Prime
MAHOJIANO MAALUMU: Salum afunguka siri ya ukwasi wa Chaumma uchaguzi wa 2025
Muktasari:
- Mapema mwaka jana, baada ya uchaguzi wa ndani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baadhi ya makada wake, akiwemo Mwalimu, walikihama chama hicho na kuhamia Chaumma.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, amefichua siri ya ukwasi uliokuwepo ndani ya chama hicho miezi michache kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka jana.
Kwa mujibu wa mtendaji mkuu huyo wa chama hicho cha upinzani, hawakuwa na mfadhili mmoja katika kipindi hicho, na kwamba walifadhiliwa hata na watu kutoka ndani ya Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mapema mwaka jana, baada ya uchaguzi wa ndani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baadhi ya makada wake, akiwemo Mwalimu, walikihama chama hicho na kuhamia Chaumma.
Hatua hiyo ilifuatiwa na kishindo cha matukio yaliyoonesha ukwasi ndani ya Chaumma, ambayo awali haikuweza hata kufanya mikutano yake katika kumbi kubwa nchini.
Picha linaanza! Pasi kutegemewa, chama hicho kilitangaza kufanya kikao chake cha Kamati Kuu katika moja ya ukumbi wa hoteli ya kifahari iliyoko eneo la Masaki, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilifuatiwa na lingine la kuwapokea wanachama wapya, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, eneo ambalo chama hicho hakikuwahi kulitumia kufanyia mikutano yake. Kisha ikafuata ziara ya Oparesheni ya Chaumma for Change (C4C).
Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu akifanya mahojiano maalumu na Mwandishi wa Mwananchi Juma Issiaka
Katika oparesheni hiyo, chama hicho kilitumia helikopta na msururu wa magari kuzunguka mikoa kadhaa nchini, jambo lililozidisha mjadala wa wapi fedha hizo zinatoka.
Mwalimu amesema hayo wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini, jijini Dar es Salaam.
Nani mfadhili wa Chaumma?
Alipoulizwa iwapo chama hicho kilikuwa na mfadhili, Katibu Mkuu huyo amesema hakukuwa na mtu mmoja aliyewafadhili, isipokuwa walihamia Chaumma wakiwa na mikakati ya kukipa hadhi chama hicho kiwe na mvuto kwa wananchi.
“Hakukuwa na mfadhili kusema kwamba yule ndiye mfadhili wa chama. Lazima kwenye siasa uonyeshe watu tunachokitafuta tunakimudu, tuna uwezo nacho. Sasa hapa kuna kujitoa mhanga kwenye mambo mengi,” amesema Mwalimu.
Mazingira hayo amesema yanaweza kumfanya mtu ahisi kuna fedha, lakini zilizotumika ni akili, mikakati na mbinu ili kujenga taswira njema ya chama kiheshimike na kukipa hadhi ya kuwa chama kinachoweza kushinda uchaguzi.
Mbali na akili na mbinu ya kujenga taswira ya chama, amesema pia kulikuwa na watu waliokuwa wakifurahishwa na wanachokifanya, hivyo walijitoa kuwachangia fedha na hata magari kwa ajili ya ziara.
“Kuna wakati unaweza ukakaa ukapokea ujumbe, na wakati mwingine mtu hata humjui, akakwambia kama utaridhia naomba peleka gari tatu kesho asubuhi kituo cha mafuta fulani jaza mafuta, na humjui, na ukimpigia simu hapokei,” amesema.
Amesema kuna wengine walikuwa wakilipa hata hoteli, kuwapa magari ya kufanyia ziara mikoani, kutuma fedha, na hiyo ilifanywa hata na marafiki zake.
Amesema michango hiyo waliipokea pia hata kutoka kwa wanachama wa chama tawala na watu wa serikalini, ingawa hawakuwahi kupokea kutoka CCM kama taasisi au serikalini moja kwa moja.
“Nina watu wako sehemu mbalimbali, na wengine wako serikalini, wengine wako CCM, wengine wako kwenye vyama vingine vya upinzani. Kusema kwamba bwana tuna ziara hii, huyu akasaidia hiki, huyu akakusaidia kile hao wapo.
“Lakini siyo chama kama CCM eti kimekaa sasa kikasema Salum Mwalimu huu mzigo wako kutoka kwetu, hapana sijawahi, na Mungu aninusuru,” amesema Mwalimu.
Imekata pumzi?
Alipoulizwa imeishia wapi nguvu hiyo, amesema haijaisha, isipokuwa shughuli za sasa hazilingani na zile za nyakati za uchaguzi.
“Hakuna chama cha siasa, maisha yake wakati wa kampeni ndio maisha yake ya kawaida muda wote, haiwezekani. Ule ulikuwa ni wakati wa kukitengeneza chama kwa ajili ya kuwashawishi watu wakipigie kura,” amesema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi.
Amesisitiza si kwamba wameishiwa pumzi, bali ni nyakati zimebadilika na kwamba chama kinaendelea, na shughuli mbalimbali zinaendelea pia.
Amesema wameshatangaza kufanya oparesheni itakayoshuka ngazi za chini hivi karibuni.
Kwa nini Chaumma?
Katika mahojiano hayo, Mwalimu ameelezea uamuzi wake wa kuhamia Chaumma kwamba ulitokana na kutokukubaliana na msimamo wa kilichokuwa chama chake cha Chadema wa kutoshiriki uchaguzi mkuu.
“Tumeafika mahala tumetofautiana kwenye kutokushiriki uchaguzi. Ni jambo ambalo sijawahi kuliamini, siliamini, na sidhani kama nitakuja kuliamini. Sasa kama mwenendo ni huo, na mimi nimeshawaambia kwamba nimejipanga na nimejiandaa kugombea ubunge wa Kikwajuni, basi mimi nafikiri tuachane kwa amani, kusiwe na ugomvi, kusiwe na kelele,” amesema.
Hata hivyo, amesema aliwaaga makada wa Chadema tangu mwaka 2021, akiwaambia baada ya kumalizika kwa muhula huo wa uongozi hatakuwa tayari kuwa sehemu ya uongozi wa chama hicho.
“Na Januari 21, 2025 pale Mlimani City nilipopewa nafasi ya kuaga, nilirejea na nikashukuru kwamba nilipoaga watu walinielewa,” amesema.
Kustukizwa kugombea urais
Alipoulizwa kwa nini alipohamia Chaumma hakwenda kugombea ubunge Kikwajuni kama alivyodhamiria awali, amesema wenzake ndani ya chama hicho walikuwa wanamuwazia nafasi ya kugombea urais.
“Unajua mambo haya wakati mwingine wewe unaweza ukaona hivi, wenzako wakaona vile. Kwa hiyo mimi mipango yangu ilikuwa ni ubunge, lakini wenzangu wakaona tofauti dakika ya mwisho kabisa kwamba nipeperushe bendera ya chama kwenye nafasi ya urais,” amesema.
Hali hiyo ya kushtukizwa amesema ilimtokea hata alipoteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais mwaka 2020 akiwa Chadema, kwani hakutarajia, ilikuwa ghafla.
Mwalimu amesema hata yeye anasikia kauli kwamba Chaumma ilikuwa na mgombea mwingine wa urais kabla ya kuteuliwa yeye, akisema kwenye chama hicho walikuwa na mipango yao.
“Kama kulikuwa kuna maneno basi tuyaache tu hayo maneno, kwa sababu huwezi ukayajibia maneno. Maneno ni mengi na huwezi ukajibu yote, lakini kwenye chama sisi tulikuwa tuna mipango yetu na tulikuwa tuna mikakati yetu, na wakati tunapanga kumbe wenzangu hao wananiangalia mimi bila mwenyewe kujua,” amesema.
Kuhusu utofauti wa kuwa mgombea mwenza na mgombea urais, Mwalimu amesema ukigombea urais unakuwa wa mwisho, wakati mgombea mwenza unamwombea kura mgombea urais.
“Nilipokuwa mgombea mwenza 2020, nilikuwa na kazi kubwa sana ya kumuombea kura mgombea wangu wa urais, kwa hiyo nilikuwa na wajibu wa kumuelezea, kumpamba, kumjengea hoja, kueleza sifa zake kwa nini wamchague yeye na si mwingine,” amesema.
Lakini alipokuwa mgombea urais, amesema hayo yote unayafanya kwa ajili yako binafsi, ikiwemo kujizungumzia, jambo alilosema ni gumu.
Chaumma ni mradi?
Kuhusu uvumi kuwa chama hicho ni mradi wa Serikali, Mwalimu amesema anachukulia maneno hayo kama michezo ya kisiasa na mara nyingi anayapuuza.
“Ukiwa kwenye siasa utaijua michezo ya kisiasa. Yaani chama project (mradi) vipi? Na hamna mtu atakupa maelezo ataishia hapohapo chama project, wewe huwaoni? Kuwaona wanazunguka huko mikoani kwa kila anayezunguka mikoani ni project. Ndio tunachosema mtu ataishia hapo tu,” amesema.
Itaendelea kesho