Prime
Gwajima aingia mitini jimbo la Kawe

Muktasari:
- Katibu wa CCM Kinondoni, Amos Richard amethibitisha kutokuwapo kwake kwenye orodha ya wagombea 37 waliorejesha fomu.
Dar es Salaam. Wakati uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba ridhaa ya kuwania ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ukitamatika leo, Julai 2, 2025, mbunge wa Kawe anayemaliza muda wake, Joseph Gwajima, si miongoni mwa walioomba ridhaa hiyo.
Gwajima, aliyeliongoza jimbo hilo kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, kutokuchukua fomu ya kutetea nafasi hiyo ni dhahiri ameachia kijiti kwa watia nia wengine waliojitosa.
Akizungumza na Mwananchi leo jioni, Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Amos Richard, amethibitisha kuwa Askofu Gwajima hakuomba ridhaa hiyo mpaka dirisha linafungwa saa 10:00 jioni.
CCM ilitoa siku tano kwa makada wake wenye nia ya kuomba ridhaa ya kugombea kuchukua na kurejesha fomu kuanzia Juni 28 hadi leo, saa 10:00 jioni.
Richard amesema walifunga kazi ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu katika wilaya hiyo kwa makada 61 kujitokeza kutangaza nia ya kuwania ubunge katika majimbo mawili ya wilaya hiyo ambayo ni Kawe na Kinondoni.
"Kawe pekee jumla ya watia nia 37 wamejitokeza kuchukua na kurejesha fomu," amesema Richard.
Akijibu swali kuhusu Askofu Gwajima kama amechukua fomu, Richard amesema mpaka anahitimisha kazi hiyo, hakuwa miongoni mwa waliojitokeza.
"Kama nilivyosema, kwa Jimbo la Kawe tumefunga tukiwa na wanachama 37 waliochukua fomu. Askofu Gwajima hajachukua," amesema.
Mbali na Kawe, Richard amesema kwa Jimbo la Kinondoni mpaka wanahitimisha, makada waliochukua na kurejesha fomu walikuwa 24.
Hatima ya Askofu Gwajima kurejea bungeni kupitia CCM ilianza kuwa njia panda tangu Mei mwaka huu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzungumza katika Mkutano Mkuu wa CCM, akiwataka wajumbe wa vikao vya chama hichio kufanya uchujaji wa haki na uadilifu, lakini wale ‘magwajima’ waachwe nje.
Bila kufafanua, Rais Samia alisema: “Tukitoa mwanya ndugu zangu, tukipitisha wale wanaotaka ‘na mie niwemo’ ndiyo tunapata wale wanaokwenda huko, chama kinakuwa Gwajimanized. Kwa vyovyote vile, tusigwajimanize chama chetu, magwajima tuyaache nje, hamna kuoneana aibu wala haya.”