Polisi ilivyobadili mbinu kudhibiti waumini kanisa la Askofu Gwajima

Muktasari:
- Juni 2, 2025 Serikali ilitangaza kulifuta Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima kwa madai limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.
Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imebadili mbinu ya kuwadhibiti waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima.
Tofauti na awali, tangu kanisa hilo lilipotangazwa kufutwa na polisi kulizungushia utepe kuashiria kutoruhusu waumini kuendelea na ibada, leo Jumapili Juni 22, 2025 utaratibu wa ulinzi kanisani hapo umebadilika.
Juni 2, 2025 Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa alitangaza kulifuta kanisa hilo kutokana na kukiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, “kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.”

Barua ya Kihampa kwenda kwa Askofu Gwajima, nakala ilitumwa kwa Mkuu wa Polisi Tanzania (IGP), Camilius Wambura kwa ajili ya utekelezaji wa uamuzi huo.
Uongozi wa kanisa hilo lenye matawi zaidi ya 2,000 nchini umefungua kesi inayoendelea Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, wakiomba amri ya muda ya kuondoa zuio lililowekwa dhidi ya kuendelea na shughuli zake za kidini.
Tangu uamuzi huo wa Serikali kulifuta, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, inayoongozwa na Kamanda Jumanne Muliro imekuwa ikifanya doria kwenye kanisa hilo lililopo Ubungo, Kibo jijini Dar es Salaam.
Leo Juni 22, 2025 ambayo ni Jumapili ya tatu tangu waumini wazuiwe kuendelea na ibada na siku ya 20 tangu kanisa hilo litangazwe kufutwa, Mwananchi imeshuhudia mbinu tofauti ya Polisi kudhibiti waumini na kuimarisha doria katika kanisa hilo.
Mwananchi iliyofika saa 2:02 asubuhi kwenye eneo hilo imeshuhudia ulinzi wa Jeshi la Polisi ukiwa umeanzia mtaa wa Msewe, mita zaidi ya 300 kutoka yalipo makao makuu ya kanisa hilo, Kibo jijini hapa.
Katika njia panda ya Mtaa wa Msewe, kulikuwa na takriban polisi 10 baadhi wakiwa na silaha za moto kwenye defenda wakiendelea kuimarisha ulinzi.

Eneo hilo ni upande wa pili wa kanisa ambako ndipo waumini wa kanisa hilo wiki iliyopita walikusanyika na kufanya ibada barabarani kabla ya kutawanywa kwa kupigwa mabomu ya machozi.
Mbali na defenda hiyo, mita kama 100 pia wamesimama polisi wawili wenye silaha na mbele kidogo wapo askari wengine wakiwa wamesimama vikundi wawiliwawili hadi watatu wakiwa na bunduki na virungu, utaratibu ukiwa ni huohuo hadi usawa wa lilipo kanisa hilo, kama unaelekea Ubungo Maji.
Polisi hao wamedhibiti eneo lote la Barabara ya mchepuko (Service road) ambayo ipo upande wa pili wa lilipo kanisa.
Katika eneo hilo, hakuna muumini yoyote wala kikundi kilichokusanyika zaidi ya kuruhusu watu kupita na kuendelea na safari zao pasipo kusimama simama.
Katika eneo la kanisa, kuna ulinzi umeendelea ambako polisi wanaendelea kuongezwa kuungana na waliopo kuimarisha ulinzi.
Hadi saa 2:30 asubuhi eneo hilo lilikuwa na basi dogo la polisi, defenda nyingine mbili zenye askari wenye silaha na gari ya maji ya kuwasha ambayo ilikuwepo kwenye eneo hilo tangu Juni 3, 2025 polisi walipozingira kanisa hilo na kutawanya waumini waliokuwa kwenye ibada ya mkesha wa kufunga na kuomba kanisani hapo.
Ilipofika saa 3:32 asubuhi ziliongezwa defenda nyingine tatu zilizokuwa na askari wa kutuliza ghasia wenye kofia nyekundu na gari nyingine aina ya Noah ya polisi yenye askari wenye silaha za moto na virungu wakiwa tayari kwa lolote.
Endelea kufuatilia Mwananchi