Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM yaonya vikao vya mchujo, teuzi

Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo Chama cha Mapinduzi (CCM),Amos Makalla akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo,kuhusu wanachama waliochukuwa fomu kwaajili ya uchaguzi Mkuu.Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Msingi wa kutolewa kwa onyo hilo ni idadi kubwa ya waliojitokeza kuwania udiwani, ubunge na uwakilishi. Mwanasiasa mkongwe na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Paul Kimiti akumbusha tunu za Taifa.

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa maagizo kwa kamati za siasa za chama hicho kutenda haki na wasionee watu katika vikao vya mchakato wa mchujo kwa watia nia waliomba kugombea udiwani na ubunge ili kupunguza malalamiko na manung’uniko.

Chama hicho kimetoa maagizo hayo siku moja baada ya kufungwa kwa dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania udiwani, ubunge na uwakilishi lililofunguliwa Juni 28 hadi jana Jumatano, Julai 2, 2025.

Msingi wa maagizo hayo ni idadi kubwa ya waliojitokeza, ambayo imevunja rekodi, na hamasa ilikuwa kubwa. Hivyo, wajumbe wanaotembea na orodha zao mifukoni wanapaswa kuziweka kando kwa maslahi mapana ya chama hicho.

Leo Alhamisi, Julai 3, 2025, katika ofisi ndogo za CCM jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla akizungumza na waandishi wa habari amesema makundi mbalimbali, ikiwemo vijana, wanawake na wasanii wamejitokeza, na hiyo inaonyesha CCM ina hazina kubwa ambayo lazima ilindwe kwa kutenda haki katika mchakato huo.

“Takwimu za haraka waliochukua fomu kwa majimbo Tanzania Bara wako 3,585 na Zanzibar wako 524, jumla ya wanachama walioweka nia katika majimbo ni 4,109, na tuna majimbo 272. Unaweza kuona namna hamasa ilivyokuwa kubwa,” amesema Makalla.

Amesema upande wa uwakilishi Zanzibar waliochukua fomu za kutia nia ni wanachama 503, wakati Umoja wa Wanawake (UWT) wako 623 Tanzania Bara na ndani yake wapo 61 kutoka makundi maalumu, lakini Zanzibar wamejitokeza wanane.

“Viti Maalumuu vya uwakilishi kule Zanzibar wako tisa, kwa hiyo jumla ya UWT waliojitokeza ni 640. Umoja wa Vijana wamechukua 161 na Zanzibar wako saba. Jumuiya ya Wazazi Tanzania Bara wako 55, na Zanzibar pamoja na uwakilishi jumla ni 575,” amesema.

Makalla amesema kwa upande wa ubunge na uwakilishi, jumla ni 5,475. Kwa kuwa fomu za ubunge zilikuwa zinatolewa kwa Sh500,000, hii ina maana chama hicho kimekusanya zaidi ya Sh2.7 bilioni.

Kwa ngazi ya udiwani, amesema takribani kuna kata 3,960 bado hazijafanya majumuisho, lakini wanatarajia kuwa na watia nia zaidi ya 15,000 nchi nzima. Gharama za fomu za udiwani ni Sh50,000, hivyo kama idadi hiyo itafikiwa, chama kitapata Sh750 milioni.

Makalla amesema baada ya kukamilika kwa shughuli ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu, kuanzia kesho Ijumaa vikao vya uchambuzi vitaanza kuanzia ngazi ya kata, ambapo kamati za siasa zitaanza kutoa mapendekezo kwa waliotaka kugombea udiwani na viti maalumu.

“Kamati za siasa za mkoa kwa ratiba ya chama zitaanza kukaa Julai 9, 2025 kuanza kufanya uteuzi wa mwisho kwa wanaoomba nafasi za udiwani, lakini uwakilishi na ubunge uteuzi wa mwisho utafanywa na Kamati Kuu kuanzia Julai 19, 2025.

“Katika uteuzi huo tutapata wagombea watatu, na kwa namna wanawake walivyotokeza, tutazingatia jinsia,” amesema.

Makalla amesema mchakato wa mwisho kwa waliotaka udiwani utafanywa na ngazi ya mkoa, lakini kwa uwakilishi na ubunge, Kamati Kuu ya chama itafanya uteuzi huo.

“Wakati wa shughuli hii kamati za siasa zitende haki, mgombea apatikane kwa kuzingatia sifa na uwezo. Wale wenye orodha waziweke kando ili kupunguza minong’ono,” amesema.

Makalla amesema ni muhimu vikao vyote vya mchujo na uteuzi vitende haki kwa makada wote na wasionewe kwa fitina au majungu.

“Tukatende haki, tuteue watu kwa haki na tusionee mtu. Tunapokwenda kwenye uchaguzi tuna mengi ya kusema ikiwemo ilani, lakini yote yatanogeshwa tukiwa na wagombea wazuri,” amesema.

Neno la Kimiti

Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Paul Kimiti, aliyetafutwa na Mwananchi kupata mtazamo wake juu ya kauli ya Makalla, amesema ni muhimu maagizo hayo yazingatiwe kwani misingi ya uongozi ni haki na watu.

“Watu ndio wanaotufikisha kwenye nafasi hizi tunazoziomba. Ni lazima tulipe fadhila kwa kutenda haki na kuonyesha kuwa tunawajali wananchi. Haki lazima izingatiwe kila mahali. Usipofanya hivyo, unapoka haki hata ya wanyonge,” amesema.

Kwa mujibu wa Kimiti, hata Mwalimu Julius Nyerere katika maandiko yake alisisitiza kuwa tunu ya haki lazima izingatiwe ili kuonyesha uongozi sahihi.

“Tuchague mgombea bila kuangalia anatoka wapi. Kama anastahili, mpe haki yake. Kutumia njia za mkato hakutusaidii. Siku hizi kuna vitendo vya rushwa vinavyotisha. Sisi zamani hatukufanya hivyo. Sasa kwa kweli Mungu atunusuru,” amesema.

Amesema baadhi ya watu wanafanya vitendo vya “kufa na kupona” kwa kutumia rushwa kwa kificho, hivyo ni muhimu kwa chama kuwa macho na kuwatendea haki wananchi walioweka matumaini yao kwa CCM.