Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jina Kanisa la Gwajima laibua mjadala kortini, maombi ya zuio yakataliwa

Muktasari:

  • Jaji amesema amejizuia kushughulikia mawasilisho kuhusu matendo ya mjibu maombi wa tatu (IGP) kwa sababu maombi yaliyopo mbele yake yalijikita katika  amri zilizohusiana na hadhi ya usajili wa kanisa la mleta maombi.

Dodoma. Tofauti ya majina kati ya kanisa linalodaiwa kufutwa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia na lile la Glory of Christ Tanzania Church linalomilikiwa na Askofu Josephat Gwajima, limefanya maombi yao ya zuio kugonga mwamba.

Katika maombi yaliyofunguliwa chini ya hati ya usikilizwaji wa dharura, waombaji waliomba amri ya upande mmoja, mahakama izuie utekelezaji wa barua ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia kulifuta kanisa hilo.

Lakini katika ombi mbadala, waliomba amri kuwa shughuli za kanisa hilo ziendelee kama zilivyokuwa mwanzo (status quo ante) wakati suala la usajili linafanyiwa kazi, kwani hawajapata mawasiliano rasmi.

Kanisa la Askofu Gwajima kupitia Bodi ya Wadhamini, lilifungua maombi dhidi ya Msajili wa Jumuiya ya kiraia kama mjibu maombi wa kwanza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Inspekta Jenerali wa Polisi.

Hata hivyo, katika uamuzi alioutoa leo Juni 13, 2025 baada ya kusikiliza mabishano ya kisheria baina ya mleta maombi na wajibu maombi, Jaji Juliana Masabo wa Mahakama Kuu ameyakataa maombi hayo, kiini kikiwa kanisa gani hasa limefungwa.

Kanisa la The Glory of Christ Tanzania Church ambalo limesajiliwa na mjibu maombi wa kwanza, linaendeshwa kutokea  makao makuu yaliyopo Dar es Salaam na lina matawi 2,000 maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Juni 1, 2025 walianza maombi ya kufunga kwa siku saba kwa ajili ya kuliombea Taifa, lakini wakati wanaendelea na maombi, waliona barua iliyokuwa ikisambaa mitandaoni ikionyesha msajili amefuta kanisa la Glory of Christ Church.

Licha ya kuwapo tofauti za majina, kati ya jina la kanisa la mleta maombi na lile lililofungwa mitandaoni, IGP, akijifanya kutekeleza uamuzi wa Msajili, aliingilia maombi yaliyokuwa yakiendelea na kukamata baadhi ya waumini wa kanisa hilo.

Juni 3, 2025 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro aliitisha mkutano na waandishi wa habari ambao aliutumia kumshauri mleta maombi kama hakubaliani na uamuzi wa msajili akate rufaa.

Ni kutokana na ushauri huo, mleta maombi amekata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na akafungua maombi katika mahakama hiyo akiomba itoe zuio la muda kwa wajibu maombi kuingilia shughuli za ibada katika makanisa hayo.


Hoja za kanisa

Akiwasilisha hoja kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo, wakili Peter Kibatala aliomba kiapo cha Bryson Lema kiwe sehemu ya hoja zake.

Alidai amri au uamuzi wa mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Msajili wa Jumuiya za Kiraia nchini kama ilivyotekelezwa na IGP, imeingia na kuvuruga shughuli za uendeshaji wa kanisa hilo.

Baadhi ya maaskofu wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania, wakiwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kwenye kesi ya kupinga kufutwa kwa kanisa hilo.

Amedai mahakama kuingilia suala hilo ni jambo la muhimu ili kurejesha shughuli za kiimani, yakiwamo maombi ya mfungo wa siku saba ambayo yameingiliwa na kuvurugwa na inaliletea hatari kanisa hilo.

Kibatala amedai kuna hatari ya akaunti za benki za kanisa kusitishiwa huduma kama watabaini limefutwa, hivyo hawataweza kutekeleza majukumu yao muhimu kama kanisa.

Majukumu hayo amedai ni kulipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mishahara na michango ya wafanyakazi katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Amedai ili haki ionekane inatendeka, wamewasilisha ombi kwa mahakama iweze kutoa amri ya zuio la muda kwa mjibu maombi wa kwanza ili uamuzi wake usitekelezwe kusubiri uamuzi wa maombi yao.

“Hii ni kwa sababu amri ya kulifuta kanisa la muombaji haiko katika jina la muombaji, lakini bado imeendelea kutekelezwa na mjibu maombi wa tatu, IGP ambaye sasa analihodhi na kuzuia shughuli,” amedai.

“Kama uamuzi wa Msajili ni kwa ajili ya mleta maombi, bado hajajulishwa rasmi wala hajawahi kupewa notisi yoyote kwamba mjibu maombi anakusudia kulifuta kanisa hilo. Kwa hiyo wameadhibiwa bila kusikilizwa.

“Ni ombi letu kuwa ombi la zuio la muda likubaliwe. Kuhusu ombi mbadala la shughuli ziendelee kama kawaida wakati uamuzi ukisubiriwa, basi nalo mahakama ilikubali,” amedai.


Majibu ya Serikali

Mawakili wa Serikali wakiongozwa na wakili mwandamizi, Narindwa Sekimanga akishirikiana na mawakili Eric Rumisha na Kumbukeni Kiondo, walipinga maombi hayo wakidai amri inayolalamikiwa haina jina la mleta maombi.

Kwa niaba ya wenzake, Rumisha alidai hata barua yenyewe haijasainiwa na haijakabidhiwa rasmi kwa mleta maombi.

“Hivyo mahakama haiwezi kutoa zuio kwa jambo lisilo na athari kisheria,” amedai na kuongeza kuwa, hata amri ya kutaka shughuli ziendelee  ikitolewa itakuwa imeegemea katika uvumi kwa kuwa hakuna uamuzi rasmi.


Uamuzi wa Jaji

Jaji Masabo amesema  kutokuwapo ubishani kuhusu jina la kanisa lililofutwa na lile la muombaji, inamaanisha kama kuna uamuzi wa kufuta kanisa, haumhusu mwombaji.

“Kwa vile hiyo inayodaiwa ni amri haijasainiwa na pia haijakabidhiwa rasmi kwa mleta maombi kama wao wenyewe walivyokiri kwenye kiapo chao, hii maana yake kisheria ni kuwa hakuna amri au uamuzi kutoka kwa Msajili,” amesema.

Amesema katika maombi hayo, ni lazima kile wanachokieleza kionyeshe waziwazi kuwa kuna amri dhidi ya muombaji na imegusa usajili wa kanisa hilo.

Jaji amehoji kwa maelezo yaliyopo, hilo limethibitika?

Alinukuu sehemu ya maelezo ya waleta maombi inayosema: “Mahakama inaombwa kutoa amri kuwa mawasiliano ya Msajili ya Juni 2, 2025 ambayo hadi tunawasilisha maombi hayajawasilishwa rasmi kwa muombaji yazuiwe kusubiri maombi yaliyoko mbele ya mahakama.”

Pia amenukuu kiapo cha mleta maombi kinachoonyesha akieleza kanisa lake linaitwa The Glory of Christ Tanzania Church lakini barua iliyosambaa mitandaoni inaonyesha kanisa lililofutwa ni Glory of Christ Church, yakiwa ni majina tofauti.

Jaji amesema mahakama ni lazima izingatie kile kilichoelezwa na mleta maombi na katika maombi hayo, mleta maombi amekiri waziwazi kuwa barua ya kufutwa kanisa haina jina lao wala haijasainiwa.

Kutokana na hayo, Jaji amekubaliana na hoja za mawakili wa Serikali kuwa ombi la kwanza la mleta maombi la kuomba zuio haliwezi kusimama.

Mawakili wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania, Peter Kibatala na Gloria Ulomi wakiwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kwenye kesi ya kupinga kufutwa kwa kanisa hilo.

Kuhusu ombi la amri mbadala kuwa shughuli za kanisa ziendelee kama zilivyokuwa mwanzo, ni tofauti na zuio ambalo kisheria linafahamika kama Status quo, ambayo ni kutaka hali iliyopo sasa ibaki ilivyo.

Jaji amesema maombi ya kutaka amri ya mahakama kuwa hali ya uendeshaji wa kanisa ibaki kama ilivyokuwa mwanzo inataka kuashiria kuna kufutwa kwa usajili wa kanisa hilo na mahakama inaombwa kubadili uamuzi huo.

Amesema amri zote mbili zisingewezekana kwa sababu tayari mahakama imeshasema barua inayolalamikiwa haina utambulisho wowote wa mleta maombi, hivyo hakuna hatari yoyote iliyopo ya kufutwa kwa kanisa la mleta maombi.

Jaji amesema amejizuia kushughulikia mawasilisho kuhusu matendo ya mjibu maombi wa tatu (IGP) kwa sababu maombi yaliyopo mbele yake yalijikita katika amri zilizohusiana na hadhi ya usajili wa kanisa la mleta maombi.