Rais Samia amwagia sifa Dk Tulia

Rais Samia Suluhu Hassan akilihutubia bunge kabla ya kulivunja Bunge la 12, jijini Dodoma leo Juni 27, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
- Rais Samia ameeleza hayo leo Ijumaa Juni 27, 2025 wakati akihutubia Bunge jijini Dodoma. Mkuu huyo wa nchi analivunja Bunge la 12, ikiwa ni maandalizi ya kwenda katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ameliongoza vyema Bunge la 12 na kufanikisha kukamilika kwa jumla ya mikutano 19 ya Bunge hilo.
“Najua haikuwa kazi rahisi, lakini pia ni kazi nyepesi kwako, najua kwenye wengi kuna wengi na kila mmoja ana kichwa chake. Haikuwa kazi rahisi kwako ila kwa uhodari mkubwa umeweza kufikisha mashua yetu bandarini,” amesema Rais Samia.
Rais Samia ameeleza hayo leo Ijumaa Juni 27, 2025 wakati akihutubia Bunge jijini Dodoma. Mkuu huyo wa nchi analivunja Bunge la 12, ikiwa ni maandalizi ya kwenda katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba baadaye.
Mkuu huyo wa nchi, amesema katika historia ya Tanzania, Dk Tulia ni mwanamke wa pili kushika wadhifa huo, akitanguliwa na Spika wa zamani, Anne Makinda aliyeongoza Bunge la 10.
“Hakika haujatuangusha wanawake wenzio, mheshimiwa Spika uzoefu wa kitaifa na kimataifa, umehakikisha kazi hii inafanyika kwa viwango na kuendelea kulijengea heshima Bunge letu,” amesema Rais Samia.
Mbali na hilo, Rais Samia amempongeza pia Dk Tulia kwa kutekeleza majukumu yake sambamba na kuwa rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani, (IPU), akisema huko nako ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.
“Tunakupongeza sana kwa kutumia vema wadhifa huo,” amesema Rais Samia.
Dk Tulia, kabla kushika wadhifa huo, alikuwa Naibu Spika, lakini baada ya Job Ndugai kujiuzulu alichaguliwa kushika nafasi hiyo, Februari mwaka 2022.