Juvicha yawaita vijana kujadili Katiba Mpya, fursa za ajira
Kiongozi wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Ukombozi wa Umma(Chaumma), Masoud Mambo akizungumza na waandishi wa habari.
Muktasari:
- Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Juvicha, Masoud Mambo maadhimisho hayo yamepewa kauli mbiu ya ‘vijana wakati ni sasa’ yatafanyika jijini Dar es Salaam Agosti 12, 2026 ambayo huadhimishwa kidunia pia.
Dar es Salaam. Jukwaa la Vijana la Chama cha Ukombozi wa Umma (Juvicha) unawaalika vijana wa vyama mbalimbali vya siasa nchini kushiriki maadhimisho ya Siku ya Vijana Dunia yatakayojadili upatikanaji wa Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Juvicha, Masoud Mambo maadhimisho hayo yamepewa kauli mbiu ya ‘vijana wakati ni sasa’ yatafanyika jijini Dar es Salaam Agosti 12, 2026 ambayo huadhimishwa kidunia pia.
Amefafanua lengo la kauli mbiu hiyo ni kuwahamasisha na kuwakumbusha vijana kuwa kesho yao iliyobora na kujaa matumaini ya vizazi vilivyopo na vijavyo inategemea hatua na uamuzi watakaouchukua kuanzia hivi sasa.
Mambo amesema hayo jana Alhamisi Juni 24, 2026 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu maadhimisho hayo ambayo dunia huadhimishwa Agosti 12 ya kila mwaka.
“Vijana wakati ni sasa ni wakudai haki katika Taifa, Katiba Mpya, ongezeko la fursa za ajira nchini, kupinga utekaji, kupinga gharama za maisha, uvujaji wa mali zao na mifumo mibovu ya elimu,” amesema Mambo.
Kiongozi wa Juvicha amesema maadhimisho hayo yatakuwa ya kihistoria yatakayokusanya maelfu ya vijana kutoka kila kona ya nchi watakaojadili changamoto zote zinazowakabili.
“Tutajadili kuhusu fursa tulizonazo, lakini tumezikosa kutokana na Serikali iliyopo. Tutakutana kujadili mustakabali wa Taifa letu, kama ambavyo nimesema wakati ni sasa, tukishindwa kuchukua hatua stahiki sasa hivi kesho yetu itakuwa mikononi mwa nani? Anahoji.
Amesema vijana wa Chaumma hawakubaliana na msemo kwa vijana ni Taifa la kesho bali vijana ni Taifa la leo na kesho na watachukua hatua stahiki za kufanya uamuzi utakaoweka kesho yao bora.
“Maadhimisho haya si vijana wa Chaumma pekee, bali yanawahusu wote iwe ni CCM, CUF, Chadema, NLD, ACT au Demokrasia Makini unakaribishwa ili kuadhimisha siku hii adhima,” ameeleza Mambo.
Akizungumzia hatua hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, Ruqayya Nassir amesema hadi sasa bado hawajapata mwaliko kuhusu maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Juvicha Agosti 12, mwaka huu.
“Ngome ya vijana ya ACT Wazalendo ni taasisi, kwa hiyo mwaliko ukija tutakaa na kujadili, maana sisi ni vijana na siku hiyo tutakuwa mpango yetu kama ngome kuadhimisha. Mwaliko ukija tutaujadili na inawezekana tukatuma mwakilishi,” amesema Ruqayya.