Kiongozi ACT Wazalendo amvaa Waziri upendeleo fedha za Tasaf, mwenyewe amjibu

New Content Item (1)

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Muktasari:

  • Zitto amvaa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Jenister Mhagama amtaka ajitokeze hadharani kutoa maelezo kina kuhusu fedha za Tasaf, mwenyewe ajibu kuwa ameshawaambia wahusika.

Kasulu. Chama cha ACT- Wazalendo, kimemvaa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Jenister Mhagama, kikimtaka kutoka hadharani na kueleza utaratibu wanaotumia kutoa fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf).

Hatua hiyo, inatokana na ACT- Wazalendo kupokea malalamilo ya wananchi  hasa wazee katika maeneo ya mikoa ya Tabora, Ruvuma na Kigoma wakidai kufanyishwa kazi ngumu kwa kigezo cha kupatiwa fedha za mpango huo uliopo chini ya ofisi ya Rais.

Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta Mhagama kupata ufafanuzi wa Serikali kuhusu kauli ya Zitto ambapo amesema," nimeshawaambia Tasaf waandae (ufafunuzi), hebu wasiliane nao," amesema Mhagama.

Juzi akiwa safari kwenda Kigoma  Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto alisimamishwa na wananchi wa Ilolangulu waliomlalamikia mwanasiasa kuhusu mwenendo wa upatikanaji wa fedha za Tasaf katika eneo hilo.

" Hivi baba (Zitto), mimi nasaidia Serikali au Serikali inanisaidia? Hivi kweli na uzee huu naenda kuchimba bwawa halafu narushiwa fedha kwa simu? hivi kweli hadi ili upate fedha za Tasaf ndio ufanye kazi hadi mimi mzee," amesema Dotto Kaduga  akitoa malalamiko yake kwa Zitto kuhusu Tasaf.

Leo  Alhamisi Machi 16, 2023 akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika wanja wa Jumba la Maendeleo wilayani Kibondo mkoani Kigoma, Zitto amesema kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu fedha za Tasaf akisema mbali na hilo pia mpango umekuwa ukitolewa kwa ubaguzi hasa kwa wananchi wa vyama.

“Nimeumizwa sana nilipoelezwa na wazee na watu wenye ulemavu changamoto ya kucheleweshewa kupata malipo ya Tasaf, hata zinapowafikia wanalazimishwa kufanya kazi za nguvu kama vile kuchimba mitaro na mabwawa.

"Pia wanalazimishwa  kufanya usafi kwenye shule au kufyatulishwa matofali kama kigezo cha kupatiwa fedha za Tasaf jambo sio sahihi kwa nchi ya Tanzania," amesema  Zitto.

Zitto aliyewahi kuwa mbunge wa Kigoma Mjini amesema fedha za Tasaf  zimelengwa kwa makundi mbali mbali wapo wanaopata baada ya kutakiwa kufanya kazi (kama Mradi) na wapo wanaostahili kupata kutokana na hali yao ya uzee na ulemavu (ruzuku ya kujikimu).

"Nilichoshangaa wazee  wangu wamenieleza,  wameniambia ili wao wapate hizi fedha wanawajibika kufanya kazi ya kuchimba mitaro au jukumu lingine lolote watakalopangiwa na mamlaka husika," amesema Zitto.

Zitto amedai kuwa fedha za Tasaf hivi  sasa hivi zinatolewa kwa ubaguzi au kutumika vibaya na viongozi wa CCM ili kujinufaisha kisiasa kwa kuwatisha watu wenye vigezo vya kunufaika na mpango huo  kuwa hawatonufaika iwapo hawatajiunga na chama tawala.

“Fedha hizi ni za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB) wahisani wengine, zinalipwa na Watanzania wote bila ya kujali itikadi ya vyama vyao kwa kuwa watakatwa kupitia kodi mbalimbali, haikubaliki kuona watu wa chama au wasiokuwa wanachama wanabaguliwa," amesema.

Zitto ambaye yupo katika ziara ya kuimarisha chama na kusikiliza kero za Watanzania wa mikoa mbalimbali amemtaka Mhagama kujitokeza hadhara na kutoa ufafanuzi wa utolewaji wa fedha hizo za Tasaf.

" Endapo Mhagama atashindwa ACT- Wazalendo kitawaandikia barua wafadhili wa mradi huo kusitisha kutoa msaada kwa kuwa walengwa wake hawanufaiki kama ilivyokusudiwa," alisema Zitto na kupigiwa makofi na wananchi.

Hata hivyo, Zitto amesema njia pekee ya kumaliza tatizo hilo ni  Serikali kuimarisha mfumo wa hifadhi ya jamii kwa wote, " Hii yote ni kwa sababu nchi yetu haina mfumo wa pensheni kwa wazee, haina mfumo wa kuwainua watu wasio na ajira. ACT-  Wazalendo tutaenda kufanya mageuzi ya maisha ya wazee," amesema Zitto.