Kadogoo wa Chadema aibukia kongamano la Chaumma, atoa neno

Muktasari:
- Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani, Sheikh Ally Kadogoo amejitokeza katika kongamano la Chama cha Ukombozi wa Umma (Chadema), jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya kujivua uanachama na vyeo vyake, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani, Sheikh Ally Kadogoo ameibukia katika kongamano la Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Hata hivyo, amekana kujiunga na chama hicho kwa kile alichodai msimamo wake ni kwenda mkoani Tabora kufanya shughuli zake za kibiashara ili kujitafutia fedha na atabakia mdau wa kawaida wa kisiasa.
Kongamano hilo la Chaumma linafanyia leo Jumatatu, Juni 16, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila. Kongamano hilo, litatumika kuwapokea wanachama wapya wanaojiunga na chama hicho.
Wanachama zaidi ya 200 watajiunga na Chaumma, ikiwa ni mwendelezo wa chama hicho kuendelea kuhamisha wanachama wa Chadema tangu kilipoanza kufanya hivyo kwenye mkutano maalumu uliofanyika ukumbi wa Ubungo Plaza Mei 23, 2025.
Mwananchi limezungumza na Kadogoo kujua kama anajiunga rasmi na Chaumma, lakini katika maelezo yake amekana kujiunga na chama hicho na kujitokeza kwake katika kongamano hilo ni kutaka kuunga mkono uamuzi uliochukuliwa na wanachama hao.
"Nimekuja kuwaunga mkono uamuzi waliochukua ni sahihi, si kwamba nataka kujiunga Chaumma, unajua hawa walinipokea kule Chadema nimekaa nao kindugu kabisa ili kuwa ni busara nije kuwasalimia," amesema Kadogoo.
Amesema hapo wanapofanyia mkutano huwa anapaki magari yake baada ya kumuona wengi walimtaka akazungumze nao na alishindwa kukataa: "Nikaona niwape neno la faraja."
Awali, akizungumza katika kongamano hilo Kadogoo amesema pamoja na kuchukua umuzi huo sahihi, aliwahusia makada hao kuwa wavumilivu wakati wote.
"Vita haipiganwi katika majukwaa ya kijamii, ingawa inahitajika nidhamu na heshima vyama vya upinzani ilikufanya kazi kunahitaji kujitolea, kuvumiliana, mnaweza kufika mbali, iwapo mtavumilia," amesema.
Amesema uamuzi wake kwa sasa, baada ya kujivua unachama wa Chadema atapumzika kujihusisha na siasa na anaenda Tabora kufanya shughuli za kibiashara ili apate fedha.
"Niwahakikishie sina mpango tena wa kugombea udiwani, ubunge wala urais, wala kitu chochote ingawa kuna maeneo mengi zaidi wananisema mtandaoni kwamba nimeondoka Chadema eti nina njaa ni maneno niliyozoea," amesema.
Kadogoo amesema alikuwa Mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), kabla ya kujiunga na Chadema lakini alichogundua siasa haina shukrani akitomlea mfano Mwenyekiti wa zamani wa Chadema, Freeman Mbowe aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 20 akitumia rasilimani zake lakini mwisho wa siku alidharauliwa.
"Mara kalambishwa asali, lakini kuna mambo yanaendelea ndani ya chama mkubwa hajulikani ni nani, mnazungumza mambo mengi na ndicho hata mie kilinisukuma kukihama Chadema busara hakuna kabisa," amesema Kadogoo.
Kadogoo alikuwa Makamu mwenyekiti wa Kanda ya Pwani yenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na Mwenyekiti wa kanda hiyo ni Boniface Jacob maarufu kama 'Boni Yai'.
Kutojiunga na chama chochote
Kadogoo amesema tangu jana Jumapili alipotangaza kujivua uanachama amekuwa akipigiwa simu kutoka kwa viongozi mbalimbali wakitaka ajiunge na chama hicho.
"Nimesema Hapana, nimeomba kwa sasa nitulie nifuatilie mambo yangu nitakapoona kuna haja nitashiriki kwa maana ya kuunga mkono," amesema Kadogoo.
Akizungumzia kongamano hilo, Mwenyekiti wa Kata ya Kiwani, Sailas Mwongi amedai wanachama zaidi ya 200 kutoka Chadema watajiunga Chaumma.
"Naratibu shughuli hii, wanachama zaidi ya 200 watakihama Chadema na kujiunga na Chaumma, huu ni mwanzo bado wengine wanakuja," amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi