Makada 83 CCM Arusha wajitosa kumrithi Zelothe

Katibu wa CCM Mkoani Arusha, Musa Matoroka.
Muktasari:
- Wanachama 83 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, wamejitosa kuchukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania nafasi ya uenyekiti iliyoachwa wazi na Zelothe Stephen, aliyefariki dunia, Oktoba 27, 2023.
Arusha. Harakati za kuwania nafasi ya uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha, zimezidi kupamba moto kwa makada 83 kuchukua na kurejesha fomu.
Kwa muda mrefu sasa nafasi hiyo imekuwa na ushindani mkubwa kutokana na aina ya siasa za Arusha huku mchakato wake ukuhusisha makada maarufu na wenye uwezo kifedha.
Kumekuwa na usiri mkubwa wa kuweka hadharani makada waliochukua fomu na kurejesha mpaka sasa. Hata hivyo, Mwananchi linafahamu kuwa kuna makada maarufu kadhaa waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo akiwemo Mjumbe wa Kamati ya Siasa mkoa Arusha, Robert Kaseko na aliyekuwa mkuu wa mkoa Morogoro, Lootha Sanare.
Pia, wamo Mbunge wa Arumeru Mashariki, Daniel Palangyo na aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Thomas Sabaya ambaye ni baba wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.
Hadi kufikia jana jioni Alhamisi, Novemba 23, 2023, wakati dirisha la kuchukua na kurejesha fomu likifungwa rasmi makada watano walishindwa kurejesha fomu hizo.
Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mussa Matoroka amesema:
"Tulifungua pazia la uchukuaji wa fomu Novemba 21 na Novemba 23, 2023 tumefunga rasmi. Kati ya wanachama 88 walioonyesha nia kwa kuchukua fomu ni 83 tu ndio waliorejesha wengine wameingia mitini."
Kuhusu sababu za mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu kutumia siku chache (tatu), Matoroka amesema ulilenga kuwapa makada wachache wenye sifa stahiki kuongoza nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa Matoroka baada ya mchakato wa kurejesha fomu kukamilika, hatua inayofuata ni vikao husika kuchambua na kupitia sifa za walioomba kisha hatua zingine zitafuata.
Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuwaonya makada kutojihusisha na siasa za kupakana matope na rushwa kwani, kwa kufanya hivyo ni kunyume cha kanuni za chama.