Maelekezo ya Rais Samia kwa Jeshi la Polisi matukio ya watu kupotea

Rais Samia Suluhu Hassan akilihutubia bunge kabla ya kulivunja Bunge la 12, jijini Dodoma leo Juni 27, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi
Rais Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi kuongeza jitihada kukomesha matukio ya watu kupotea yanayoripotiwa sehemu mbalimbali nchini.
Amesema Serikali imeendelea kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza miundombinu, akieleza vituo vya polisi 472 vimejengwa hadi ngazi ya kata na shehia.
“Kasi ya kuwabaini wahalifu na kuwafikisha mahakamani imeongezeka, jambo ambalo hatujafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani, lazima nazo tuendelee kulifanyia kazi,” amesema na kuongeza:
“Nalielekeza Jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kukomesha matukio ya watu kupotea.”
Amesema Serikali imeboresha makazi ya askari na vitendea kazi, ikiwamo magari na pikipiki kwa ajili ya kazi za utawala na operesheni. Aidha, askari 16,000 wameajiriwa huku maofisa na wakaguzi 13,633 wakipandishwa vyeo.
“Natoa pongezi nyingi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya. Hatuna budi kutambua kwamba, uhalifu unaozuiliwa kwa jitihada za Jeshi la Polisi ni mkubwa kuliko unaofanyika,” amesema.
Amesema hayo leo Juni 27, 2025 bungeni jijini Dodoma alipolihutubia kuhitimisha shughuli za Bunge la 12.