kwa kutenda haki, hivyo kuelekea kwenye uchaguzi, malalamiko yote ya Watanzania kuhusu uchaguzi yafanyiwe kazi.

“Viashiria vinavyoweza kuvunja amani wakati wa uchaguzi vinapaswa kufanyiwa kazi na kiashiria moja wapo ni kuwepo kwa kilio cha watu ambao wameona mfumo wa uchaguzi hauwatendei haki,” amesema.

Ameongeza kuwa ni muhimu kufanya vikao vya kitaifa vya wadau wote wa uchaguzi, ili kutathmini namna ya kwenda kwenye uchaguzi na namna ya kuboresha mifumo ya uchaguzi, ili amani iendelee kuwepo.


Askofu Bagonza ahoji

Wakati hayo yakielezwa, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Benson Bagonza amesema haki ndiyo inayowaunganisha wote bila kujali itikadi, dini, jinsia, kabila, hali ya kiuchumi, ufupi au urefu wa mtu.

Katika andiko lake lililosambaa mitandaoni, Askofu Bagonza amesema kuna mambo 10 hayako sawa kwa sababu hivi sasa, mtu anapozungumzia haki, anatazamwa yeye ni dini gani badala ya kusikiliza anaongea nini.

“Mtu akiongelea haki anatazamwa ni wa chama gani badala ya kusikiliza anaongea nini? Mtu akilalamika amepotelewa na nduguye, anaambiwa anavuruga amani. Mbuzi akipotea anapatikana lakini mtu akipotea hapatikani na kulalamika kuwa mtu amepotea kunaonekana ni kuvuruga amani.