Waumini wa Askofu Gwajima waizidi mbinu Polisi, waibukia kanisa la KKAM

Muktasari:
- Wakati waumini hao na wengine wa kanisa hilo wakiendelea na ibada, asubuhi ya leo Jumapili, Juni 29, 2025 gari la polisi ilifika na kuegeshwa pembeni ya eneo la kanisa bila waliomo ndani kushuka.
Dar es Salaam. Baada ya Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kudhibiti eneo lote la pembezoni mwa barabara ya kutoka Ubungo maji hadi Kibo kutawanywa waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima, waumini hao wameibukia kwenye Kanisa la Kiluthel Afrika Mashariki (KKAM) na kuendelea na ibada.
Kanisa hilo lipo jirani la makao makuu ya lilipokuwa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Ubungo Kibo, Dar es Salaam.
Wakati waumini hao na wengine wa kanisa hilo wakiendelea na ibada, asubuhi ya leo Jumapili, Juni 29, 2025 gari la polisi ilifika na kuegeshwa pembeni ya eneo la kanisa bila waliomo ndani kushuka.

Pia umbali wa kama mita 200 kutoka inapoendelea ibada hiyo kuna magari manne ya polisi wenye silaha pia yalikuwa yameegeshwa jirani na mataa ya kituo cha Corner.
Juni 3, 2025, Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa alitangaza kulifuta kanisa hilo kutokana na kukiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.
Tayari kanisa hilo, limefungua kesi Mahakama Kuu, Masjala ya Dodoma kupinga uamuzi huo.

Kwa wiki mbili mfululizo kila Jumapili, waumini wamekuwa wakifika maeneo ya kanisa hilo wakijikusanya na kuendesha maombi huku Polisi ikiwa inaendelea kuimarisha ulinzi katika kanisa hilo ambalo limezungushiwa utepe kuzuia mtu yeyote kuingia.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea katika Kanisa la KKAM