Polisi yatumia mabomu ya machozi kutawanya waumini wa Askofu Gwajima, KKAM

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetumia mabomu ya machozi kutawanya waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima na wale wa Kanisa la Kiluthel Afrika Mashariki (KKAM).
Waumini hao waliungana na kuendelea na ibada leo Jumapili Juni 29, 2025 kwenye kanisa la KKAM lilipo katikati ya kituo cha Kibo na Corner jijini Dar es Salaam.

Wakati ibada ikiendelea saa 5:42 asubuhi gari la polisi ilifika eneo hilo na kuegeshwa pembezoni mwa barabara na waliomo ndani hawakushuka, huku gari nyingine nne zikiwa zimeegeshwa umbali takribani wa mita 200 kutoka kanisani hapo.
Ilipofika saa 6:00 mchana baada ya ibada, waumini hao walitoka upande wa eneo la kanisa na kusogea pembezoni mwa barabara ya mchepuko wakiwa na mabango.
Polisi iliwaamuru kutawanyika na waumini hao kueleza kutorudi nyuma wakipaza sauti wanataka uhuru wa kuabudu, kabla ya gari za polisi zilizokuwa upande wa pili kusogea na kuwatawanya kwa kupiga mabomu ya machozi.
Waumini kadhaa wamekamatwa huku waliokuwa wakaidi wakikumbana na kichapo na kupakizwa kwenye magari ya polisi.
Hadi kufika saa 6:45 mchana eneo lote la kanisa la KKAM lilikuwa limesafishwa, huku waumini wachache ambao waliponyoka na kukimbia wakiwa umbali wa kanisa wakisikilizia kinachoendelea.

Waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Gwajima wameamua kwenda kusali Kanisa la KKAM baada ya kanisa halo Juni 3, 2025 kufutwa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa kutokana na kukiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.”
Kanisa la KKAM lipo karibu na Kanisa la Ufufuo na Uzima, Ubungo jijini Dar es Salaam. Uongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima umefungua kesi Mahakama Kuu, Masjala ya Dodoma kupinga uamuzi huo wa Serikali.
Habari zaidi endelea kufuatilia Mwananchi