Kampeni ya C4C yapiga hodi Kanda ya Kaskazini

Muktasari:
- Katika Kanda ya Kaskazini mikutano hiyo inatarajiwa kuanza kufanyika leo Alasiri mkoa wa Arusha maeneo mawili Ngara Mtoni na Usaliver kabla ya kumalizia kesho Arusha Mjini na kuhamia mkoa wa Kilimanjaro, Manyara na Tanga.
Manyara. Mikutano ya Operesheni C4C ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), inapiga hodi rasmi katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini baada ya kumalizika Kanda ya Magharibi.
Chama hicho ambacho leo Alhamisi Juni 12 kinaendeleza kampeni yake hiyo Kanda ya Kaskazini, alasiri kitafanya mkutano wake wa hadhara eneo la Ngara Mtoni na Usaliver mkoani Arusha.
Na kesho kitamalizia Arusha mjini kabla ya kuelekea Mkoa wa Kilimanjaro, Manyara na kitamalizia mkoani Tanga.
Baada ya kumaliza mzunguka huo, viongozi wake watarejea Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya mkutano mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika siku mbili kuanzia Juni 27 na 28, 2025.
Akizungumza na Mwananchi leo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Cchama hicho, John Mrema amesema baada ya kumaliza kwa ngwe ya kwanza ya Kanda ya Kaskazini, “tunarudi Dar es Salaam tutapumzika kidogo na kisha tutaendelea na maandalizi ya mkutano mkuu.”
Mrema amesema baada ya mkutano mkuu, wataendelea na ngwe ya pili ya C4C itakayohusisha Kanda ya Nyasa na Kusini, Kati Pwani na hatimaye Zanzibar.

"Mapumziko hayatachukua muda mrefu, tutaendelea na mzunguko wa pili wa mikutano yetu ya C4C," amesema Mrema.
Mikutano ya C4C yenye malengo manne ikiwamo kukiandaa chama hicho kushiriki Uchaguzi mkuu, ilizinduliwa rasmi Juni3, 2025 katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chaumma, mbali na kukiandaa chama kwa ajili ya uchaguzi, operesheni hiyo inalenga kutambulisha safu ya uongozi wa kitaifa, kujaza nafasi za uongozi ngazi ya mikoa zilizowazi na kupokea wanachama wapya.
Akitoa tathimini fupi ya ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma-Bara, Benson Kigaila amesema mwanzo umekuwa mzuri na matarajio yao wakimaliza watakuwa wamefikia malengo.
"Tukimalizia mikoa ya Kanda ya Kaskazini Chama cha Mapinduzi (CCM), tumekigaragaza na watatepeta kama mkate uliotiwa kwenye chai," amesema.
Kigaila amesema mpinzani wao kwa sasa ni CCM, kwa kuwa anashika dola wanayohitaji kuichukua Oktoba baadaye mwaka huu.
"Hatuwezi kushughulika na vyama vingine vya upinzani kwa sababu hawana jambo la kutuzidi, upinzani ilo kwa CCM walioshindwa kuleta kubadilisha maisha ya wananchi kwa kutumia raslimali zilizopo," amesema kiongozi huyo.