INEC: Changamoto ya mawakala tumejirekebisha
Muktasari:
- Jumatano ya Oktoba 29, 2025, Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Urais huku Tume ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikisema imejifunza juu ya changamoto za mawakala katika chaguzi zilizopita.
Dar es Salaam. Katikati ya malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu changamoto wanazopitia mawakala wao ikiwemo kuenguliwa au kukosa utambulisho, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema imejirekebisha katika hilo na kuweka taratibu za kuondokana na kadhia hiyo.
Kutokana na hatua hizo, INEC imesema katika chaguzi ndogo zilizofanyika, hakukuwa na changamoto kwa mawakala hao na imevisihi vyama vya siasa kuwasilisha kwa wakati majina ya mawakala wao kwa mujibu wa sheria ili waapishwe na kuandaliwa utambulisho mapema.
Wakati tume ikiyasema hayo, vyama vya siasa vimesema maneno pekee hayatoshi, badala yake kuwepo mwongozo utakaowazuia wasimamizi kuruhusu uchaguzi kuendelea, iwapo mawakala wote hawatakuwa wamefika.
INEC inakuja na kauli hiyo, zimeshapita chaguzi kadhaa ambazo vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamikia kunyimwa haki kwa baadhi ya mawakala wao, ama wanachelewa kuapishwa, wengine wakinyimwa barua za utambulisho.
Changamoto nyingine ni mawakala kuzuiwa au kucheleweshwa vituoni na utaratibu wa viapo vinavyotolewa katika ofisi ambazo mara nyingi zinawapa ugumu kuzifikia.
Kilio cha mawakala ndicho kilichosababisha maandamano ya Chadema kwenda ofisi ya Mkurugenzi kudai barua za utambulisho wa mawakala, tukio hilo, lilisababisha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini kupigwa risasi na kuuawa akiwa kwenye daladala baada ya Polisi kutumia silaha wakati wa kutawanya maandamano.
Kauli ya INEC
Leo, Ijumaa Agosti 1, 2025, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima ameeleza hayo wakati wa kikao kati ya tume hiyo na na wahariri wa vyombo vya habari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.
Amesema tume hiyo imezifanyia kazi changamoto mbalimbali za mawakala katika chaguzi zilizopita na kuwa hazitatokea kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
“Angalia mwenendo wa tume wakati wa uchaguzi mdogo, hakukuwa na changamoto za mawakala, tumekwisha kujirekebisha kutokana na changamoto zile,” amesema.
Amesema mawakala safari hii wataapishwa kwenye kata na viapo vyao vikiwa pamoja na picha zao watavikuta kwenye vituo vua kupigia kura.
Amevitaka vyama kuhakikisha vinawasilisha majina ya mawakala kwa wasimamizi wa uchaguzi siku saba kabla ya siku ya kupiga kura.
“Tunawaomba ninyi wahariri, mvihamasishe vyama vya siasa kuhakikisha vinawasilisha majina ya mawakala kwa mujibu wa sheria yaani Oktoba 22,” amesema Kailima.
Mbali na hilo, mkurugenzi huyo wa uchaguzi amesema jumla ya vituo ya kupigia kura 99,911 vitatumika. Kati ya vituo hivyo, 97,349 vipo Tanzania Bara na 2,562 Zanzibar.
Vituo hivyo ni ongezeko la vituo 18,344 kutoka vituo 81,567 vilivyotumika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Awali, akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele amesema maandalizi muhimu kwa ajili ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri, ikiwemo kukutana na makundi mbalimbali.
Maneno matupu
Akizungumzia ahadi hiyo ya INEC, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita amesema tatizo la mawakala halikuwa la kisheria, bali ni uendeshaji mbovu uliosababishwa na Tume.
Kwa sababu ya ubovu wa uendeshaji huo, amesema wasimamizi wa uchaguzi kwa makusudi waliamua kutowapa barua za utambulisho na wasaidizi wao walitumia nafasi hiyo kufanya uharibifu zaidi.
Katika hatua iliyopo, amesema INEC inapaswa kuuhakikishia umma kuwa ucheleweshaji huo wa barua kwa mawakala hautakuwepo na waeleze mapema wapi wataapishwa.
Mchinjita amesema pia kuwepo na mwongozo unaotaka uchaguzi usiendelee katika eneo ambalo mawakala wote hawatakuwa wamefika.
“Haitoshi tu kusema sheria, inatakiwa tume itoe mwongozo utakaokuwa umewahusisha wadau wote, na unaomzuia msimamizi asipokuwa na maelezo yanayokubalika kisheria asianzianze uchaguzi, isipokuwa mawakala wote watakapokuwepo katika eneo husika,” ameeleza Mchinjita.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe amesema bado hawajaona marekebisho hayo, hivyo inakuwa vigumu kuamini.
Ameeleza wanachotamani ni kuona matokeo, badala ya ahadi na maneno mazuri kuhusu mwenendo wa uchaguzi husika.
“Sisi bado hatujaona marekebisho itabidi tusubiri tuone, tukiona sasa hapo tunasema sawa,” amesema mwenyekiti ambaye pia ni mwasisi wa chama hicho.