Zelote awataka Arusha kushiriki sense

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Zelote Steven (aliyevaa kofia) akiawa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya chama hicho mkoa katika ziara ya kukagua madarasa yaliyojengwa na fedha za Uviko-19 katika shule ya sekondari Karatu. Picha na Teddy Kilanga
Muktasari:
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Zelote Steven amewataka wananchi wa mkoa wa Arusha kushiriki katika sense ya watu na makazi inaayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Zelote Steven amewataka wananchi wa mkoa wa Arusha kushiriki katika sense ya watu na makazi inaayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Akizungumza katika kuelekea maadhimisho ya miaka 45 ya CCM ambapo kwa mkoa wa Arusha yamefanyikia wilayani Karatu, Zelote amesema amewasihi wanachi kajitokeza kwenye sense ili kuisaidia Serikali kupata takwimu sahihi za idadi ya watu zitakazosaidia katika mipango ya maendeleo.
"Sensa inasaidia kufahamu takwimu ya idadi ya watu waliopo nchi ili kuandaa mpango wa maendeleo kwa wananchi husika," amesema Zelote na kuongeza
"Pia sensa inasaidia Serikali kutekeleza miradi yake kupitia taarifa za wananchi ambazo zinatokana na sensa hivyo tushirikiane na mjitokeza katika kufanikisha jambo hili ambalo ni muhimu kwetu pamoja na Serikali,"amesema Mwenyekiti huyo.
Pia Zelote ameagiza hospitali ya Wilaya ya Karatu kuanza kutoa huduma mara moja itakapokamilika ili kuwarahisishi wananchi wanaohitaji huduma za matibabu.
Hospitali hiyo ya wilaya ambayo imejengwa kwa fedha za Uviko-19 ipo katika hatua za mwisho za kukamilika majengo hayo ni jengo la utawala, OPD, maabara na jengo la dawa.
"Pamoja na hilo hospitali ya wilaya ya Karatu ianze kazi kwa juhudi zote za kutoa huduma kwa wananchi na isingependeza kusubiri kiongozi wa nchi ndio aje atoe agizo," amesema Mwenyekiti huyo.
Zelote ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kutunza miundombinu ya shule na vituo vya afya vilivyoboreshwa na Serikali hivi karibuni huku akitoa rai kwa wazazi kuwahimiza wanafunzi kuhudhuria masomo.
"Ndani ya mkoa wa Arusha Serikali imefanikiwa kujenga madarasa zaidi ya 513 ya fedha za Uviko-19 hivyo ni vyema wazazi wakaendelea kuwahimiza wanafunzi kwenda shuleni kusoma kwani wameondolewa adha ya michango ya ujenzi wa madarasa pamoja na ununuzi wa samani za shule," amsema Zelote.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karatu (DC), Dadi Kolimba amesema wilaya hiyo walipokea Sh1.2 bilioni ambazo zimesaidia kujenga madarasa 60 ambayo yameshakamilika na wanafunzi wameanza kuyatumia.
Kolimba amesema mpaka sasa wanafunzi waliojiunga kidato cha kwanza ni 3301 kati ya 4000 sawa na asilimia 74 hivyo amewataka wazazi wa wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni kuwapeleka kabla ya wiki ijayo.
Amesema kuwa kuanzia wiki ijayo uongozi utapita nyumba kwa nyumba kufanya msako wa vijana ambao wamechaguliwa lakini bado hawajaripoti.
"Haiwezekani Serikali inaboresha mazingira ya shule halafu watoto hawapelekwi shule na wazazi wao tutapita nyumba kwa nyumba kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake," amesema.
Amesema kwa upande wa ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo ambao umegharimu Sh2 bilioni za Uviko-19 upo katika hatua za mwisho za kukamilika ambapo majengo hayo ni jengo la utawala, OPD, maabara na jengo la dawa.