Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu avunja ukimya madai kusubiri uteuzi

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, amefunguka kuhusu uteuzi na ukaribu wake na Rais.



Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, amevunja ukimya kuhusu tetesi za kusubiri kuteuliwa serikalini, akisema atapokea uteuzi iwapo nafasi husika haitakinzana na misimamo ya chama chake.

Sambamba na hilo, ameeleza kuhusu aina ya ukaribu alionao na mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan, akisisitiza sio wa kirafiki bali ni masuala rasmi kama kiongozi mwenzake wa kisiasa.

Aidha, amezungumzia msimamo wa chama hicho kuiunga mkono tume na ripoti yake ya uchunguzi wa ghasia wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Oktoba 29, mwaka jana akisema, walijiridhisha na sifa za wajumbe na ripoti imegusa maeneo yanayolalamikiwa na wengi.

Mwalimu ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Amesema hata yeye amekuwa akisikia kuhusu tetesi za yeye kuteuliwa kushika nafasi serikalini, ingawa hakuwahi kuambiwa na mamlaka ya uteuzi wala kuona jina lake katika orodha ya wateuliwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi.

“Nazisikia tu, sasa unajiuliza sasa uteuzi gani hausemwi, nikiangalia PDF simo,” amesema baada ya kuulizwa kuhusu tetesi za kusubiri uteuzi. 

Alipoulizwa iwapo itatokea yuko tayari, Mwalimu amesema inategemea na aina ya nafasi atakayoteuliwa kuhudumu, kama inakinzana na misimamo ya chama chake hatakubali.

“Inawezekana ukateuliwa kuna vitu vingine labda vikakinzana na misimamo ya kitaasisi, itakuwa shida na hiyo sitokubali kwa gharama yoyote kuisaliti taasisi ninayoitumikia, iliyoniamini ikanipa nafasi hii kwa maslahi yangu binafsi,” amesema.

Amesisitiza katika nafasi aliyonayo sasa ndani ya Chaumma, haitatokea akakubali kufanya jambo lolote kwa kutanguliza maslahi yake binafsi, huku akiacha ya chama hicho.

“Niwahakikishie wanachama wenzangu, haitatokea maslahi yangu binafsi yakawa mbele ya maslahi ya taasisi iliyoniamini,” amesema.

Hata hivyo, amesema hata ikitokea ameteuliwa atashauriana na chama chake na kuona kama nafasi husika haitaleta athari kwa maslahi ya Chaumma atapokea.

“Ni swala la mashauriano, mnashauriana mtasema bwana hili halina mkwamo wowote na pengine litasaidia chama kukua, litasaidia chama kujitangaza, litasaidia chama kuimarika chama kitaamua kisha tutaendelea,” amesema Mwalimu.

Pia, amesema yeye si miongoni mwa wanasiasa wenye uchu wa madaraka, kwa kuwa ameishi katika nafasi ambazo alikuwa karibu na mamlaka muda mwingi.

“Nilipokuwa kwenye nafasi za ajira, nilikuwa naogelea kwenye korido za mamlaka kwa sababu mnafanya kazi na Serikali kwa ukaribu zaidi, kwa hiyo unaogelea kwenye hizo korido,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu akifanya mahojiano maalumu na Mwandishi wa Mwananchi Juma Issiaka

Ameeleza majukumu yake akiwa mfanyakazi wa baadhi ya nafasi kabla ya siasa, yalimfanya awe karibu zaidi na Serikali, Bunge na viongozi wengi wa Serikali.

“Kama ningeamua ni mtu ninaamini katika siasa hizo, nilipochagua kuondoka au kuja kwenye siasa za mstari wa mbele ningekwenda lakini, kwangu mimi ukiniambia wewe njoo kwa sababu upate cheo, sio kitu nilichokuwa nakitafuta,” amesema.


Kuhusu ripoti ya tume

Mtendaji mkuu huyo wa Chaumma, amesema uamuzi wa chama hicho kuiunga mkono tume na ripoti yake, umetokana na kugusa mambo ambayo wengi wanayalalamikia ikiwemo suala la Katiba Mpya.

Amesema hawakuona sababu ya kuipinga tume hiyo hasa baada ya kuona sifa za wajumbe wake. Hata hivyo, ilikuwa mapema kuipinga, wakati ambao hata haijatoa ripoti.

Amesisitiza ripoti hiyo imegusa maeneo ambayo vyama vya siasa hasa vya upinzani vimekuwa vikiyalalamikia na hivyo huenda ripoti ndiyo ikawa chanzo cha jawabu.

Amesema jambo muhimu ni wadau waungane kuishinikiza Serikali itekeleza mapendekezo ya tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Chande Othman.

“Nani leo chama chake kimekaa kimejadili hakikusema kwamba tuna tatizo la vijana na ugumu wa maisha kwenye nchi hii. Sasa tume ikiyasema tukaunga mkono kuna watu watatupiga mawe lakini watu walewale wanarudi wanayasema na wenyewe yaleyale. Sasa hapa tuna tatizo,” amesema Mwalimu.


Makada wanaotaka kurudi Chadema

Kuhusu madai ya baadhi ya makada wao kutaka kurudi Chadema, Mwalimu amesema amewahi kusikia na hana pingamizi dhidi ya uamuzi wa yeyote kuhusu hilo, kwa kuwa atakuwa anatimiza haki yake.

“Ni haki yao, mimi si niliondoka (Chadema) nikaja huku (Chaumma), sasa hiyo dhambi ya wao kutoka kwenda kwingine inatoka wapi,” amesema.

Hata hivyo, amesema linapotokea jambo kama hilo, kama chama na viongozi wake wanafanya jitihada za kumuuliza mwanachama husika iwapo kuna tatizo na ikitokea mwanachama amekataa anamwacha kwa sababu ni haki yake.

“Kama mimi nilitumia hiyo haki kwenye maisha yangu, nikuzuie wewe usiitumie haki yako mimi ni nani. Ni haki yao wana uhuru kwa sababu wakati mwingine mtu anakuwa ameshaamua,” amesema.

Amesema mwanachama yeyote ambaye anadhani anakwazika na akafikisha taarifa kwenye chama na ikashindikana kumshawishi na kumsaidia, ana haki ya kuamua vinginevyo.

“Lakini kama tutatimiza wajibu wetu tukamsaidia kwa uwezo wetu wote tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu na bado akawa haoni hizo juhudi, ana uhuru, utafanya nini sasa,” amesema.


Ana ukaribu na Rais?

Alipoulizwa kuhusu ukaribu wake na mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan, Mwalimu amesema ukaribu wao sio wa maisha binafsi, bali ni mambo ya kisiasa kama ilivyo kwa wanasiasa wengine wa upinzani.

“Bila shaka naweza nikamfikia kwa sababu mimi ni katibu mkuu wa chama, mnapokuwa na jambo ni rasmi mnaweza mkafikiana, kama ni kumwandikia barua, kama kumtafuta kupitia kwa wasaidizi wake,” amesema.

Ameeleza ukaribu wao unaishia kwenye masuala ya msingi kama kiongozi mwenzake wa kisiasa, lakini si nje ya hapo na vinginevyo.

“Kuna mtu mmoja aliniambia yaani wewe jamaa tunakuona Ikulu tu, kwa nafasi yangu kama katibu mkuu wamealikwa makatibu wakuu utaachaje kuniona,” amesema.

Amesema uhusiano na ukaribu wao ni wa matukio rasmi kwa sababu ni kiongozi mwenzake wa kisiasa na panapohitajika mawasiliano yanafanyika.

Alipoulizwa iwapo wao ni marafiki, amesema; “ukiita marafiki hapana ni mtu ninayemheshimu tu. Si kwamba naweza nikampigia simu mheshimiwa Rais shikamoo... mambo vipi.. hiyo hatua sijafika. Yeye ni Rais ni mtu ninayemheshimu, kwangu mimi ni mama, ninamheshimu sana tena sana tu.”

Alipoulizwa heshima hiyo haimaanishi kuwa ni mfuasi wake, amejibu wengine wanasema hivyo ilimradi kumrushia maneno ili kumchafua, akisisitiza falsafa yake ya siasa si kujenga uadui na anayepishana naye kimtazamo.

“Kwa watu wanaonijua vizuri haijalishi wewe ni nani. Nikiwa kwenye siasa, ni mtu unayezungumza nafsi yangu, haijalishi wewe ni nani isipokuwa nitakueleza kwa ustaarabu,” amesema.

Amesema hata kama atakosoa, atafanya hivyo kwa ustaarabu, hawezi kutukana na inapobidi anaweza kufanya hata mawasiliano na mhusika kuzungumza naye faragha na sio hadharani.