Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu ataja mambo sita ya kurekebishwa ili washiriki uchaguzi

Muktasari:

  • Amesema yasipofanyika hawawezi kushiriki, asisitiza mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, uwazi, usalama na haki kwa vyama vyote na wagombea.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ametaja mambo sita ambayo yakifanyiwa kazi chama hicho kitashiriki Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu.

Lissu ametaja mambo hayo leo Jumanne, Aprili 8, 2025 wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma kwenye mwendelezo wa ziara ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Operesheni ya ‘No Reforms, No Election’ inayoendelea Kanda ya Kusini.

“Katika mapendekezo yetu kulikuwa na mambo sita, hatukuyaanzisha sisi, isipokuwa tumeyapigania kutoka katika Tume ya Jaji Nyalali ambayo ilisema tubadilishe mfumo wetu wa uchaguzi kwa sababu uliopo unapendelea upande mmoja. Lakini imepita miaka 30 bado tunaimba wimbo uleule.

“Tunahitaji kubadilisha mfumo wa uchaguzi kusiwe na mgombea anayepita bila kupingwa, pili hatutaki taratibu za uchaguzi zinazoruhusu wagombea wengine kuenguliwa, tatu hatutaki kuandikishwa watoto wadogo kwenye daftari la kudumu la mpigakura.

“Nne hatutaki kufanyiwa fujo tena kwenye kampeni zetu tunazofanya, tano mawakala wa vyama vyote wawe huru kufanya shughuli zao, ikiwemo kujua kura zao na kama hakuna mawakala uchaguzi usifanyike, sita hatutaki kuona uchaguzi unaotoa kafara za watu ili wapate uongozi,” amesema Lissu.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akihutubia wananchi wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma akiwa kwenye muendelezo wa kutoa elimu ya No Reforms No Election.

Mwanasheria huyo amesisitiza bila utaratibu wa uchaguzi kubadilishwa wananchi hawawezi kupata viongozi sahihi watakaowajibika, kuwatetea na kuwasemea changamoto zinazowasibu.

Amesema chaguzi nyingi zinazofanyika zinawanyima wananchi fursa ya kuchagua viongozi, akitolea mfano ule wa serikali za mitaa wa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020 zilizokipendelea chama tawala na wale wanaotoka vyama vya upinzani wakienguliwa bila sababu za msingi.

Amesema kwa kutambua hilo, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 vyama vya upinzani havijakaa kimya, vimekuwa vikipigania mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi lakini hadi sasa havijafanikiwa.

Mbali na mambo hayo, Lissu amezungumzia “wizi wa kura unaofanyika kwenye vituo vya kupigia kura”, kuwa pia ni sababu ya kupatikana viongozi ambao si chaguo la wananchi.

“Haiwezekani tena na chaguzi za namna hii, wanaosema twende tu hatuwezi kwenda machinjioni, wanaenda kukata wagombea wetu, mnasema twende tu, hatuwezi kukubali,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Eden Mayala amesema kwenye Jimbo la Namtumbo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 wagombea wa chama hicho katika nafasi za udiwani wote walienguliwa.

“Nilikata rufaa kwa wagombea wa udiwani 20 waliokatwa kwa hujuma, lakini majina mawili pekee yalirudi, ni unyanyasaji mkubwa huku wananchi wakipitia wakati mgumu,” amesema.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akihutubia wananchi wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma akiwa kwenye muendelezo wa kutoa elimu ya No Reforms No Election.

Awali, aliyekuwa mgombea wa ubunge Namtumbo, Zamuda Ngonyani amesema wananchi wa eneo hilo wanapitia maisha magumu licha ya kwamba wanazungukwa na rasilimali za kutosha.

“Wanachimba madini yetu, hakuna kinachoendelea, barabara zetu hazipitiki kwa baadhi ya maeneo, ni wakati kwa wananchi kufanya mabadiliko,” amesema.


Lema aunguruma

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema amesema nchi yeyote iliyofikia maendeleo endelevu inajengwa kwa maarifa akitoa mfano kuwa kuna mataifa yametajirika kwa kilimo cha ngano.

“Tanzania yenye rutuba nzuri ya udongo, ngano inaagizwa nje ya nchi, hata ukisema hapa watu wote wahamishwe na vitu vyao vyote halafu Waarabu waje kuishi huku Tanzania, watakuwa matajiri,” amesema.

Amesema kuna nchi zinapigana vita kila siku, lakini inashangaza kuona Namtumbo ambayo ina ardhi yenye kila kitu, mashamba, makaa ya mawe, gesi yote iko kusini lakini watu wake wanaongozwa kwa masikini. 

“Ukifika Dar es Salaam watu wanaofanya shughuli za umachinga wanatoka kusini, mna maeneo ya kutosha ya kulima mazao mbalimbali ikiwemo korosho lakini mmepigwa changa la macho,” amesema.

Naye, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema kutoka Zanzibar, Sheikh Omary Nassor amesema lengo la kuanzishwa mfumo wa vyama vingi Tanzania mwaka 1992 ilikuwa kutoa fursa kwa wananchi kuchagua watu wanaotakiwa kuwa viongozi.

“Na mfumo huo uliletwa ili kutoa ushindani wa kisera na kuondoa dhana ya chama kimoja kutawala, mwisho wa siku kitajisikia na kujiona chenyewe ni kila kitu na kitakuwa kinafanya kazi vile kinavyojisikia,” amesema.


Askofu Mwamakula

Kwa upande wake, Askofu Emaus Mwamakula wa Kanisa la Uamsho la Morovian amesema ukandamizaji unashika hatamu katika nchi pale inapoonekana hadi viongozi wa dini wanakuwa nyuma kukemea.

“Nchi jirani hapa Malawi ulishatokea ukandamizaji lakini ulikoma baada ya wananchi kuungana na kuwa kitu kimoja, ndipo walifanikiwa,” amesema.

Amesema jukumu lililo mbele kwa Watanzania kwa sasa ni kuungana ili waweze kuandika Katiba Mpya na kuundwa upya kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambayo itaruhusu kura ya kila mwananchi kufanya uamuzi.

“Kura yako itasaidia kuondoa mifumo ya ukandamizaji, kuamsha upya na kujenga mifumo ya haki, ili kiongozi yeyote awe wa kuteuliwa au kuchaguliwa, ajenge hofu na kuwa na heshima katika kuwatumikia wananchi,” amesema.