Bunge laridhia kugawa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, uanzishwaji AFC

Muktasari:
- Bunge limehitimisha mkutano wa 19 wa Bunge la 12, kwa kupitisha maazimio mawili la mkataba wa uanzishwaji wa Shirika la Fedha la Afrika (AFC) na kufanya marekebisho ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Dodoma. Bunge limeridhia azimio la mkataba wa uanzishwaji wa Shirika la Fedha la Afrika (AFC) wa mwaka 2007 ambao unatoa kinga dhidi ya upekuzi, ukamataji, utaifishaji na aina nyingine za kukamata, kuchukua au kuzuiliwa kwa mali za AFC kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi mwanachama.
Mbali na hilo, Bunge limeridhia azimio la kufanya marekebisho ya mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambapo eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,617 limemegwa kuwarejeshea wananchi, Pori la Akiba Selous na kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo.
Akiwasilisha azimio hilo bungeni leo Alhamisi, Juni 26,2025, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema mkataba huo inahusu kinga ya misamaha na upendeleo wa kidiplomasia na kwamba nchi itakayojiunga na shirika hilo itatakiwa kuipa AFC hadhi, kinga, misamaha na upendeleo wa kidiplomasia.
Amesema mkataba huo unatoa kinga kwamba, AFC haiwezi kushtakiwa na nchi mwanachama, mwanahisa au mtu yeyote kuhusu masuala ambayo yanasimamiwa na mikataba ya usuluhishi au masuala binafsi.
“Ibara ya 10 inahusu uhuru wa shughuli za AFC ambapo nchi wanachama wanapaswa kuondoa vizuizi vya usimamizi vinavyohusu masuala ya fedha na shughuli za AFC,” amesema.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana akiwasilisha bungeni jijini Dodoma leo Juni 26, 2025 azimio la bunge la kuridhia marekebisho ya mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dk Mwingulu amesema mkataba huo unatoa kinga ya nyaraka za AFC dhidi ya upekuzi au kutolewa isipokuwa pale nyaraka zinapohitajika na mahakama au mashauri ambayo AFC linahusika.
Pia mkataba huo unatoa kinga, upendeleo na misamaha ya kodi zote kwa watumishi, wawakilishi, wakurugenzi, viongozi na washirika wa AFC wakiwemo Watanzania wakati wakitekeleza wajibu wa AFC.
Hata hivyo, Dk Mwigulu amesema mkataba unaondoa kinga na upendeleo ambapo Bodi ya Wakurugezi na Mtendaji Mkuu wa AFC wana mamlaka ya kuondoa kinga na upendeleo kwa mtendaji mkuu, watumishi au mshauri elekezi mtawalia.
Amesema mkataba huo umebainisha ulazima wa nchi kutoa msamaha wa ushuru wa forodha na kodi zote kwa AFC, mali, mapato, shughuli zote za uendeshaji na fedha za AFC.
Ametaja shughuli hizo pamoja mawakala wanaofanya malipo kwa AFC kupewa msamaha wa kodi zote zilizopo katika sheria za nchi au zitakazoainishwa baadaye katika sheria za kodi.
“Misamaha hiyo ni pamoja na msamaha wa kodi kwenye mali, akiba, mtaji, gawio, mikopo, dhamana, uwekezaji, riba, malipo ya uwakala, faida, ada, mapato na fedha zozote zitakazopatikana au mapato kutokana na uwekezaji wowote utakaofanywa na AFC,” amesema.
Amesema msamaha wa kodi utakaotolewa utakuwa sehemu ya gharama za utekelezaji wa mkataba endapo AFC itapata hadhi ya kidiplomasia.
Dk Mwigulu amesema ilianzishwa kwa lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya viwanda kwa nchi za Afrika kama Bara na kwa nchi moja moja ambapo hadi Machi, 2025 jumla ya nchi 44 za Afrika zilikuwa zimejiunga na shirika hilo.
“Hadi Desemba, 2024, shirika lilikuwa na mali (assets) zenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 14.4 na hisa zisizo na riba (equity) zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.9 katika miradi mbalimbali barani Afrika katika sekta za miundombinu, nishati, uchukuzi, mawasiliano na viwanda.
“Kwa mujibu wa taarifa ya fedha ya mwezi Septemba, 2024, tangu kuanzishwa kwake Shirika hilo limegharamia dola za Marekani bilioni 14.79 katika miradi kwa nchi wanachama 34,” amesema Dk Mwigulu.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mjumbe wa kamati hiyo, Bahati Ndingo amesema ili nchi iweze kufaidika na AFC inatakiwa kujiunga kama mwanachama pekee au mwanachama mwenye hisa katika shirika hili.
Hata hivyo, amesema kwa mujibu wa maelezo ya Serikali, Tanzania inapendekeza kujiunga kama mwanachama pekee.
“Kamati inatoa angalizo la Serikali kuhakikisha kuwa Ibara ya 7 hadi 15 ya mkataba ambazo zinahusu kinga, upendeleo na misamaha ya kikodi kwa AFC pamoja na watumishi wake zinawekewa maangalizo ili zisikinzane na sheria, kanuni na taratibu za nchi,” amesema.
Ametaka Serikali ikajifunza kwa nchi za Liberia, Ethiopia na Somalia ambazo zimejiunga na shirika hilo kwa kuweka angalizo.
Hifadhi ya Taifa ya Nyerere yamegwa
Wakati huo huo, Bunge limeridhia azimio kuhusu kufanyika kwa marekebisho ya mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambapo eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,617 limemegwa kuwarejeshea wananchi, Pori la Akiba Selous na kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo.
Akisoma azimio hilo, Waziri wa Maliasili na Maliasili, Dk Pindi Chana amesema baada ya uamuzi huo mpaka wa hifadhi hiyo utasomeka kwa ukubwa wa kilometa za mraba 29,276 kutoka kilomita za mraba 30,893 ilivyokuwa awali.
Dk Chana amesema wamerekebisha mpaka wa Hifadhi ya Taifa Nyerere kwa kumega ukubwa wa kilometa za mraba 195.64 kwenda Pori la Akiba Selous na kilometa za mraba 259.55 kwenda kwenye vijiji na eneo la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Pia, amesema kilometa za mraba 687.46 zitakwenda Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori huku 474.35 zitakuwa ni Hifadhi ya Msitu wa Taifa kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mzava ameshauri Serikali kuhakikisha kwamba, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na taasisi nyingine zote za Serikali husika, zinashirikishwa kuandaa mipango endelevu ya matumizi bora ya ardhi hiyo.
“Hatua hii ambayo Serikali inapendekeza kuchukua, ni hatua ambayo inatarajiwa kupanua wigo wa fursa za kimaendeleo, shughuli za kiuchumi na uwekezaji,” amesema.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni jijini Dodoma leo Juni 26, 2025, azimio la bunge la kuridhia mkataba wa uanzishwaji wa Shirika la Fedha la Afrika. Picha na Edwin Mjwahuzi
Mzava amesema kwa kuzingatia suala hilo, kamati inashauri kwamba, Serikali ishirikishe kikamilifu kamati za ardhi za vijiji, ili kuepuka uwezekano wa kutokea migogoro ya mgawanyo wa ardhi na kuendelea kurekebisha mpaka katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
“Katika kushughulikia azimio hili, kamati imebaini kuwa kuna vijiji na maeneo ya mipaka ya utawala yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambayo hayajaguswa na azimio hili lakini yana migogoro ya mipaka,” amesema.
Mzava ameshauri kuwa Serikali iendelee kufanya tathmini ya kina na kuja na azimio ambalo litashughulikia migogoro yote ya vijiji na maeneo mengine ambayo yanazunguka hifadhi hiyo.
Amesema katika kushughulikia migogoro hiyo, Serikali ihakikishe inawashirikisha wananchi na wawakilishi wanaotoka katika maeneo hayo.
Pia, ameshauri kurekebisha mipaka katika hifadhi zingine za Taifa kwa kuwa kamati imebaini kuwa katika baadhi ya maeneo yanayozunguka hifadhi nyingi za Taifa yana migogoro ya mipaka kati ya vijiji na maeneo mengine ya utawala.