Waziri Gwajima afungua dawati la jinsia stendi ya Magufuli, asema…

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dorothy Gwajima akizungumza na wakazi wa mbezi na viunga vyake leo Juni 30, 2025 wakati wa uzinduzi wa Dawati la Huduma za Kijamii kwenye stendi ya Mabasi Mbezi Magufuli
Muktasari:
- Serikali yaanzisha madawati ya jinsia katika vituo vya mabasi na bandari kulinda watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema kuna umuhimu wa kuanzisha madawati ya jinsia katika vituo vyote vya mabasi na bandari nchini ili kusaidia kuwatambua na kuwaokoa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, hususan wenye mahitaji maalumu.
Dk Gwajima amesema hayo leo Jumatatu Juni 30, 2025 katika uzinduzi wa dawati la huduma za kijamii uliofanyika Stendi ya Mabasi Mbezi Magufuli, jijini Dar es Salaam.
Amesema hatua hiyo inalenga kukabiliana na ongezeko la watoto wanaojikuta wakifanya kazi mitaani zisizowahusu, jambo alilosema linatokana na wazazi na walezi kukosa uwajibikaji katika malezi ya familia zao.

"Tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi limekuwa ni changamoto kubwa katika jamii. Watoto hawa hujikuta wakifanya kazi kama kuosha magari, kuokota makopo, kuuza bidhaa barabarani au kuombaomba mitaani. Wengine hata huajiriwa katika nyumba za watu ambako hukumbana na vitendo vya unyanyasaji," amesema Dk Gwajima.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2025, jumla ya watoto 10,782 wameokolewa kutoka katika mazingira hatarishi na kuwekwa kwenye mazingira salama.
Amesema uzinduzi wa dawati hilo la kijamii katika Stendi ya Mbezi Magufuli ni mfano wa madawati mengine yaliyoanzishwa katika vituo mbalimbali nchini, ambapo mpaka sasa tayari kuna madawati 14 yaliyosimikwa katika mikoa 11 hapa nchini.

Aidha, amewahimiza wazazi na walezi kushirikiana na Serikali katika utatuzi wa migogoro ya kifamilia kwa njia ya kuwapeleka watoto wao serikali za mitaa ili kupata msaada wa kitaalamu.
"Jamii inapaswa kuelewa kuwa malezi ni jukumu la pamoja. Serikali za mitaa zina wataalamu wa huduma za jamii ambao wanaweza kusaidia familia zinazopitia changamoto," amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, Felix Wood amesema Serikali ya Uingereza ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanapatiwa msaada na ulinzi unaostahili.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Railway Children Africa (RCA), Mary Gatama amesema ni heshima kubwa kwa shirika lake kushiriki katika uzinduzi huo, akisisitiza kuwa jukumu la kuwalea watoto ni la jamii nzima, si la Serikali pekee.
Amewataka wananchi kushirikiana kwa dhati katika kuisaidia Serikali kuwahudumia watoto hao, huku akiahidi ushirikiano wa moja kwa moja kutoka kwa shirika lake katika kuendeleza juhudi hizo.

Dereva wa bajaji kwenye stendi hiyo, Twalibu Urasa amesema ni jambo la furaha kuona uwepo wa dawati la jinsia, maana wanayajua matatizo ya watoto hao wanaoishi mitaani.
Amesema anashuhudia watoto wakifanya kazi za hatari kama vile kuuza bidhaa barabarani, kuosha magari, na hata kuombaomba, huku wakijiuliza kuna namna gani wanaweza kuwasaidia ili waepuke hatari zinazowakabili.