Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saa saba hekaheka polisi, waumini wa Askofu Gwajima, mabomu yakirindima

Muktasari:

  • Uamuzi wa kulifuta kanisa hilo la Askofu Josephat Gwajima,  maarufu Kanisa la Ufufuo na Uzima ulitangazwa Juni 2, 2025 na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa akidai limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kile alichoeleza limekuwa linatoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitangaza kulifuta Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church, waumini wa kanisa hilo wamejitokeza kando ya nyumba hiyo ya ibada wakitaka kuingia kusali.

Uamuzi wa kulifuta kanisa hilo la Askofu Josephat Gwajima,  maarufu Kanisa la Ufufuo na Uzima ulitangazwa Juni 2, 2025 na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa akidai limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kile alichoeleza limekuwa linatoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa.

Uongozi wa kanisa hilo lenye matawi zaidi ya 2,000 nchini umefungua kesi inayoendelea Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, wakiomba amri ya muda ya kuondoa zuio lililowekwa dhidi ya kuendelea na shughuli zake za kidini.

Wakati kesi hiyo ikiendelea, polisi wameendelea kusimamia utekelezaji wa Serikali kwa kufutwa kwa kanisa hilo huku Askofu Gwajima kupitia akaunti zake za kijamii, akiwaita waumini kukutana kanisani hapo, Ubungo jijini Dar es Salaam.

Askofu Gwajima ambaye pia ni mbunge wa Kawe (CCM) ameandika: “Waebrania 10:25, wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.” Aidha, akaongeza tangazo jingine: “Kesho (leo) ni Jumapili; Tukutane nyumbani mwa Bwana!.”

Saa saba za hekaheka

Asubuhi ya leo Jumapili, Juni 1, 2025 Mwananchi imefika eneo la kanisa hilo mbili asubuhi na kukuta askari wenye silaha wakiwa wametanda maeneo mbalimbali kuhakikisha hakuna anayeingia kanisani hapo.

Baada ya waumini kukaa kwa makundi askari kwa nyakati tofauti walianza kuwatawanya ingawa baadaye saa nne kuelekea saa tano wakakusanyika mita chache kutoka kanisani, pembeni ya barabara wakaanza kuabudu kwa wingi.

Kadri muda ulivyokuwa ikisonga, waumini waliongezeka kwa makundi. Wakati wakiendelea na ibada pembeni ya barabara askari wakiwa kwenye difenda wakafika eneo hilo kisha kuwaamuru waondoke kwakuwa si eneo salama.

Kwa sauti nyingi waumini hao wakahoji waende wapi na kanisa lao limefungwa. "Mkitaka tuondoke hapa tufungulieni kanisa letu tukaabudu huko" walisikika waumini hao.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina mmoja ya waumini wa kanisa hilo amesema ataendelea kuwepo mahali hapo hadi mwisho wa ibada saa tisa mchana.

"Tumefungiwa tukaabudu wapi? Leo tutaabudu hapa hadi kieleweke hatuondoki," amesisitiza akizungumza kwa sauti kali.

Muumini huyo amesema hataondoka na Jumapili ijayo atashiriki ibada mahali hapo.

Licha ya katazo la polisi kwa wingi waliokuwepo mamia hao wa waumini wakaamua kuingia Barabara ya Morogoro inayokwenda Ubungo Maji usawa wa daraja la Kijazi.

Kwa nyimbo za mapambio na mabango mikononi mwao waumini hao kwa ujasiri wakawa wanaelekea upande huo ambapo wakakutana na askari wametanda barabarani.

Baada ya mzozano wa dakika kadhaa askari wakaanza kuwaondosha barabarani ndipo mabomu ya machozi yakaanza kurindima.

Kila mmoja akashika njia yake ndipo hekaheka ilipoanza. Baadhi ya waumini wakakamatwa na Polisi wakapandishwa kwenye difenda kwa nyakati tofauti.

Jitihada za kumtafuta Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro hazikufanikiwa ili kujua idadi ya waliokamatwa. Vivyo hivyo kwa Askofu Gwajima ambaye alitaka wakutane ‘nyumbani mwa Bwana!’ lakini hadi walipotawanywa kwa mabomu ya machozi saa nane mchana hakuonekana.