Mchakato zabuni uuzaji mradi wa Dege waendelea

Muktasari:
- Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba amesema thamani ya mfuko huo imeongezeka na kwamba, fedha za wanachama ziko salama.
Dar es Salaam. Mchakato wa kumsaka mzabuni kwa ajili ya uuzaji wa mradi wa Dege Eco Village uliopo Kigamboni, Dar es Salaam uliogharimu Sh330 bilioni, bado unaendelea.
Mradi huo ulianzishwa na NSSF mwaka 2014 unahusisha majengo ya hoteli, kumbi za mikutano, eneo la wazi la mapumziko, shule, hospitali na nyumba za kifahari.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema mradi huo uliamuliwa uuzwe baada ya kufanyika tathmini mwaka 2020 na kwamba uamuzi huo unalenga kurudisha gharama zilizotumika.
"Hivi sasa tulitangaza zabuni ambayo bado ipo katika mchakato na endapo ikatokea kwamba hatujapata mtu, ambaye amefika bei ya kurudisha ile gharama maana yake ni kuwa tutatangaza tena kwa mara nyingine," amesema Masha.
Amesema kwa namna ambavyo wawekezaji wanaongezeka nchini, kuna uhakika kwamba wataweza kununua mradi huo katika kiwango kitakachokuwa na manufaa kwa NSSF.
Ameongeza kuwa kuuzwa kwa mradi huo kutakuwa na faida kubwa kwa wanachama wa mfuko na Taifa kwa kuwa kutaepusha hasara ambazo zingeweza kupatikana iwapo wangeendelea na mradi huo.
Mshomba ametumia nafasi hiyo pia kuwahakikishia wanachama kuwa mfuko huo upo salama na kwamba, thamani yake imeongezeka hadi kufikia Sh6.6 trilioni Desemba, mwaka jana. Hilo ni ongezeko la asilimia 36 kwani hadi kufikia Machi 2021 thamani ya mfuko ilikuwa Sh4.7 trilioni.
“Ongezeko hili linatokana na michango ya wanachama na mapato yatokanayo na uwekezaji, hivyo ukuaji huu wa mfuko unathibitisha kuwa NSSF ipo imara na endelevu kwa ajili ya utoaji huduma kwa wanachama wake,” ameongeza Mshomba.
Kauli hiyo ya Mshomba kuhusu michango inatokana na ukweli kwamba, katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, mfuko unatarajia kukusanya michango ya Sh1.6 trilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 14 ukilinganisha na Sh1.4 trilioni zilizokusanywa kwa mwaka 2021/22.
Kuhusu mapato yatokanayo na uwekezaji nayo yanatarajiwa kupanda kutoka Sh500 bilioni hadi Sh700 bilioni kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
SAHIHISHO/UFAFANUZI:Jana katika ukurasa wetu wa Instagram tuliandika kichwa cha habari kuwa: NSSF yakosa tena mteja mradi wa Dege. Sahihi ni kuwa mchakato bado unaendelea ili kumpata mzabuni atakayefikia kiwango cha fedha kilichopangwa na mfuko huo kuuza mradi husika.
Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.
Mhariri