Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuna nini bungeni?

Muktasari:

  • Wadau wapendekeza kutenganisha uwaziri na ubunge ili kuimarisha mgawanyo wa madaraka. Ubunge pia huonekana kama njia rahisi ya kujikwamua kiuchumi na kijamii.

Dar es Salaam. Makada 5,475 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza kuomba ridhaa ya chama kuteuliwa kuwania nafasi za ubunge katika majimbo mbalimbali nchini katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, ukiacha wanachama wa vyama vya upinzani.

Idadi hiyo haijapishana sana na mwaka 2020, ambapo makada 10,367 walijitokeza kuwania nafasi 358 za ubunge wa majimbo na viti maalumu katika uchaguzi huo.

Sasa, sio wanasiasa pekee, bali wanataaluma, wanazuoni, wafanyabiashara, na viongozi wastaafu wamo miongoni mwa wanaotaka uwakilishi wa wananchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Wingi wa wanachama wanaotaka ubunge unaibua maswali lukuki, ikiwamo kuna nini bungeni, kiasi cha kuvutia makundi haya yote?

Wimbi la wananchi kuzisaka nafasi hizo, linahusishwa na ukubwa wa maslahi, kwa maana ya mshahara, marupurupu, posho za vikao na kiinua mgongo wanavyopata wabunge, kama inavyofafanuliwa na wataalamu wa uongozi na wadau wa siasa.

Ukiacha wenye mtazamo huo, wapo wanaosema watu wanaacha nafasi na taaluma zao kwenda kugombea ubunge wakitarajia wateuliwe kuwa mawaziri, huku wengine wanaona ubunge ni kazi huru inayokupa nafasi ya kuamua nini cha kufanya na muda wa kufanya, bila kusimamiwa au kushurutishwa.

Kuanzia Juni 28 hadi jana, Jumatano, Julai 2, 2025, dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu lilipofungwa kwa CCM, mamia ya wanachama wamejitokeza kusaka kwenda bungeni. Majimbo ya uchaguzi ni 272.


Sumaye ataja maslahi

Katika moja ya mazungumzo yake na Mwananchi, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema maslahi makubwa yanayotokana na nafasi ya ubunge, ukilinganisha na nyingine, ndiyo sababu ya watu wengi kukimbilia wadhifa huo.

“Uwe profesa wa chuo kikuu au uwe mkurugenzi wa taasisi ya umma, au nafasi yoyote ambayo ni nje ya hizo, maslahi ya wabunge ni makubwa. Kwa hiyo watu wanaona kwamba inalipa kwenda bungeni, ndiyo maana mtu anakuwa tayari kuacha kazi ya uteuzi anakwenda bungeni,” amesema.

Katika hoja yake hiyo, Sumaye ametolea mfano ukuu wa mkoa na wilaya, akisema ni nafasi kubwa kiutawala kuliko ubunge, lakini watu wako tayari kuziacha kwa ajili ya kuwa wabunge.

Ukiacha maslahi makubwa, mwanasiasa huyo amesema wimbi lingine la watu kuutaka ubunge linachochewa na dhana kuwa watakapochaguliwa, wanakuwa karibu kuteuliwa kuwa mawaziri.

Kwa mujibu wa Sumaye, hilo linatokea zaidi kwa wataalamu na wanazuoni, ndiyo maana wengi wanatoka vyuo vikuu, wanakwenda kugombea wakitarajia kushinda na baadaye wateuliwe kuwa mawaziri.

Ajira isiyosimamiwa

Kingine kinachosababisha wengi waukimbilie ubunge, amesema, ni kukosekana kwa udhibiti katika kazi ya ubunge, akifafanua hayupo anayekusimamia muda wa kuingia na kutoka kazini.

“Kazi ya mbunge haina udhibiti mwingi, hayupo anayekwambia saa 2 uwe ofisini au asubuhi ukichelewa mstari utapigwa. Ni kazi ambayo unaweza kwenda ofisini saa nne, unaweza usiende ukaenda kwenye shughuli zako binafsi. Ni kazi ambayo watu wanaona ina maslahi mazuri lakini haina pressure,” amesema Sumaye.


Si jambo la kufurahia

Sumaye amesema, si jambo la kufurahia kama Taifa, inapoonekana watu wengi wakiwemo viongozi wa taasisi za umma na wataalamu, wanakimbilia ubunge.

Hoja yake hiyo inatokana na kile alichofafanua kuwa, kama wataalamu wengi waliobobea katika fani mbalimbali watakimbilia bungeni, nchi itatengeneza mapengo na hasara katika sekta muhimu.

Kwa mtazamo wa Sumaye, iwapo maslahi ya mbunge yatalingana na kada nyingine, hakutakuwa na wimbi kubwa la wanaokimbilia nafasi hizo kama inavyoshuhudiwa sasa.

“Naamini kwamba kama maslahi yatalingana na kada nyingine zinazofanana, hiyo itapunguza wimbi la kila mtu kutaka kuwa mbunge. Mimi naamini hicho ndicho kipengele muhimu,” amesema.

Uwaziri usitokane na ubunge

Sambamba na hilo, amependekeza uwekwe utaratibu utakaofanya mawaziri wasitokane na wabunge, kama ilivyowahi kupendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.

“Ukiwa mbunge unakuwa chini ya muhimili wa Bunge na majukumu yako. Kiukweli, mawaziri wako kwenye nguzo ya utendaji, lakini akiwa waziri yuko Serikalini, akiwa upande wa ubunge yuko kwenye Bunge au Legislature – sasa hizi ni nguzo, dola ina nguzo tatu.

“Serikali, Bunge na Mahakama, ni mihimili ambayo kila mmoja unajitegemea. Unaporuhusu mbunge kuwa waziri, maana yake unaruhusu mtu mmoja atumikie mihimili miwili, kwa sababu waziri anaitumikia Serikali,” amesema Sumaye na kuongeza;

“Bunge kazi yake ni kuishauri na kuisimamia Serikali. Unaporuhusu mbunge awe waziri, inakuwa vigumu wewe mwenyewe ujisimamie na kujishauri. Kwa hiyo, kunakuwa na mgongano mkubwa,” amesema.

Kwa mujibu wa Sumaye, eneo hilo lina utata, ndiyo maana ni muhimu kutenganisha uwaziri na ubunge na kuwepo utaratibu utakaofanya anayeteuliwa kuwa waziri asiwe mbunge.

“Najua hili eneo halipendwi. Tume ya Jaji Warioba ililiweka sawa lakini lilipigwa chini, kwa sababu wanaojadili ndiyo hao wanaofaidika kwa kuwa kwenye nafasi hizo,” amesema.

Njia fupi ya kujikwamua

Inawalazimu wengi kuutaka ubunge, kwa sababu ndiyo wadhifa unaoonekana kuwa miongoni mwa fursa kubwa za kujikwamua kimaisha, kama inavyoelezwa na Mkurugenzi wa Mikakati na Mafunzo wa Twaweza East Africa, Dk Baruani Mshale.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, ambaye pia ni mkufunzi wa masuala ya uongozi, kwa uhalisia ubunge haipaswa kuwa nafasi ya mtu kujineemesha, badala yake ilipaswa iwe ya kujitolea.

“Haikupaswa kuwa nafasi ya mtu kujitengeneza ukwasi, kupata fedha, kuwa tajiri. Ilitakiwa iwe nafasi ambayo unajitolea kwa niaba ya wananchi wenzako,” amesema.

Kadri siku zinavyokwenda, Dk Baruani amesema watu wanazidi kuona ubunge ni njia fupi ya kujinufaisha, kutokana na utitiri wa marupurupu, kiinua mgongo, posho za vikao, bima za madaraja ya juu, mishahara na udhamini wa mikopo mikubwa.

Mazingira hayo, kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, yamewafanya watu wavutiwe na nafasi hiyo, ukizingatia si rahisi kupata kiasi kama hicho cha fedha kwa haraka kama utaamua kukitafuta kupitia shughuli nyingine.

Maslahi binafsi

Wimbi lingine la wanaoutaka ubunge, linatokana na kile alichokiita kujiweka karibu na mamlaka, ili ipatikane nafuu ya tozo, kodi zinazohusiana na shughuli zao, aghalabu hii huwa kwa wafanyabiashara.

“Wapo wanaoingia kwenye ubunge ili mambo yao yawanyookee, kama biashara yake imwendee vizuri, asisumbuliwe, asibughudhiwe na tozo mbalimbali na vyombo vingine,” amesema.

Ameeleza wapo wanaoingia wakiwa na nia ya dhati ya kwenda kufanya mabadiliko, lakini wapo wale wanaofanya hivyo wakiamini kuwa karibu na Serikali kutawanyooshea mambo yao.

Pamoja na kuwepo kwa makundi hayo, Dk Baruani amesema wapo wanaoutaka ubunge wakawe sehemu ya mabadiliko ya sheria zinazoonekana kukwaza shughuli fulani, aghalabu hufanywa na wafanyabiashara.

“Mtu anaweza akasema kwa kuwa yeye ana uzoefu wa kufanya biashara na hapendezeshwi na uamuzi unaofanywa mara nyingi, anaamua kuingia katika vyombo vya maamuzi ili ashawishi uamuzi utakaolinda maslahi kama yeye,” ameeleza.

Hoja ya ukubwa wa maslahi katika ubunge, inapingwa na Mbunge wa zamani wa Kibakwe, Isack Kamwelwe, anayesema watu wanadhani kuna fedha nyingi unapokuwa mbunge, lakini uhalisia ni kinyume chake.

Amesema imebaki ikiaminiwa hivyo, kwa sababu hata wanaoingia kwenye ubunge, hawakuwahi kuweka wazi uhalisia wa maslahi yaliyopo,– wanaumia kimyakimya.

“Wanadhani kwenye ubunge kuna hela kwa sababu hata wanaoingia kwenye ubunge, wakikutana na shida hawasemi. Kwa hiyo, haijulikani kukoje.

“Mtu anakuja anaacha kazi, anaingia kwenye ubunge. Sisi huwa tunawahoji, umeacha kazi, umekuja kwenye ubunge – hali ikoje? anakuonyesha kujutia,” amesema.

Ili kuthibitisha hilo, amesema ni vema kuangalia maisha ya wanasiasa waliostaafu ubunge, wanaishije.

Ajira

Kwa upande wa vijana, amesema wengi wanajikuta katika rada za kuutaka ubunge, kutokana na changamoto ya ajira na kwamba wanaona moja ya ajira ni ubunge.

Lakini wengine, amesema wanaingia kwenye vyama kwa malengo ya baadaye, ikiwemo kuwa wabunge.

Kwa upande wake, mtaalamu wa sheria na wakili Rainery Songe alipoulizwa na Mwananchi kuhusu maoni yake alijibu kwa kifupi akisema, “Sehemu pekee ambapo fedha inapatikana kirahisi ni bungeni, kaka.”

Takwimu za kifedha

Ingawa takwimu halisi hazitangazwi hadharani kupitia vyombo rasmi vya Serikali, makadirio yanayoaminika pamoja na taarifa za bajeti zinaonyesha wabunge wanapata marupurupu ya kuvutia.

Mshahara wa kawaida wa mbunge unakadiriwa kuwa kati ya Sh3.8 milioni hadi Sh4.5 milioni kwa mwezi, kulingana na marupurupu mengine na makato ya kodi. Mbali na hayo, wabunge hupokea posho za vikao kati ya Sh240,000 hadi Sh300,000 kwa kila siku Bunge linapoketi.

Kwa wastani wa mikutano mitatu ya Bunge kwa mwaka, inayodumu hadi siku 90 kwa jumla, posho hizo pekee zinaweza kufikia zaidi ya Sh25 milioni kwa mwaka.

Aidha, wabunge wanaoshiriki kwenye kamati za Bunge hupata posho za ziada zinazoweza kufikia Sh10 hadi Sh20 milioni kwa mwaka, kutegemea na mahudhurio yao.

Wabunge wa majimbo pia hupokea posho za kuratibu shughuli za jimbo, zinazokadiriwa kuwa kati ya Sh2 hadi Sh3 milioni kwa mwezi, kusaidia kazi zao katika maeneo wanayotoka.

Wabunge pia hulipwa posho za nyumba na mawasiliano, ambazo huanzia Sh1.5 hadi Sh2 milioni kwa mwezi. Wale wanaosafiri kutoka mbali kwenda Dodoma hulipwa posho za usafiri na mafuta, zinazoweza kufikia zaidi ya Sh10 milioni kwa mwaka.

Mwisho wa muhula wa miaka mitano, wabunge hulipwa kiinua mgongo kinachokadiriwa kuwa kati ya Sh300 milioni hadi Sh400 milioni. Kwa ujumla, mbunge anaweza kujipatia zaidi ya Sh1 bilioni kwa muhula mmoja tu wa ubunge.

Hizi ni kiasi kikubwa ukilinganisha na watendaji wakuu wengine serikalini. Kwa mfano, Mkuu wa Mkoa (RC) au Mkuu wa Wilaya (DC) hupata kati ya Sh3 milioni hadi Sh6 milioni kwa mwezi, bila marupurupu ya ziada kama posho za vikao au safari binafsi, isipokuwa kwa kazi rasmi.

Hali ni kama hiyo hata kwa wasomi na wataalamu wakuu ambao mara nyingi hupata si zaidi ya Sh5 milioni kwa mwezi na mafao madogo zaidi baada ya kustaafu.

‘Kunyemelea uteuzi’

Wapo wanaojitosa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa lengo la kutaka kujisogeza karibu na mamlaka za uteuzi kama wa Mkuu wa Mkoa (RC), Wilaya (DC), Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Wilaya (DAS) – jambo linalobainishwa na kigogo mwandamizi wa CCM. Hata hivyo, ameomba hifadhi ya jina lake.

“Unajua usione hao ambao wanajitokeza, wengi wanataka CV (wasifu) zao zionekane ili hata uteuzi wa nafasi mbalimbali kama RC, DC na mashirika, waonekane kwamba hawa ni wana mfumo,” amesema kiongozi huyo mwandamizi na kuongeza:

“Ukiangalia hawa wengi ambao wanajitosa, sawa na wale wa mwaka 2020 – CV zao zinachukuliwa. Lakini wengine wanajitosa kujulikana julikana tu kwenye jamii, ili uchaguzi ujao waingie sasa rasmi.”

Kwa upande wake, aliyewahi kuwa waziri ambaye sasa anawania tena ubunge, amesema: “Bungeni kuna raha zake, safari na mikopo, ukihitaji unaipata haraka. Lakini ndugu yangu kule unaongeza mtandao wa watu wa hadhi fulani, jambo linalokufanya kutengeneza maisha.”

Mbunge wa zamani wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara maarufu Bwege amesema: “Watu wanataka kwenda bungeni si kwa ajili ya fedha tu. Linakupa hadhi, kinga na fursa. Unakuwa mtu wa maana ghafla.”

Bungara, aliyehudumu jimbo hilo hadi mwaka 2020 aliposhindwa, amesema mbio hizo zinasukumwa na nia halisi ya kuhudumu kwa umma, lakini pia na marupurupu yasiyokanushika.

Mtaalamu wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Helena Swai, amesema kuwa Bunge limekuwa eneo la kuthibitisha hadhi ya kijamii.

"Kwa watu maarufu na wenye ushawishi, Bunge linawapa uhalali. Kwa wasomi, ni nafasi ya kuona sera zao zikitekelezwa. Si vibaya, lakini nia ya mtu ndio msingi," amesema.

Kiu ya kubadilisha maisha ya nyumbani

Mbunge wa Masasi Mjini, Geoffrey Mwambe ni miongoni mwa waliowahi kuwa watumishi wa umma, akitoka kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), na baadaye akaondoka na kwenda kugombea ubunge.

Katika hoja yake kuhusu kwanini watu wengi wanaukimbilia ubunge, amesema nafasi hiyo ni uwakilishi wa wananchi, wakati utumishi wa umma ni ajira kwa ajili ya aliyekuajiri.

Amesema wengi wanalazimika kugombea ubunge baada ya kuguswa na jamii ya nyumbani kwao, wakiona ili kuwe na mabadiliko na matokeo chanya, atalazimika akawe sehemu ya uongozi.

“Kwa sababu anajua anapokuwa mkurugenzi wa taasisi ya umma, pengine hawi na mchango wa moja kwa moja wa kubadilisha jamii ya kwao. Wengi tumekulia vijijini, tunatamani maisha ya kijijini kwetu yabadilike na tunatamani tungetumia uzoefu wetu kuhakikisha angalau maisha ya kwetu yanabadilika,” amesema.

Sambamba na hilo, amesema anaona uongozi ni wito na karama ya kutaka kuwatumikia watu. Unapoiongoza taasisi au mkoa, unajikuta unatamani kufanya zaidi, ndipo mtu anapogombea ubunge.

Sababu nyingine, anasema unapokuwa mkuu wa taasisi ya umma, unakuwa na kiu ya kuchangia na kushiriki kuboresha sera au sheria zinazoigusa taasisi yako, hakuna nafasi nyingine itakayokupa fursa hiyo zaidi ya ubunge.

“Unapokuwa mkurugenzi unakuwa na mamlaka ya kushauri na sio kutunga na kupitisha sheria. Unawiwa, badala ya kusimamia taasisi, sasa unatanua wigo na kupata nafasi ya kutunga sheria na sera,” ameeleza.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi amesema kila mmoja anatumia haki yake ya kikatiba katika kuwania nafasi hizo za uwakilishi.

“Kila mmoja atakuwa anatimiza vigezo, ambavyo ni KK – kusoma na kuandika. Hivyo kila mmoja anaitumia haki yake kuwania kuwa mwakilishi.”

“Lakini pia, lazima tujue kwamba bungeni kuna raha zake – unatunga sheria, unaitwa mheshimiwa. Una nafasi kemkemu ya kupata vipato vya ziada, lakini una nafasi ya kutunga sheria na kutoa miongozo kwa Serikali na nchi kwa ujumla,” amesema Dk Mushi.

Ameongeza kuwa, “Kwa ujumla, bungeni ni patamu, na kazi yake siyo ngumu kama hizi nyingine wanazoziacha,” amesema.