Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu aichambua Kilwa, akoleza darasa la 'No Reform, No Election'

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu akisalimiana na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini,  Aden Mayala walipokutana Kilwa kivinje katika mkutano wa kwanza leo Aprili 4, 2024, ikiwa ni mwendelezo wa Operesheni Kanda ya Kusini.

Muktasari:

  • Lissu amesema Kilwa ilikuwa ngome ya upinzani na wagombea walianza kuenguliwa bila sababu yoyote na ndio maana wanapigania mabadiliko.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ameeleza namna Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi ilivyokuwa ikitawaliwa na vyama vya upinzani, kabla ya wagombea kuanza kuenguliwa.

Lissu amesema enguaengua hiyo ndiyo moja ya sababu kuu za chama hicho kuzuia uchaguzi, huku akisisitiza kama hakutakuwa na mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi hakuna uchaguzi yaani “No Reform, No Election”.

Hayo ameyaeleza leo Aprili 4, 2025 katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika eneo la Kilwa Kivinje wakati akiwa njiani kuelekea mkoani Lindi.

Kiongozi huyo wa Chadema amesema mabadiliko wanayapigania ni CCM kutosimamia uchaguzi na endapo hayatafanyika uchaguzi hautakuwepo.

“Hatutaki tena Tume ya Uchaguzi ya CCM, hatutaki tena wakurugenzi wasimamie uchaguzi kwa sababu wote ni CCM, watendaji wa kata wote ni CCM, hawa walimu wanaosimamia kwenye vituo vya kupiga kura wote ni CCM, hivyo hatutaki tena CCM, tunataka Tume huru,” amedai Lissu.

Amedai uchaguzi unapaswa kusimamiwa na watu wasiotiliwa mashaka na enguaengua ya wagombea wa vyama vya upinzani ikome, wagombea wote washindane kwenye boksi la kura.

Amedai pia wapigakura kuandikishwa upya kwani daftari la sasa lina wapigakura feki wakiwemo watu waliopoteza maisha na wanafunzi wasiostahili.

Suala lingine ni kukomeshwa vurugu wanazofanyiwa upinzani, kampeni zifanyike kwa usawa bila upinzani kuandamwa na polisi.

“Maswala yote yanayohusu mawakala tunataka yabadilishwe, ukiwa na mawakala kuapishwa kwake ni vita, wakishaapishwa majina yao kupelekwa kwenye vituo ni vita, kupata nakala ya matokeo ni vita hawapati,” amedai.

 “Yakifanyika hayo tunaenda kwenye uchaguzi, yasipofanyika tukabane nao tuzuie uchaguzi, mabadiliko hayo yote yanahitaji katiba ibadilishwe na yanahitaji sheria za uchaguzi zibadilishwe na tutengeneze utaratibu mpya,” amesema.

Historia ya Kilwa na upinzani

Akielezea historia ya Kilwa kuwa ngome ya upinzani, Lissu amesema Novemba 2024 kulifanyika uchaguzi wa vijiji Kilwa Kivinje katika vitongoji 21 hakuna mgombea wa upinzani aliyetangazwa,  hata kitongoji kimoja.

“Vitongoji 21 vyote vimekwenda CCM kwa sababu wapinzani wameenguliwa na ndio maana wakashinda mitaa yote 21, upande wa Kilwa Masoko yenye vitongoji tisa wagombe wa upinzani wote walienguliwa na mwaka 2019 kulifanyia uchaguzi na wapinzani wote walienguliwa,” amedai.

Lissu akirejea historia ya mwaka 2014 amesema huo ndiyo ulikuwa uchaguzi wa maana kwa sababu katika mitaa 21 ya Kilwa Kivinje, Chama cha Wananchi (CUF) kilishinda vitongoji vyote 21.

Pia, amesema eneo la Masoko lenye vitongoji tisa, upinzani ulishinda nafasi zote huku Chama cha Mapinduzi kikiambulia sifuri.

“Sio kwa sababu ACT Wazalendo hawapendwi au Chadema hawapendwi ni kwa sababu hawataki uchaguzi, sasa ili kusiwe na uchaguzi wanafuta wagombea wa upinzani, tuliwapiga miaka 10 iliyopita mwaka jana wanasema wagombea wetu hawajui kuandika, hawajui kupiga fomu mihuri,” amedai Lissu.

Kwa upande wa vijiji, Lissu amesema mwaka 2014 Wilaya ya Kilwa ina vijiji 114 na miaka 10 iliyopita CUF ilipata vijiji 75 na CCM vijiji 39 pekee.

Jambo la kushangaza mwaka 2019, Lissu amesema vyama vya upinzani havikupata kura yeyote kwa kile kinachoelezwa wapinzani hawajui kuandika.

Akizungumzia ngazi ya kata, amesema Kilwa kusini yenye kata 11 na kaskazini kata 13 mwaka 2014 upande wa kusini upinzani ulipata kata tisa na CCM kata mbili pekee na kaskazini, CCM ilishinda kata tatu, upinzani ikashinda kata 10.

 “Hiyo ndio hali ya uchaguzi hapa Kilwa, sasa niwaulizeni tukienda kwenye uchaguzi mwaka huu tutapata nini kama hali ndiyo hii watu wa Kilwa, tukisema tuende tu tutapata nini…ndio maana Chadema tumesema kama hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi, tuzuie uchaguzi kwa sababu tukienda hivihivi hatutapata kitu chochote,” amedai.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Godbles Lema amesema Chadema haitasusa uchaguzi bali CCM haitafanikiwa kufanya uchaguzi nchini.

“Maana yake tutawahamasisha nchi nzima siku inayotangazwa kuwa ni ya uchaguzi wananchi tuende barabarani,” amesema.