Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mradi wa Dege Eco Village ndoto iliyofutika, Serikali yasisitiza uuzwe

Muktasari:

  • Mradi wa Dege Eco Village uliokuwa unatekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwenye eneo la ekari 302, una nyumba 3,750 zilizokuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi ulisimama na kuibua maswali lukuki.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imefuta ndoto ya kuendeleza mradi wa Dege Eco Village uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, wenye thamani ya zaidi ya Sh1.3 trilioni uuzwe kwa mwekezaji mwingine, baada ya kujiridhisha kuwa itakuwa ni hasara kuendelea nao.

Kauli hiyo inatolewa takribani miaka miwili imepita tangu, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulipoeleza ulikuwa katika hatua za mwisho kuuza kwa mzabuni mwaka 2023.

Mradi huo uliokuwa unatekelezwa na NSSF wenye eneo la ekari 302, una nyumba 3,750 zilizokuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Ujenzi wake ulianza mwaka 2014 na hadi ujenzi unasimama Januari 2016, ilidaiwa kutafuna zaidi ya Sh179 bilioni ambazo zilifanya kutokamilika kwa nyumba za kifahari, hoteli, maduka makubwa, eneo la wazi la mapumziko, baa, shule, hospitali, kumbi za mikutano, nyumba za ibada na migahawa.

Mradi huo umekuwa na maswali mengi kutoka kwa wabunge na wananchi ambapo kwa takriban miaka tisa Serikali na NSSF wamekuwa wakielekeza kutafuta mwekezaji wa kuununua mradi huo, ambao hadi Oktoba 31, 2023 ulikuwa na thamani ya dola 220 milioni (Sh501 bilioni).

Kupewa kisogo kwa mradi huo kumeelezwa leo Alhamisi, Juni 26, 2025 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi.

Katika swali la msingi Kisangi ameuliza, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha majengo ya Mradi wa Dege Beach-NSSF Mbweni kwa kuwa ni wa muda mrefu.

Katika maswali ya nyongeza Mbunge wa Viti Maalumu Ester Bulaya ameuliza ni kwa nini Serikali inatumia fedha za wastaafu vibaya bila kuwapa taarifa na hatua gani zinachukuliwa kwa waliotia hasara uwekezaji huo.

Akijibu maswali hayo, Katambi amesema: “Serikali imefanya tathmini ya mradi wa Dege Eco Village uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam na kujiridhisha kuwa itakuwa ni hasara kuendelea na ujenzi wa mradi huo. Hivyo, imeamriwa mradi huo uuzwe kwa wawekezaji wengine.”

“Kwa sasa Mfuko bado unaendelea na taratibu za kuwakaribisha wawekezaji wenye nia ya kutwaa eneo hili na kueleza nia ya kuununua mradi huo.”

Kuhusu tathmini kabla ya kuanzishwa, Katambi amesema kuanzishwa kwake kulitegemea mahitaji ya wakati huo, kwani uwekezaji hufanyika ili kulinda fedha za wastaafu pale thamani ya fedha inaposhuka.

Katika hatua nyingine, Katambi amesema uamuzi wa kuhamishia makao makuu Dodoma nao uliathiri mwendelezo wa mradi huo, kwani watumishi wengi walilazimika kuhamia Dodoma.

Wakati Katambi akieleza hayo, miaka takribani miwili nyuma, Septemba 25, 2023 NSSF ilieleza hadi kufikia Oktoba 31, 2023 mradi huo ungekuwa umekamilisha hatua zote za uuzwaji wake kwa karibu Dola 220 milioni za Marekani (zaidi ya Sh501 bilioni).

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mkuu wa wa NSSF, Masha Mshomba katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kwa uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mshomba alisema mradi huo ungeuzwa kama ulivyo, ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa Bodi ya Mfuko na Serikali ili kurudisha fedha za wanachama zilizowekezwa awali katika mradi huo.

Kwa mujibu Mushomba, hadi uamuzi wa kuuzwa mradi huo unafikiwa tayari ulikuwa umeshatumia zaidi ya Sh330 bilioni na kwamba kwa mnunuzi waliyekuwa wamempata wangekuwa wamepata faida.

"Kwa sasa mfuko kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali unakamlisha taratibu za zabuni baada ya kukamilika kwa hatua ya tathmini ya zabuni na maafikiano ya bei. Matarajio ni kusainiwa kwa mkataba wa mauzo ya mradi huu kabla ya Oktoba 31, 2023," alisema Mshomba.

Bila kumtaja mnunuzi kutokana na taratibu kubana, alieleza kuwa wanaamini kuwa mnunuzi angeendelea kama ilivyokuwa imekusaudiwa.

Hata hivyo, hadi majibu ya Serikali yanatolewa bungeni hakuna taarifa zozote zilizotolewa kuhusu maendeleo ya mauaziana hayo.