Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge ‘darasa la saba’ wanavyoacha alama bunge la 12

Muktasari:

  • Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, inampa mtu sifa za kuwa mbunge hata kama hakuwahi kusoma katika mfumo rasmi wa elimu ya msingi ilimradi mhusika ajue kusoma na kuandika katika lugha mbili ama Kiingereza au kwa Kiswahili.

Dodoma. Sifa mojawapo kwa Mtanzania anayetaka kugombea katika kiti cha ubunge wa jimbo au viti Maalum, ama udiwani ni kujua kusoma na kuandika hata kama hatakuwa na cheti cha elimu ya kiwango chochote.

Sifa hizo ni tofauti na zile zinazompasa kuwa nazo mtu anayetaka kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pamoja na mambo mengine ni lazima mtu huyo awe na elimu ya kiwango cha shahada au elimu inayofanana na hiyo.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, inampa mtu sifa za kuwa mbunge hata kama hakuwahi kusoma katika mfumo rasmi wa elimu ya msingi ilimradi mhusika ajue kusoma na kuandika katika lugha mbili ama Kiingereza au kwa Kiswahili.

Kazi nyingi kwa sasa hata zile ambazo hazina mishahara mikubwa zimekuwa na viwango vya kuwekewa vigezo kwa kuwataka watu wawe wamesoma walau kiwango cha kuanzia kidato cha nne.

Ndiyo maana hadi leo wawakilishi katika vikao vingi vya uamuzi ikiwemo bungeni bado wapo katika kiwango cha elimu ya msingi na kwa sehemu kubwa michango yao inatambulika na kuthaminiwa.

Bunge la 12 linamaliza kipindi muhula wake wa miaka mitano waliodumu madarakani ili kupisha uchaguzi mwingine ambao unatarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Bunge hili lilikuwa na wabunge wengi ambao walijitanbulisha kuwa ni darasa la saba ingawa ingekuwa vigumu kuwatambua kutokana na uwezo mkubwa waliokuwa nao katika kujenga hoja.

Miongoni mwao walikuwemo Juma Kishimba (Kahama), Joseph Kasheku Musukuma (Geita Vijiji), Livingston Lusinde Maarufu Kibajaji (Mvumi), Nicodemus Maganga (Mbogwe) na Deo Sanga wa Makambako.

Misimamo yao na jinsi walivyojenga na kuibua mijadala yenye tija, baadhi walitunukiwa vyeo vya kisomi ikiwemo Profesa na daktari.

Siyo wabunge hao pekee wenye kiwango cha chini kwa elimu, bali ndiyo waliojiweka hadharani kuhusu elimu yao ingawa wote walikiri katika kushindania kusomesha watoto wao hadi elimu ya juu.

Watano hawa katika lugha ya kawaida tunaweza kusema 'walikiwasha' na waliweza kujenga hoja ambazo zimedumu kuwa gumzo ndani ya chombo hicho cha uwakilishi katika utungaji wa sheria.

Watatu kati ya wabunge hao, ni wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM huku mmoja akiwa Mwenyekiti wa CCM wa mkoa, mwingine aliwahi kuwa kwenye nafasi hiyo kabla ya kuwa mbunge.


Kishimba alifunika

Katika orodha ya wabunge wa kundi hilo, Kishimba anamaliza Bunge la 12 akiwa ameibuka hoja nne ambazo zilipelekea akabatizwa cheo cha Profesa huku akililia mabadiriko makubwa katika mfumo wa elimu.

“Mheshimiwa Spika, nani aliyesema ubungo wa mwanadamu unajifinza kwa mwaka mzima darasa moja, kwa nini tunawachelewesha vijana kumaliza elimu ya msingi,” alisema Kishimba.

Hoja yake ililenga kuwepo na utaratibu wa kuibua vipaji hasa kwa watoto wenye uwezo mkubwa ambapo ingesaidia mwenye kujua mambo kwa haraka akiwa shuleni wahusika wampaishe haraka aruke madarasa na kumaliza masomo ili akasaidia wazazi wake.

Hoja nyingine ya Kishimba ni kutaka Serikali iruhusu Kilimo cha bangi ili wakulima wafaidike kwani zao hilo lina fedha kama litauzwa kihalàlli.

Kishimba anapinga uzio la zao hilo alieleza wasomi wameshindwa kufanya utafiti kwamba zao hilo lingesaidia kuongeza uchumi kwa ulipaji wa kodi na pato la mkulima.

Huyu ndiye Kishimba aliyekuja na hoja ya wazazi kutunzwa na watoto wao baada ya kuwasomesha na wasipofanya hivyo washitakiwe mahakamani.

“Mheshimiwa Spika, wazazi wanawatunza na kuwasomesha watoto kwa gharama kubwa, lakini wakitoka shule wanakuja mzazi amefilisika lakini wanakataa kuwatunza, hii siyo sawa,” anahoji Kishimba.

Kwa maono yake, anaamini Serikali inawaonea wazazi kwa kuwacheleweshanvijana wao na sababu ni kuwa wazazi na walezi wanatumia gharama kubwa kusomesha watoto wao lakini mwisho wa siku mtoto anarudi na karatasi moja (cheti) ambacho hakimpi dhamana ya kukopa huku akiwa hawezi hata kuchunga ng'ombe wala kulima.

Aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtangaza Kishimba kwa kumpa jina la Profesa kutokana na uwezo wa kujenga hoja na kuzisimamia na hasa kwenye mijadala ihusuyo elimu.

Musukuma

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma anamaliza akiwa amebeba ujasiri wa kusema hadharani kile kinachokuwa kwa faida ya umma lakini Mawaziri waliojisahau hawatamsahau.

Musukuma ambaye aliwaka kung'aka kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba kuhusu Bwawa la Mwalimu Nyerere, baada ya kutoka hadharani kumwambia hana msaada zaidi ya kurukaruka.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa CCM Mkoa wa Geita, anamaliza Bunge kwa hoja ya mbunge mwenzake Askofu Josephat Gwajima(Kawe) ambaye kanisa lake limeingia kwenye misukosuko na Serikali na mara kadhaa wabunge wanamwamini Gwajima kutokana na uwezo wa kupanga hoja lakini Musukuma amejaribu kupambana naye.

Kwa upande wake Nicodemus Maganga, amekuwa na kauli tata mara nyingi akieleza kujiamini zaidi huku akiliambia Bunge kuwa hajawahi kufeli mtihani wowote alioufanya.

Hata hivyo, mara kadhaa amekuwa akikutana na maagizo ya Spika kutaka afute kauli zake kwani amekuwa akizungumza wakati mwingine hata yale ambayo kwa wakati huyo hayakupaswa kuzungumzwa bungeni.

Mbunge Livingstone Lusinde, naye amekuwa akitumika kama kiraka katika hoja za Serikali na wapinzani inapotokea mkwamo wa mvutano kati ya Serikali na wabunge.

Lusinde, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, anatambulika kama mtu wa vijembe kwa wabunge wa upinzani kwani majibizano yake ndani ya mbunge humtenganisha kwa uwezo wake na wabunge wengine kwa namna ya kukitetea chama chake (CCM).

Mbali na hoja aliyowahi kuibua ya kumtaja Hayati John Magufuli (Rais wa awamu ya tano) alipotaka aongezewe muda, Mbunge wa Makambako, Deo Sanga, yeye anamaliza kipindi hiki kwa kuweka rekodi ya msemo wake wa mabi na mabi, akimaanisha mabilioni.

Sanga ambaye uchangiaji wake huwavuta wengi kutokana na sauti yake ya juu, amekuwa na misimamo chanya kuhusu chama chake hata ndani ya Bunge. Ni mbunge ambaye kwa sasa pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe.

Wabunge hao wote wametangaza kurudi tena katika uchaguzi mkuu wa Oktoba huku Maganga akitamba kwamba ataweka rekodi ya ushindi ambayo haijawahi kutokea kwake.

Wabunge Musukuma na Sanga wamekuwa wakipiga vijembe kuwa wapo watu wanaonyatia na kuonya kuwa haitawezana ‘fisi’ kuachiwa mnofu wakati bado kuna uhitaji wa mnofu huo.

Wakati huohuo, Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ilikuwa imejadiliwa na Bunge la Katiba mwaka 2014, ilibaki na sharti hilohilo la sifa za kujua kusoma na kuandika kwa nafasi za uwakilishi, hivyo hata ingepitishwa bado inawapa nafasi.