Prime
KONA YA MALOTO: Majaliwa ameshauriwa, amejishauri au ameukimbia ubunge bila uwaziri mkuu?

Naikumbuka Novemba 27, 2015. Imesalia miezi minne na zaidi ya siku 23, itimie miaka 10. Siku hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikuwa na siku nane tu ofisini. Alifanya tukio ambalo lilibeba tafsiri ya aina ya uongozi wake.
Majaliwa, alitinga Bandari ya Dar es Salaam kwa kushitukiza. Akamsimamisha kazi aliyekuwa Kamishna wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki na viongozi wengine wa taasisi hiyo, kwa upotevu wa makontena 349.
Upotevu huo wa makontena, ulisababisha Serikali ikose mapato ya kodi Sh80 bilioni. Majaliwa alitoa maelekezo ya Masamaki kukamatwa na viongozi wengine tajwa wa TRA. Ulikuwa mwanzo wa zama za Waziri
Mkuu wa “tit for tat”, yaani ukilikoroga, anakushukia mzimamzima na kukusimamia ulinywe.
Wakati huo, ilionekana Majaliwa angekuwa na wakati mzuri ofisini, akifanya kazi chini ya Dk John Magufuli ambaye alikuwa Rais kwa
wakati huo. Magufuli alikuwa Rais mtumbua majipu. Aliongoza nchi kwa mtindo wa kuwaumbua na kuwaaibisha aliowaita majipu.
Magufuli akiwa na siku 22 ofisini na Majaliwa siku nane, mstari ulikuwa umeshachorwa kwamba muhula wa mwaka 2015 mpaka 2020, haukuwa salama kwa wala rushwa na mafisadi. Ilikuwa dhahiri moto ungewawakia wavivu na wakosa uaminifu serikalini na ofisi za umma.
Hazikupita siku nyingi baada ya hapo, Majaliwa alianza kuwa Waziri Mkuu, ambaye sehemu kubwa ya shepu yake ilimezwa na Magufuli. Utendaji wa Magufuli ulimfanya Rais awe kila mahali, Waziri Mkuu alifichwa.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 33 (2) inataja Madaraka ya Rais kuwa ni Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.
Ibara ya 52 (1), (2) na (3), inataja mamlaka ya Waziri Mkuu kuwa ndiye mwenye madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwamba Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni. Na kwamba katika utekelezaji wa madaraka yake, Waziri Mkuu atatekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza yatekelezwe.
Tafsiri ni kuwa waziri mkuu ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali, kwa maana hudhibiti, kusimamia na kutekeleza mambo yote yenye kuihusu serikali.
Mwongozo huo wa kikatiba, unampambanua waziri mkuu kama kiongozi ambaye anapaswa kuwa ‘bize’ na mwenye kuonekana kuliko mwingine yeyote serikalini.
Hata hivyo, Dk Magufuli alikuwa kila mahali serikalini. Hiyo ilisababisha Majaliwa kutoonekana. Na hapo ndipo palipo na tafsiri kuwa shepu halisi ya Waziri Mkuu iliondolewa wakati Magufuli alipokuwa Rais na Majaliwa mtendaji mkuu wa serikali.
Majaliwa wa Samia
Machi 17, 2021, taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilitangaziwa kifo cha Magufuli. Ilikuwa mara ya kwanza kwa nchi, kufiwa
na Rais aliye madarakani. Aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliapishwa kuwa Rais.
Samia alikula kiapo kuwa Rais wa Tanzania, Machi 19, 2021. Hiyo ilikuwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, ibara ya 37, ibara zake
ndogo hasa 2, 4 na 5, pamoja na vipengele vyake. Usahihi kabisa Makamu wa Rais yupo kama Rais wa akiba. Ndiyo sababu, Magufuli alipofariki dunia, Samia alishika hatamu.
Katiba ya Tanzania, ibara ya 37 (5), inaeleza wazi kuwa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kikiwa wazi kutokana na kufariki
dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kwa maradhi, Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliosalia. Halafu Makamu wa Rais baada ya kuwa Rais, atateua Makamu wa Rais baada ya kushauriana na chama chake, kisha uteuzi huo utathibitishwa na Bunge.
Rais Samia alimteua Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais. Bunge lilimpitisha Mpango. Rais Samia pia alitakiwa kufanya uteuzi wa Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri jipya. Hata hivyo, Samia aliendelea na Majaliwa bila kumteua upya.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 57 (2) (f), inaelekeza kuwa Rais mteule anapokaribia kushika madaraka, yaani pale anapokaribia kuapishwa, mawaziri na manaibu wao wote, vyeo vyao hukoma.
Msingi wa ibara hiyo ni kuwa Rais anapokula kiapo kuwa Mkuu wa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sharti ateue Baraza la Mawaziri na awaapishe ili wawe na uhalali wa kuzitumikia nafasi zao.
Sharti hilo siyo kwa Rais mwingine, hata aliyepo anapokuwa mteule, hupaswa kufanya uteuzi upya wa Baraza la Mawaziri. Ndiyo sababu,
Rais anapomaliza muhula mmoja, anapogombea na kushinda wa pili, huteua tena Baraza la Mawaziri. Hapaswi kusema “naendelea na watu wangu walewale.”
Hakatazwi kuendele nao, ila Katiba inataka awateue upya na awaapishe. Ni kwa msingi huo, Rais Samia alitakiwa kumteua upya Majaliwa, athibitishwe na Bunge, kisha amwapishe.
Taswira ipo hivyo. Majaliwa amekuwa Waziri Mkuu, chini ya marais wawili, Dk Magufuli na Dk Samia, chini ya kiapo kimoja. Miaka mwili baada ya Rais Samia kula kiapo na kuendelea na Majaliwa kama Waziri Mkuu, alimteua Doto Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu.
Hiyo ilikuwa inajenga picha ya wazi kwamba Rais Samia hakuona sababu ya kumwondoa Majaliwa, lakini aliona alihitaji msaada, kwa hiyo akamteua Biteko.
Upo ujumbe ambao Majaliwa aliusoma bila shaka, kuwa Rais Samia anahitaji Waziri Mkuu wa tofauti, ambaye atamfanya asihangaike kuteua Naibu Waziri Mkuu.
Uwaziri mkuu bila ubunge
Hesabu kuwa Rais Samia anahitaji Waziri Mkuu tofauti, inaweza kuwa sababu ya Majaliwa kufanya uamuzi wa kutogombea ubunge. Maana, hakuna namna unaweza kuwa Waziri Mkuu bila kupita jimboni.
Katiba ya Tanzania, ibara ya 51 (2), inasema: “Mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku kumi na nne, baada ya kushika
madaraka yake, Rais atamteua Mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika Jimbo la Uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi bungeni au kama hakuna chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi, anayeelekea kuungwa mkono na wabunge walio wengi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.”
Kwa tafsiri hiyo, Waziri Mkuu ni lazima kwanza agombee ubunge na kushinda. Hakuna namna Waziri Mkuu anaweza kupatikana kwa kuteuliwa ubunge.
Hivyo, Majaliwa kwa kutogombea ubunge, maana yake ametangaza kustaafu uwaziri mkuu.
Maswali ya kujiuliza ni je, Majaliwa amejishauri mwenyewe kuacha ubunge ili asifikiriwe na Rais Samia kumteua kuwa Waziri Mkuu, au ameshauriwa kukaa pembeni kwa sababu hana cha kuongeza?
Je, Majaliwa anaona miaka 10 ya uwaziri mkuu inatosha kukaa pembeni, au amejishauri asimsumbue Rais Samia kuwaza jinsi kutomteua?
Yupo mtu amewaza kwamba Majaliwa ameona siyo heshima kubaki mbunge wa dawati la nyuma bila cheo (backbencher), kwa hiyo bora kujiweka kando kwa hiari.
Kama wazo ni hilo, basi ni kosa. Ubunge bila cheo haipaswi kuchukuliwa kama anguko. Ubunge ni cheo kikubwa. Ni uwakilishi. Kama Majaliwa amejipima na ameona hana cha kuongeza akiwa mbunge, sawa, ila siyo kukimbia kukwepa kuwa mbunge wa kawaida.
Tanzania ubunge unatazamwa kama cheo cha kawaida. Mbunge ni mwakilishi wa wananchi na msimamizi wa serikali. Ndiyo maana nchi zote zinazofuata mfumo wa urais, mawaziri huomba kazi na kupitishwa kwenye mchakato wa ajira bungeni.
Kuteua wabunge kuwa mawaziri ndiyo sababu mbunge anapokosa uwaziri, watu hudhani amepoteza, wakati si kweli. Mbunge ni kiongozi mkubwa.